Maalumu kwa mama yangu.
Ilikuwa tarehe 12th
April 198…, saa mbili usiku jijini Arusha, ilikuwa siku ambayo familia ya
Mesaya Simanga Masakoi na Tiinoi Mashon Kivuyo (Mr & Mrs Mesaya) walipotunukiwa
na Mungu zawadi ya mtoto wa kiume. Najaribu kuvuta hisia zangu juu ya furaha
waliokuwa nao vijana hawa wa enzi zile kwa kufanikiwa kumpata mtoto mwenye afya
njema na ambaye alipofinywa kwenye kisigino cha mguu wake alilia mara tatu
kuonyesha kwamba ni mwanaume rijali.
Mtoto huyu siku ya leo
anatimiza zaidi ya miongo miwili na nusu tangu alipozaliwa. Ni kipindi kirefu
sana kwa maisha ya mwanadamu wa siku hizi, lakini shukrani za pekee na za dhati
zimwendee mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kuwa mlinzi wake na msaidizi wake
kwa magumu mengi ambayo amepata kupitia ama anapitia kwenye maisha yake ya kila
siku.
Baada ya kutoa utangulizi
huo sasa niende moja kwa moja kwenye kiini cha rai yangu hii ya leo ambayo
nimeipa jina la “maalumu kwa mama yangu”.
Leo ninapoazimisha siku hii ya kuzaliwa, nimependa nitumie muda wangu
kuandika rai hii ya kumshukuru mama yangu kwa malezi bora na mema aliyonipatia
hadi leo hii na mimi nimekuwa mtu kwenye kundi la watu.
Mama yangu mpendwa, najua
waweza usipate bahati ya kusoma ujumbe huu moja kwa moja kutokana na kutokuwa
na access na mitandao hii ya kijamii. Ila niweke tumaini kwamba ujumbe huu
lazima utakufikia popote pale ulipo ama kupitia kwangu (mwanao), mtoto wangu
(mjukuu wako), mchumba wangu, wadogo zangu, ndugu na jamaa zangu, marafiki
zangu ama hata kupitia kwa walimwenguni wengine ambao wataona kuna haja ya
ujumbe huu kutoka kwa uzao wako wa kwanza wa tumbo lako kukufikia.
Mama yangu mpendwa, hata
kama ikatokea nikaitwa na mwenyezi Mungu kwa muda wowote, neno langu hili
litakupa faraja na litaendelea kudumu milele na milele, vizazi na vizazi na
hata jamii kwa jamii kwani hata maandiko yanasema na vile vile wahenga walipata
kunena kwamba “mambo yote yatapita lakini neno litasimama”
Mama yangu mpendwa,
nilipochukua jukumu la kuandika rai hii, nilipata shida sana kumalizia maneno
kutoka aya moja kwenda aya nyingine kutokana na kububujikwa na machozi ya
furaha na upendo wa dhati ulionao kwangu mwanao. Kila ninapomalizia mstari
naona kama vile bado sijakidhi haja ya moyo wangu kueleza jinsi moyo wangu
ulivyo na furaha kutokana na wewe kuwa mama yangu. Hakika hakuna kama wewe mama
yangu.
Mama yangu mpendwa, ni
miezi tisa (9) nimekaa ndani ya tumbo lako nikila na kujisadia kwenye tumbo
lako, nikivuta na kupumua pumzi kwa msaada wa tumbo lako, nikicheza na kufurai
ndani ya tumbo lako, nikirusha mikono na miguu ndani ya tumbo lako na…….dah,
nakupenda sana mama.
Mama yangu mpendwa,
nimeishi kwa kutegemea damu yako yaani ziwa lako kwa zaidi ya miaka miwili (2).
Ukiwa na furaha, ukiwa na huzuni, ukiwa umechoka, ukiwa na haraka,, ukiwa na
safari, na hata ukiwa na msiba, hata siku moja hukuninyima wala hukusita kunipa
ziwa lako mama yangu pale nilipolihitaji.
Mama yangu mpendwa, kwa
zaidi ya miaka 15 nimeishi na wewe, ukinielekeza yapi ya kuyafanya na yapi ya
kutofanya kwenye jamii. Ukinielekeza tabia njema na nidhamu bora kama silaha
itakayonisaidia niishi na ndugu, jamaa na jamii kwa ujumla.
Mama yangu mpendwa, hadi
leo hii umekuwa kiongozi na mwalimu mzuri sana kwangu na kila nikaapo na wewe
nahisi nimekaa kwenye kitovu cha elimu. Neno lako moja kwangu laweza kuwa na
nguvu zaidi ya maneno elfu moja niliyowahi kusikia hapa duniani. Nasaha zako
kwangu ni zaidi ya elimu niliyoipata shuleni.
Mama yangu mpendwa, sioni
chochote chenye kuweza kuonyesha kiasi cha furaha na upendo nilionao kwako,
ijapokuwa moyo wangu peke yake ndio unaojua na kulitambua hili. Laiti kama moyo
ungekua na kioo ili uweze kuona ni jinsi gani jina lako na hadhi yako
ilivyozungushiwa alama ya kopa na kuchukua sehemu kubwa sana kwenye moyo wangu,
ungalithibitisha hili nisemalo. Lakini kwa kuwa siku hizi unaamini viungo vya
mwili wako haviwezi kufikiri ama kutenda kinyume na matakwa yako, basi nami
kama sehemu ama kiungo cha mwili wako niamini kwa haya niyasemayo.
Mama yangu mpendwa, sioni
zawadi ya kukupa ambayo inaweza ikawakilisha ama ikatoa ufafanuzi wa kina juu
ya upendo nilionao kwako. Zawadi pekee ni kutoa maisha yangu yote kukupenda kwa
dhati. Naimani kwamba kwa maneno yangu haya ambayo yanatoka kwenye kiini cha
moyo wangu, hata Mungu baba ataniongezea umri wa kuishi ukichukulia ya kwamba
alitanabaisha kwenye amri zake kwamba “mpende baba yako na mama yako ili siku zako
zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana Mungu wako”
Mama yangu mpendwa,
nisikuchoshe sana kwa siku ya leo kwa kuandika rai ndefu sana, ila ujumbe huu
ukufikie kwamba siku yangu hii ya kuzaliwa nimetoa maalumu kwako kama sehemu ya
upendo wangu wa dahti nilionao kwako. Salamu na pongezi zote kutoka kwa ndugu,
jamaa na marafiki zangu na wengine wote duniani za kunitakia kheri kwa siku hii
zifanyike kuwa maombi ya kukuombea na kukutakia maisha mema, marefu na yenye
amani na furaha hapa duniani na hata milele na milele.
Nakupenda sana mama,
nakupenda sana mama, nakupenda sana mama, nakupenda sana mama, nakupenda sana
mama, nakupenda sana mama, nakupenda sana mama……….
Nimeandaa na kuandika mimi
mwanao mpendwa na uzao wako wa kwanza, Ismail Mesaya
Makala naipenda kuliko makala zote nilizowahi kuandika
ReplyDelete