CHUO KIKUU KIMEGEUKA CHOO KIKUU
Yapata miaka zaidi ya
miaka miwili (2) toka makala hii iliyoshika kasi na kupendeza machoni mwa
wasomi wa CHUO KIKUU ilipopotea
kwenye mbao za matangazo za Cafteria na Getini Mabibo Hostel. Kwa wale
waliokuwa sehemu ya umajimui huu wa UDSM, makala ya mwisho ilitoka tarehe 17th
December 2011 ikiwa na kichwa cha habari kilichonakshiwa kwa maneno ya MCHAWI HUYU HAPA.
Makala ile iliyovuta
hisia za walio wengi hasa ukizingatia hali halisi ya chuo kwa kipindi kile
baada ya chuo kuwafukuza na kuwasimamisha masomo baadhi ya wanafunzi ambao
utawala wa chuo waliwaita vinara wa migomo na maandamano.
Sina lengo la
kuwakumbusha machungu hayo yaliyowakumba kaka zenu wala kuziamsha hisia zenu
juu ya unyama na ukatili uliyofanywa na utawala wa chuo kikuu kwa shinikizo
kutoka posta. Vile vile sina lengo la kuomba hisani kwenu kufanya
“revenge” kwa hili lililotendwa na utawala wa Prof. R. Mkandala kwa moyo mweusi na uso uliokunjamana.
Baada ya tarehe ya
mwisho ya makala hii kupotea kwenye mbao za matangazo, ilinilazimu kutafuta
njia mbadala za kuendelea kufikisha makala ile machoni kwa wadau ambao
walionekana kuongezeka kila kuitwapo leo. Niliona ni vyema nikitumia mitandao
ya kijamii kuwafikia wasomaji wangu lakini pia kulikuwa na kikwazo kwani
ningeweza kuwafikia wale walio marafiki kwangu pekee. Ndivyo nilivyoona ni
vyema nikiwa na blog ambayo kazi yake ni kutawanya elimu ya fukununu kwa watu
wote. Blogu hii ambayo nayo imeanza kupata umaarufu kwa makala zenye elimu kwa
umma zinazochapishwa humo, inapatikana kwa http:fukununu.blogspot.com.
Nadhani kwa
utangulizi huo kila mmoja wetu angalau kinaga ubaga ameshatambua wapi FUKUNUNU
lilipotoka na nini hasa dhima yake. Nisipoteze kurusa nyingi kuendelea kutoa
ulumbi juu ya makala hii, niende moja kwa moja kwenye mada kuu ya siku ya leo
yenye jina la CHUO KIKUU KIMEGEUKA CHOO KIKUU.
Chuo kikuu kama
walivyokisha tanabaisha walionitangulia ni kitivo cha ujuzi na maarifa. Chuo
kikuu pia ni jukwaa la majadiliano na malumbano ya mawazo ili kuzaa mawazo
kuntu kwa ajili ya mstakabali wa taifa letu na jamii zetu.
Mwalimu Nyerere
aliwahi kusema; “A university must be a scholarly pitch where new thoughts are
born”…… Kwame Nkuruma alinena kuwa “A university is a think tank”…… Sokoine
aliwahi kukosoa juu ya wajibu wa wasomi waliopo vyuo vikuu kwa kusema,
“maendeleo ya nchi yanafikiwa kwa kuwepo kwa midahalo na mijadala miongoni kwa
wananchi juu ya namna gani tunaweza kufikia maendeleo hayo tunayoyataka, na
kazi kubwa ya wasomi ni kuratibu na kuongoza majadilianao hayo”
Nukuu hizi zinaweza
kusukuma mawazo yetu ili tufikiri zaidi nini maana ya chuo kikuu.
Chuo kikuu hiki
kimekuwa ni chimbuko la mawazo kuntu ambayo yamewezesha nchi nyingi za afrika
kupata uhuru na pia kitovu cha maendeleo kwa nchi yetu hasa enzi za utawala wa
Mwalimu. Mapambano ya kudai uhuru wa Mozambique mwaka 1975, iliyokuwa South
Rhodesia mwaka 1980 na hata harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika
ya kusini, yalifanywa na wanaharakati waliokuwa sehemu ya umajimui wa chuo
kikuu hiki wakitumia eneo liligeuzwa kwa sasa na utawala wa UDSM kuwa eneo la
kutunzia majani ya mifugo. Eneo hili si linguine bali ni lile lililowekewa uzio
na utawala wa UDSM kana kwamba kuna biashara haramu iliyokuwa ikifanyika pale
na kwa chini wamegeuza soko kwa kuwakodishia wafanyabiashara ili tukuharamisha
matumizi ya awali ya eneo lile.
Eneo hili maarufu kwa
wanasiasa na viongozi mbalimbali wa bara la afrika waliopata kusoma hapa chuo
kikuu cha Dar es salaam, kwasasa ni eneo ambalo ni haramu kutolea mawazo na kwa
yeyote atakayefanya hivyo atakuwa amejitafutia barua ya kufukuzwa chuo mara
moja na moja kwa moja. Kwa wale walioko mwaka wa pili na wa kwanza wa masomo
wangetamani kulifahamu eneo hili ambalo lilipata kutumiwa na watu kama, John Garang’, Joseph Kabila, Yoweri
Museveni, Zakiah Meghji, Samwel Sita, Issa Shivji, Jakaya Kikwete, John Mnyika,
Julius Mtatiro, James Mbatia, Yonas Laiser, Alphonce Lusako, Mwambapa Elius,
Ambros Evarest, Oduor oduang’, Ismail Mesaya, Zito Kabwe, na wengine wengi
katika kutetea haki na maslahi ya makundi mbalimbali katika jamii zao na nchi
zao. Kwa jina maarufu eneo hili linajulikana kwa jina la REV. SQUARE ikiwa na
maana ya REVOLUTION SQUARE.
Katika kuwaziba
midomo na kugeuza chuo kikuu kuwa sawa na shule ya msingi, watawala wameamua
kulifunga eneo hili na kuharamisha mijadala na midahalo yote yatakayofanywa na
wanafunzi wake. Kwa kufanya hivi tunatengeza taifa lenye watu wasio na uwezo wa
kuhoji, kulinda na kutete haki na maslahi yao katika Nyanja mbalimbali.
Chuo kikuu kiwe ni
sehemu ya kuwandaa vijana kurithi nafasi mbalimbali na kulitumikia taifa lao.
Chuo kikuu kitumike kutengeneza taifa lenye watu wenye utashi wa kuhoji na
kunyooshea kidole pale panapoonekana kutendwa kinyume na taratibu. Chuo kikuu
kitumike kuwaandaa wanachi wenye utashi na udhubutu wa kuwawajibisha wale
waliopewa dhamana kuwatumikia katika sekta mbalimbali. Chuo kikuu kiwatengeneze
watumishi na wafanyakazi wenye kukubali kushauriwa na kukosolewa. Chuo kikuu
kiwe chachu na kitovu kikuu cha kusukuma maendeleo ya nchi yetu.
Chuo kikuu kisiwe
sehemu ya kutengeneza jamvi la wasomi wa wa makaratasi wasio na uwezo wa
kuhoji, kutetea na kufanya mambo mengine kuntu kwenye jamii zaidi ya kile
kilichopo kwenye makaratasi.
Nawaomba wale
wahusika walifikiri hili suala kwa kina kwa maslahi ya nchi yetu na jamii zetu
na pia kuwatengeneza watumishi na wafanyakazi wenye manufaa chanya kwa taifa.
Imeandaliwa na kuandikwa:
Jina: Mesaya Ismail
Cont: +255 756 688 090
0 comments:
Post a Comment