Music

Tuesday, May 27, 2014

SAUTI YA VIJANA TANZANIA- MAAZIMISHO YA SIKU YA UKOMBOZI WA AFRIKA 25/05/2014

UCHUUZI- AFRIKA KATIKA AWAMU YA MAKUCHA YA UTANDAWAZI






UTANGULIZI
Awali ya yote nitangulize salamu zangu kwako wewe unayenisikiliza kwa namna ambavyo utaoona itakupendeza wewe. Iwe ni kwa mrengo wa imani yako, itikadi yako ama kulingana na umri wako, hapo ulipo salamu zangu zikufikie.
Pia nimshukuru mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kuendelea kunibariki kwa kila jambo ninalolitenda.

Bila kusahau, vile vile nishukuru na kupongeza Baraza kuu la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa maamuzi yao waliofikia tarehe 25/07/2013 ya kurejesha masomoni baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamefukuzwa na kusimamishwa masomo mwaka 2011/2012. Niendelee kutoa rai yangu kwa chombo hiki cha juu kabisa cha utawala cha chuo hiki kuendelea kutafakari na kufanya uchunguzi wa kina juu ya sababu na taratibu zilizofuatwa na utawala wa chuo hiki katika kufikia maamuzi ya kuwafukuza na kuwasimamisha masomo baadhi ya wanafunzi waliopewa jina la “vinara wa migomo” kwani ni mengi yamejificha nyuma ya pazia na ile ilikua ni sawa na mchezo wa funika kombe mwanaharamu apite.
Kwa heshima ya pekee kabisa, niwapongeze waandaaji wa kongamano hili (SAVITA), kwani kama walivyotangulia kunena waasisi wa taifa hili, namna pekee ya kuondoa umasikini na hali duni ya maisha kwa wanajamii, ni kwa kuruhusu jukwaa la majadiliano na malumbano ya mawazo baina ya makundi mbalimbali kwenye jamii husika juu ya namna ya kulimaliza tatizo hilo. Na kazi kubwa sana ya wasomi ni kuratibu na kuongoza majadiliano hayo.

Pasipo kupoteza muda niende moja kwa moja kwenye mada yetu ya leo iliyopewa kichwa cha somo “uchuuzi Afrika katika awamu ya makucha ya utandawazi”.
Mjadala wangu nimeugawa katika sura kuu nne. Sura ya kwanza ni maana ya neno uchuuzi pamoja na faida na hasara zake. Sura ya pili ni mjadala juu ya utandawazi. Sura ya tatu itajadili kuhusu Afrika katika zama hizi za uchuuzi na utandawazi. Na sura ya mwisho ni mjadala juu ya nini kifanyike barani Afrika ili kukabiliana na sera hizi za uchuuzi na utandawazi.





SURA YA KWANZA
UCHUUZI
Uchuuzi kwa lugha sanifu ya Kiswahili ni kazi ya kuuza vitu rejareja katika duka dogo au kuvitembeza njiani, madukani au majumbani. Kwa fasiri ya lugha ya kiingereza ni “retail business, business of small shopkeepers or dealers in second hand goods.
Uchuuzi unaweza ukawa ni wa bidhaa kama magari, nguo, vyakula n.k. Vile vile rasilimali kama vile madini, bidhaa zitokanazo na kilimo, bidhaa zitokanazo na wanyama n.k. Pia kuna uchuuzi wa teknolojia, mfano teknolojia ya kuzalisha magari, teknolojia itumikayo mahosipitalini, teknolojia ya kuzalishia vyakula na vinywaji mbalimbali n.k.Tusisahau vile vile kuwa uchuuzi waweza kuwa wa vitendea kazi kama zana za kilimo, zana za kufundishia, zana za kujengea na zana zote zile zitumikazo kurahisisha utendaji kazi. Nguvu kazi pia inaweza kufanyiwa uchuuzi, mfano fundi makenika toka china anafanya kazi Tanzania, vile vile madaktari bingwa, wahadhiri, wakufunzi na wataalamu mbalimbali.
Uchuuzi una faida nyingi kwa wananchi, nchi na dunia kwa ujumla katika Nyanja zote za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
KIUCHUMI
Kama nilivyosema awali, uchuuzi unaweza kufanyika kwa vitu mbalimbali kama, bidhaa, teknolojia na vinginene vingi. Uchuuzi unawezesha upatikanaji wa vitu vyote hivi katika kila kona ya dunia tena kwa bei nafuu na katika madaraja, viwango na ubora tofauti.
v  Uchuuzi unamwezesha mtumiji wa bidhaa (Consumer) kupata aina mbalimbali za bidhaa anazohitaji kwa bei nafuu. Upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kwa bei nafuu, unaogeza wigo wa kuboreka (improvement) kwa hali ya maisha na kupungua kwa gharama ya maisha.
v  Upatikanaji wa teknolojia unaongeza uzalishaji (mass production) na kupungua kwa wastani gharama za uzalishaji (average total cot).
v  Kuongezeka kwa uzalishaji kunakotokana na kutumika kwa teknolojia, unaongeza uwepo wa bidhaa sokoni yaani kwa watumiaji ambao ni wananchi, na kumwezesha mwananchi kupata bidhaa bora zaidi kwa gharama kidogo
v  Vile vile uwepo wa uchuuzi kwa bidhaa mbalimbali zinazotumiwa na mtumiaji wa mwisho (consumer), kunaongeza ushindani kati ya wazalishaji wa ndani na wazalishaji wa nje. Hii itasababisha kuongezeka kwa ubora wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
v  Uchuuzi kama nilivyotangulia kusema, huongeza ushindani miongoni mwa wazalishaji, hivyo husababisha kushuka kwa bei ya jumla na kushuka kwa mfumuko wa bei (inflation)
v   Uchuuzi vile vile unawezesha nchi kuuza bidhaa chakavu ama zile ambazo hazitumiki tena kwa matumizi ya kawaida ndani ya nchi husika. (Disposal of obsolesce material)
v  Uchuuzi pia unasaidia kuongezeka kwa wigo wa kodi (Tax base) kutokana na kuongezeka kwa biashara mbalimbali na ujasiriamali.
KIJAMII
Uchuuzi kama nilivyoainisha awali kama upatikanaji wa vitu mbalimbali kwa rejareja, una manufaa kuntu kwa jamii na nchi kwa ujumla katika sekta ya kijamii.
v  Uchuuzi unawezesha jamii kuwa na njia rahisi ya kupata na kupashana habari. Mfano uwepo wa soko la rejareja la vyombo mbalimbali vya habari kama Televisheni, Redio na Magazeti, kumewezesha jamii kupata habari kutoka kwenye kila kona ya dunia kiurahisi zaidi.
v  Uchuuzi umewezesha jamii kuwa na uwezo wa kufanya malipo na manunuzi mbalimbali popote walipo bila kuwatembelea wauzaji wa bidhaa hiyo. Mfano uwepo wa MAX MALIPO, MPESA n.k
v  Vile vile imerahisisha utunzaji wa mazingira. Mfano uwepo wa majiko ya gesi, unasaidia kupungua kwa ukataji wa miti na utumiaji wa mkaa.
KIUTAMADUNI
Katika nyanja ya utamaduni, uchuuzi umewezesha jamii kuachana na mila, desturi na tamaduni zile zilizo mbaya na zinazorudisha nyuma maendeleo. Mfano upatikanaji wa teknolojia ya habari umewezesha jamii kuachana na ule utamaduni wa mwanamke kutoruhusiwa kutumia baadhi ya vyakula.
KISIASA
Kukua kwa soko la habari na vyombo vya habari, kumewezesha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa uwazi na demokrasia katika tasnia ya siasa. Vile vile kuwezesha wananchi kuzifahamu haki na wajibu wao na kuzidai pale wanapoona zimekiukwa.
Pamoja na faida lukuki zinazoambatana na uchuuzi, tukumbuke ya kwamba soko hili la rejareja halichagui ni kipi cha kuleta machoni kwa watu kwa ajili ya kununua. Soko hili linaleta vile vilivyo na madhara chanya pamoja na vile vinavyotuadhiri na kuturudisha nyuma kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kiuchumi. Mfano;
v  Uwepo wa bidhaa za aina mbalimbali kwenye soko hili la rejareja kumewezesha kuwepo kwa bidhaa ambazo zinaathiri asili ya mtu na utu wake. Mfano kijana wa sasa atajiona wa dhamani kubwa kama atavaa nguo zinazoonyesha baadhi ya viungo vya mwili wake, kuliko kuvaa nguo zile za asili ya jamii au taifa lake zinazositiri mwili wote.
v  Uchuuzi umewezesha upatikanaji wa habari kwa rejareja bila kujali staha na umri wa mtu ambaye anapata habari hiyo. Mfano mtu mwenye umri wowote anaweza kununua video hizi za ngono moja kwa moja kupitia kwenye mitandao ama kwenye maduka ya kawaida.
v  Kutokana na kuongezeka kwa ushindani kunakosababishwa na uwepo wa soko hili la rejareja, kila mzalishaji anajitahidi kuzalisha kile ambacho kinaweza kununuliwa na mwananchi wa kawaida (gharama nafuu) bila kujali ubora wa bidhaa yenyewe.
v  Vile vile uchuuzi umekua ni chachu ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu vya kuhujumu uchumi (Black market). Hali hii inasababisha kudumaa na hatimaye kufa kwa viwanda vyetu vidogo vidogo
v  Aina hii ya biashara pia inafanya nchi kuwa kama jaa (Dumping place), kwani kila aina ya bidhaa huingizwa ndani ya nchi hata vile ambavyo havina manufaa chanya kwa wananchi na nchi kwa ujumla
v  Nchi zilizoendelea zinaweza kutumia mwanya huu kunyonya rasilimali zetu kwa mrengo w misaada na hisani

SURA YA PILI
 UTANDAWAZI
Utandawazi kulingana na Sullivan (1994) ni ule usambaaji wa maswala mbali mbali kama vile biashara, mawasiliano, utamanduni n.k kutoka kwa kiwango cha kitaifa hadi katika kiwango cha kimataifa. Akifafanua zaidi, yeye anasema kuwa utandawazi ni ule usambaaji wa maswala kama haya nje ya mipaka ya kitaifa kwa kipindi cha miaka ishirini (20) iliyopita.

Naye mtu mwingine ajulikanaye kwa jina Mwaro (2001), alisema kuwa utandawazi una maana ya mtandao ambao huleta utengamano wa kimataifa na vile vile ongezeko la haraka la ubadilishanaji maarifa katika eneo pana. Akiongezea, alifafanua kuwa utandawazi ni nguvu zinazougeuza ulimwengu na kuufanya kama kijiji haswa kupitia upanuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA).
Ryanga (2002) alieleza utandawazi kuwa utambuzi wa mataifa ya ulimwengu kuwa lazima yafanye kazi pamoja, yashirikiane kibiashara, kiteknolojia, na katika kufanya uwamuzi unaohusu maswala yanayoathiri ulimwengu.

Utandandawazi kwa waarabu wanamaanisha ni makampuni mengi kuenea duniani kote.

Utandawazi ni njia ambayo wenyeji au taifa hufanya mambo kuwa ya kimataifa, kufanya mambo pamoja duniani. Hii inahusu suala zima la uchumi au biashara, teknolojia, siasa na utamaduni.

Utandawazi pia ina maana ya kuwa, ni jambo linalolenga umiliki wa kifikra na kiutamaduni juu ya tamaduni nyingine zilizo dhaifu, kwa ajili ya kusaidiana na kuungana yaani kuwa kitu kimoja, kuondoa mipaka na masafa kati ya nchi na nchi, kukusanyika pamoja na kuleta kitu kinachoitwa “kijiji-ulimwengu”

Hivyo basi tunaweza kusema utandawazi ni mfumo wa ulimwengu wenye lengo la kuinua uchumi, kwa njia ya biashara na mtiririko wa fedha. Mfumo huu unavuka mipaka ya tamaduni, siasa na mazingira

Matumizi ya neno hili “utandawazi” yalianza kushika kasi zaidi kwenye miaka ya tisini, yakimaaanisha kukifanya kitu kuwa katika kiwanggo cha kimataifa, na kukihamisha kutoka katika mipaka na kukifanya kuwa cha wazi na kikafanywa na watu wa aina yote duniani.

Watu wana msimamo tofauti sana kuhusu suala hili la utandawazi. Baadhi wanahisi kwamba inasaidia kila mtu, wakati wengine wanafikiria kwamba inaumiza baadhi ya watu.


MTAZAMO WA MATAIFA MBALIMBALI JUU YA UTANDAWAZI.
Mataifa mengine yanauona utandawazi kama mfumo utakaoleta maendeleo na faida. Yanauona utandawazi kama ufunguo wa maendeleo ya uchumi wa dunia.
Vile vile kuna mataifa mengine ambayo yanauona utandawazi kama mfumo unaolenga kuyanufaisha mataifa machache. Hivyo mataifa haya yameingiwa na woga yakiamini kwamba utaondoa usawa kati ya taifa moja na jingine, utasababisha ajira kuwa ngumu na kuleta ugumu wa maisha.
Utafiti unaonyesha kwamba, tangu mwaka 1980. utandawazi ulipoanza kuvuma, mataifa yaliyojiingiza katika mfumo wa utandawazi yanakuwa haraka kiuchumi na kupunguza umasikini.
Utandawazi ulipoanza kushamiri, nchi za Latin Amerika, na Afrika zilisita kuingia katika mfumo huu. Uchumi wake ukaanza kudumaa na baadaye kuporomoka. Umasikini ukaanza kuongezeka na thamani ya fedha ikashuka haraka kwa kiwango cha kutisha. Nchi nyingi za Afrika zikawa na hali mbaya. Kadiri nchi hizi zilivyokubali kuingia katika utandawazi, mapato yao yaliongezeka, mabadiliko mengi ya kimaendeleo yakaanza kuonekana. Sasa ulimwengu umehakikisha kwamba, kuruhusu utandawazi ni kuruhusu uchumi kukua, ni kuruhusu maendeleo kupatikana, ni kuondoa umaskini na ule ufukara wa kupindukia.

SERA ZA UTANDAWAZI (Globalization policies)
Mfumo wowote ni lazima uwe na sera ili uweze kufanikisha malengo yake baadaye. Vivyo hivyo kwa mfumo huu pia wa utandawazi nao pia una sera katika nyanja zote ili malenggo yake yaweze kutimia. Sera hizo nimeziweka katika makundi ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kielimu, kilugha, kidini na kisayansi na teknolojia.
v  Uchumi;
Sera hii inajipambanua kwamba ili kuinua maisha ya watu toka kwenye hali duni,
(i)                 Ni lazima uchumi ushikwe na watu na mataifa tajiri, au makampuni yenye uwezo.
(ii)               Sera ya ubinafsishaji itumike yaani wawekezaji waruhusiwe kuwekeza katika nchi maskini. 
(iii)             Mfumo wa soko huria uimarishwe. Nchi zisiwe na mipaka katika kuuza bidhaa zake. Mfano ni maonyesho ya biashara ya kimataifa (International trade fairs and exihbitions). Kuanzishwa kwa maduka ya jumla.
(iv)             Kuanzisha mfumo wa kununua kwa njia ya kadi (Card System) ili kupunguza kasi ya watu kutembea na fedha.
(v)               Kuwa na sarafu moja, mfano wa nchi za ulaya.
v  Siasa;
Katika tasnia ya siasa, sera hii ya utandawazi ilijitutumua kwamba amani ya ulimwengu haiwezi kupatikana mpaka ulimwengu umekuwa na Serikali moja.
(A One World Government and One Unit Monetary System..... In the form of feudal system as it was in the middle Ages...) Sera hii imeendelea kujinasibu kwamba, kutokana na ulimwengu kukabiliwa na vita ya ugaidi vilivyotapakaa kila nchi, maisha ya watu hayawezi kuboreshwa mpaka mataifa yawe na amani. Na hili suala la ugaidi haliwezi kuisha mpaka mataifa yaungane na kuwa na nguvu moja.
v  Uhuru na jamii (Community freedom
Utandawazi unadai uhuru wa mtu kutenda jambo bila kuingiliwa na mtu (Conscious freedom).
v  Elimu
Sera ya utandawazi inawataka watu wasome na kuwepo kwa mkakati ni kuboresha mashule na kuinua kiwango cha taaluma ya waalimu ili kupata wasomi watakaosimamia na kuendeleza sera za utandawazi Mfumo wa maisha
v  Sayansi na Teknolojia
Sera ya utandawazi inahakikisha kuwa sayansi na teknolojia inapenya kila mahali. Hili litasaidia kuufanya ulimwengu uwe kijiji kimoja. Television, simu, Computer, Internet, Satellite n.k. zitapelekwa kila mahali ili kuboresha mawasiliano.
v  Lugha
Sera hii inakazia kuwa na lugha moja ya biashara duniani abayo ni kiinggeza.
v  Dini
Utandawazi unapendekeza kuwepo na dini moja ya ulimwengu na siku moja ya ibada. (Universal Religion/Universal day of worship)


SURA YA TATU
AFRIKA KATIKA ZAMA HIZI ZA UCHUUZI NA UTANDAWAZI
Katika Afrika ya leo neno uchuuzi na utandawazi limetawala sana maisha ya kilasiku na kumekuwepo mjadala mzito juu ya faida na hasara zake kwa bara letu hili la asali na maziwa.
Utandawazi kama nilivyokwisha kutanabaisha awali, tunaweza kuelezea kama mchakato wa kuunganisha uchumi, siasa, jamii, uhusiano wa tamaduni n.k. baina ya nchi. Utandawazi unaifanya dunia kuwa kama kijiji kimoja kisicho na mipaka. Utandawazi unasisitiza uondoaji wa vikwazo vyakibiashara na kuifanya dunia kuwa kama soko moja. Utandawazi vile vile unahimiza soko huria, demokrasia, utawala bora, usawa w kijinsia, haki za binadamu, utunzaji wa mazinggira n.k miongoni mwa jamii husika.
Utandawazi siyo dhana mpya kama inavyotaka kuaminishwa na baadhi ya makundi mbalimbali ya watu hapa duniani. Tukiangalia kidunia tunaweza kusema utandawazi ulianza zama za Christopher Columbus alipokwenda Amerika na kuingiza mazao ya miwa, machungwa na uchumbaji mkubwa wa madini.

Kwa Afrika naweza kusema bara hili liliingizwa katika utandawazi rasmi enzi za biashara ya utumwa iliyojulikana kama “The Trans –Atlantic Slave Trade”. Kwani Afrika ilifanywa kuwa chanzo cha nguvu kazi ya bei rahisi, ambapo watumwa walipelekwa bara la Amerika katika mashamba na migodi mikubwa.
Baada ya mapinduzi ya viwanda, biashara ya utumwa ilionekana kutokuwa tena na faida na hivyo ilisitishwa.

WaAfrika walionekana kuwa wanaweza kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya Ulaya na pia kuwa soko kwa bidhaa za viwandani. Hii ilipelekea mnamo mwaka 1884 kufanyika kwa makutano huko Ujerumani, maaarufu kwa jina Mkutano wa Berln, ambapo dhana ya mkutano huu ulikuwa mahususi kuligawa bara la Afrika kwa watawala mbali mbali.
Makoloni yalihimizwa kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya Ulaya, kwa mfano makoloni yaliyokuwa chini ya Muingereza yalizalisha kwa ajili ya nchi hiyo.
Baada ya hapo kiliingia kipindi cha miaka ya 1960s ambapo mataifa mengi ya bara la Afrika yalipata uhuru wake hususan uhuru wa siasa, kwani kiuchumi hali iliendelea kuwa ya utegemezi.

Katika miongo miwili hii tumeshuhudia mfumo huu ukipewa jina jipya ambalo ni utandawazi. Sasa nijikite moja kwa moja kujaribu kuangalia ahtari ambazo Afika imekumbana nazo na hususan kiuchumi.

Kwanza; Umasikini katika bara la Afrika ni asilimia 40 mpaka 50, wananchi wake wanaendelea kuishi katika hali ya umaskini kwa sababu ya ukosefu wa kipato kwa kaya na kibaya zaidi nguvu kazi inaendelea kukua kwa kasi ya asilimia 4 mpaka 5 kwa mwaka na hakuna juhudi muhususi za kuitumia nguvu kazi hiyo katika uzalishaji na kazi za maendeleo.
Pili; Afrika inapokea asilimia 1 ya vitega uchumi toka nje (FDI) na vingi kati ya hivyo vimekuwa vinalundikana katika baadhi ya nchi za Kaskazini, nchi zinazo zalisha mafuta na Afrika Kusini, na kuziacha nchi nyingine zikiambulia vitega uchumi vichache sana na hivyo kushindwa kufaidika na uwekezaji ambao umeongezeka duniani hivi leo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo dunia inayo hivi sasa.

Tatu; Bara la Afrika ni mshiriki duni katika uchumi wa dunia, pato lake ni sawa na asilimia 1 ya uchumi wa dunia (GDP). Uchumi wa Afrika nzima unauzidi kidogo uchumi wananchi wa Ubelgiji, ikilinganishwa na Ubelgiji ambayo amabayo ni nchi ndogo sana hata kwa kuilinganisha na Tanzania

Nne; Utandawazi unahimiza biashara huria baina ya mataifa bila kuzingatia nani anashindana na nani na wanashindania nini? Kwa mujibu wa Christian Aid inakadiriwa kuwa biashara huria imesababisha uharibifu kwa bara hili kiasi cha dola za kimarekani bilioni 272 kuanzia mwaka 1980

Tano; Nchi za dunia ya tatu zinatumia kiasi cha dola za kimarekani 340 bilioni kulipa madeni yanayokadiriwa kufikia dola 2.2 trilioni, kiasi ambacho ni mara tano zaidi ya bajeti ya nchi za G8 inayotolewa kwa nchi hizo kama misaada ya kimaendeleoi.

Sita; Pengo kati ya nchi tajiri na maskini linazidi kuongezeka, kwa mfano miaka 20 iliyopita wastani wa uwiano wa kipato kati ya nchi maskini sana duniani (LDCs) na nchi tajiri ulikuwa 1:87 kwa hivi sasa unakadiriwa kuwa 1:98. Hii inonyesha kuwa utandawazi unazidi kuzinufaisha zaidi nchi tajiri na makampuni ya kimataifa kulikoni nchi maskini na makampuni yake
Dunia ya utandawazi haina huruma na umaskini na isitarajiwe kabisa kuwa nchi tajiri na makampuni yake yana dhati ya kweli kuondoa umaskini huo. Je, zifanye hivyo kwa faida ya nani?

Saba; Kilimo ni uti wa mgongo wa nchi nyingi za bara la Afrika, inakadiriwa kuwa asilimia 70 ya watu wa bara hili wanategemea kilimo, pia kilimo kinachangia katika pato la taifa asilimia 30 (30%of GDP), ni jambo la kusikitisha kuwa ni Afirka pekee ambapo, tija katika kilimo haijaongezeka kwa muda wa miaka 20 yaani kuazia miaka 1980 mpaka 2000

Bara la Afrika miaka 50 iliyopita liliweza kujitosheleza kwa chakula na ziada kuuza nje. Inasikitisha kuona kuwa hivi sasa Afrika inaongoza kwa kuagiza chakula toka nje ya bara la Afrika. Kwa mfano mwaka 1966 mpaka 1970 Afrika iliuza nje wastani wa tani 1.3 milioni za chakula kwa mwaka, na mwisho wa miaka 1970s Afrika iliagiza tani 4.4 milioni za chakula kwa mwaka na takwimu zinaongezeka kufikia tani 10 milioni kwa mwaka mpaka ilipofikia miaka ya 1980.

Nane; Katika dunia ya leo bado Afika watu wanaokadiriwa kufikia milioni 200 hawana chakula, na inakisiwa kuwa nchi 27 za kusini mwa Afrika zinahitaji msaada ya chakula. Yaani bara lililo kuwa linauza chakula nje hivi sasa linahitaji msaada, tena wakati huu ambapo kuna mapinduzi katika uzalishaji wa kilimo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kwa mjibu wa shirika moja la Uingereza la Oxfam inakadiriwa kuwa nchi tajiri zinatumia kiasi cha dola bilioni moja kwa siku kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa wakulima wa nchi hizo. Kiasi hicho ni sawa na pato la nchi maskini sana duniani (LDCs), katika dunia ya namna hii itawezekana vipi mkulima katika Afrika kuweza kushindana na mkulima kutoka nchi tajiri katika soko la kimataifa?

Tisa; Kiasi cha madini kilichoko ardhini kinapungua kila kukicha. Nchini Afrika Kusini mwaka 1960 kulikuwa na na madini yenye thamani ya dola 112 bilioni na mwaka 2000 inakadiriwa kuwepo madini yenye thamani 55 bilioni hii ni kutokana na ripoti za UN. Kwa ujumla Afrika inapoteza sana kuliko inavyopata katika madini.

Kumi; Mwaka 2004 Alpha Oumer Konare aliukumbusha mkutano wa Afrika kuwa, bara la Afrika katika kipindi cha miaka 50 limeshuhudia jumla ya mapinduzi ya serikali yapatayo 186,vita kubwa 26 na wakimbizi wapatao milioni 16 , matatizo yote hayo ukiyaangalia kwa makini yana mkono kotoka nchi za nje ya bara la Afrika kwa njia moja au nyingine.

Kumi na moja; Uwiano wa mapato duniani ni wa kutisha sana, kwa mjibu wa ripoti iliyotolewa na UNHD (Nations Human Development), watu 1.3 bilioni wanaishi chini ya dola moja kwa siku wakati huo huo watu 200 ambao ni matajri sana duniani waliweza kuongeza utajiri wao kati ya mwaka 1994 mpaka 1998 na inakadiriwa kuwa utajiri wao unazidi dola 1 trilioni. Si hivyo tu kwani mabilionea watatu wanao ongoza kwa utajri duniani wanamiliki mali zenye thamani kubwa kuliko mapato (GNP) ya nchi zile maskini sana duniani (LDCs) zikiwa na watu milioni 600.

Kumi na mbili; Tofauti ya mapato (income gap) kati ya nchi tano kwa wingi wa watu duniani katika nchi tajiri na tano kwa wingi wa watu duniani katika nchi maskini ilikuwa 74:1 mwaka 1997, 60:1 mwaka 1990 na 30:1 mwaka 1960. Wale wanaoishi katika nchi tajiri duniani wanamilki pato la dunia (GDP) kwa asilimia 86, wanamilki asilimia 82 ya mauzo ya nje, asilimia 68 ya vitega uchumi toka nje (FDI) asilimia74 ya njia za simu za dunia (world telephone lines) n.k. Huku wale wanaoishi katika nchi maskini sana duniani wanaambulia asilimia 1 tu ya yaliyo tajwa hapo juu. Usisahau pia kuwa nchi hizo tajiri zina asilimia 19 tu ya idadi ya watu wote duniani na zinamilki biashara ya dunia kwa asilimia 71

Ukiangalia nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara kwa ujumla wake asilimia 50 ya watoto wake hawana huduma ya maji salama. Moja ya tatu ya watoto wenye umri wa miaka 5 wana uzito pungufu (underweight) na zaidi ya robo tatu ya watu wake hawatarajii kuishi zaidi ya mika 40 wakati ulaya ni zaidi ya miaka 70

Utajiri wa dunia umo mikononi mwa wachache. Kwa mfano; mpaka kufikia mwaka 2000, makampuni kumi tu ya madawa ya kilimo yalimilki asilimia 85 ya dola 31 bilioni ya soko la dunia. Makampuni makubwa kumi duniani ya mawasiliano yanamilki asilimia 86 ya dola 262 bilioni ya soko la dunia. Katika biashara ya kompyuta, makampuni kumi makubwa duniani yanamilki asilimia 70 ya soko la kompyuta duniani. Asilimia 60 ya madawa ya mifungo yapo chini ya milki ya makampuni kumi makubwa duniani.

Kutokana na mlundikano wa namna hiyo nchi maskini duniani zinapata faida haba inayotokana na maendeleo ya sayandi na teknolojia na elimu kwa ujumla. Kwa mfano nchi kumi zinamilki utafiti na matumizi ya maendeleo duniani na zinamilki asilimia 95 haki miliki ya marekani (patent), kwa sababu hiyo utafiti unazingatia sana faida na siyo mahitaji ya kijamii. Katika kuteua dondoo za utafiti pesa ndiyo inayo ongea na siyo mahitaji, ndio maana tafiti za madawa ya vipodozi na nyanya zinazoiva kidogo kidogo zinapewa kipaumbele kuliko tafiti za mazao yanayositahimili ukame au kinga ya malaria.

Kumi na tatu; Dunia ya leo ya utandawazi inahitaji watu walioelimika ambao wataweza kutumia fursa za utandawazi kama zipo. Afrika inaendelea kuwa nyuma katika kuwekeza katika elimu, kiwango cha ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika ni asilimia 41.

SURA YA NNE
NINI KIFANYIKE AFRIKA ILI KUKABILIANA NA SERA HIZI ZA UCHUUZI NA UTANDAWAZI.
Kwa kuwa hii ndiyo dunia ya leo ambayo Afrika inahimizwa sana kishiriki, dunia ambayo inathamini mwenye nguvu ya mtaji, ambayo IMF, Benki ya dunia na Shirika la Baishara Duniani (WTO) ndio wadau wakuu wa utetezi wa biashara huria inayotawaliwa na nguvu za soko. Dunia ambayo mkulima maskini toka Tanzania anaambiwa ashindane katika soko la kimataifa, na mkulima wa Ulaya au Marekani anayepatiwa ruzuku, super market kama vile IMALASEKO ya hapa Tanzania inaambiwa ishindane na Wal-Mart (kampuni ya kimarekani inayoshika nafasi ya 48 duniani), kampuni ya magari ya Nyumbu inaambiwa ishindane na Mitsubishi (inayoshika nafasi ya 22), kampuni ya posta Tanzania ianaambiwa ishindane na AT&T (inayoshika nafasi ya 48) n.k. Tuwekane wazi tu kuwa katika hali halisi haiwezekani kabisa.

Serikali za nchi za Afrika zinapaswa kuuangalia utandawazi kwa mapana yake, utandawazi wa kuzidi kuziimarisha nchi tajiri na makampuni yake na kulifanya bara la Afrika kuzidi kuwa maskini haupaswi kukumbatiwa kabisa.

Hakuna wa kuliangalia bara la Afrika kwa jicho la huruma ni juu ya viongozi wetu kuwa na visheni na kuona ni kwa jinsi gani tutakuwa na mfumo wa maisha ambao wadau wote watanufaika nao.
Ukubwa wa uchumi wa nchi za magharibu na makampuni yao usitukatishe tamaa wala kutuogopesha kuwa hatuwezi, kwani kama kizazi kilichotangulia kingeogopa nguvu za kijeshi za wakolini, kusingekuwa na nchi ambayo ingekuwa huru hivi leo.
Kizazi cha uhuru wa kisiasa kilifanya kazi yao. Hivi leo tunahitaji uhuru wa kiuchuimi na ni jukumu letu sote kupigana vita ya kujikomboa kiuchumi na kuondokana na umaskini tulio nao katika bara la Afrika, hakuna lisoliowezekana, kupanga ni kuchagua.

NINI KIFANYIKE?
Ili kujikomboa na kujinusuru kutoka kwenye ombwe la kuendelea kuwa wasindikizaji na waapotezaji wa rasilimali katika zama hizi za sera za uchuuzi na utandawazi, hatuna budi kubuni aina ya mfumo mbadala ambao utakuwa na tija kwetu na vizazi vijavyo.
Tukisema tuukatae mfumo wa kiuchumi wa kiliberali, kimtazamo kunawezekana lakini kwa vitendo haiwezekani. Na tukisema turudi kwenye mfumo wa kijamaa kwa mtizamo wangu ni sawa na kuishi kwa kutegemea historia ya babu. Yaani kuishi mfumo wa kijamaa kwenye dunia ya sasa hauwezekani kabisa. Hili naweza kulithibitisha kwa kuangalia mifano ya nchi na mataifa makubwa kiuchumi ambayo yalikuwa yakiishi mfumo huu jinsi yalivyoporomoka hadi walipobadili mfumo wa kiuchumi ndipo walipojinusuru.
Kwa kuwa tukiishi kwenye mfumo wa kiliberali hatutoweza kumudu ushindani uliopo huko, na vile vile kuishi kwenye mfumo mfu wa kijamaa haiwezekani katika maisha ya dunia ya sasa, basi waafrika hatuna budi kuja na mfumo ambao utatekelezekana na wenye manufaa kwetu kulingana na rasilimali tulizonazo.
Wenzetu wa China wana mfumo wao ambao hatuwezi kuuita ni uliberali moja kwa moja wala kuuita ujamaa moja kwa moja. Mfumo huu wa wachina ndio uliowawezesha watu wa taifa hili kupiga hatua kubwa sana kiuchumi na kimaendeleo. Wachina wanaita mfumo wao huo “MFUMO WA KIJAMAA WA WACHINA” yaani Chineese characterized social economic system.
Mfumo huu unaruhusu utawandazi na uchuuzi uwepo lakini kwa manufaa ya mchina yaani unatawaliwa na mchina na siyo sera hizi kumtawala mchina. Ndio maana leo tunamwona mchina ana makampuni makubwa, akifanya biashara karibu kila kona ya dunia na akikua kiteknolojia huku mabadiliko yote haya yakimnufaisha mchina.

Ili nasi tunusurike kwenye sera hizi hatuna budi kuwa na mfumo wetu. Na mfumo ambao utatufaa sisi waafrika ni ule:

Moja; Unaotambua na kuthamini uhuru wa kitaifa.
Uhuru wa kitaifa (nationl independent) kama alivyotanabaisha Mwalimu Nyerere, ni ule ambao unafanya yafuatayo.
(a)    Unatambua na kuheshimu mila, desturi na tamaduni zetu:
Mfumo uliopo sasa wa kibeberu unawaona na kuwachukulia wale wanaofuata mila, desturi na tamaduni zetu (hata kama ni nzuri) kama wasioelimika, na siku hizi wamekuja na jina baya kwa kuwaita washenzi. Wale wanaohusudu mila, desturi na tamaduni za kigeni wanaoneka walioelimika na wastaarabu. Mfano mzuri tu wa namna ya kutekeleza sera hii kwa mfano hapa kwetu, ni kuruhusu lugha yetu yaa taifa (Kiswahili) kuwa lugha kuu ya mawasiliano na kutumika katika mitaala na taaasisi mbalimbali za elimu. Tukianggalia mataifa kama China, Japana, Ukraine na Hispania, wanatumia lugha zao kama lugha kuu ya mawasiliano na biashara. Kwanini sisi isiwezekane? Kwa kufanya hivi, tutakuwa tumewabana wale wanaotaka kuwekeza kwenye rasilimali zetu, wajifunze kwanza lugha yetu ndipo wawekeze. Vile vile mikataba yote iandikwe kwa lugha ya Kiswahili, ambayo itakuwa inaeleweka kwa kila mwananchi hata bibi yangu aliyeko Terat-Nadosoito. Hili litawezekana kwani hata wao wanafanya hivyo kwa wawekezaji kutoka nje ya mataifa yao.
(b)   Unatambua na kukuza uzalendo:
Hapa ninalenga uzalendo kwa maana ya nchi na wananchi wetu. Sii tu kwa viongozi bali kwa waafrika wote, wakiwepo watoto wa jinsia zote, vijana na waee. Uzalendo huu utapatikana kama elimu na malezi tunayowapa watoto wetu itakuwa ni ile yenye kutambua na kuziheshimu rasilimali zetu na kuwafanya wapende na kutumia rasilimali kwa maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla. Elimu hii ninayolenga ni elimu ya kilimo, ufugaji, uvuvi, sanaa na ufundi. Elimu hii itamjenga mtoto mwenye kupenda Afrika kwani amekua akitambua na kutumia rasilimali zetu tulizonazo.
(c)    Uwe na malengo na sera za kujenga taifa la kujitengemea kiuchumi:
Aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania Hayati Sokoine waliita kipengele hichi ni kusimama kwa miguu yetu wenyewe. Hii inajumuisha kuwa na soko letu la ndani kwa bidhaa tunazozalisha, kuwa na chakula cha kutosha na vile vile tuweze kunufaika na rasilimali tulizonazo. Hii itawezekana kama tutakuwa na mfumo wenye sera na mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba tunatumia rasilimali tulizonazo kwa faida ya mwafrika
Pili; Wenye nia ya kuelekeza nguvu zote kwenye rasilimali tulizonazo kama kilimo, ufugaji, uvuvi, sanaa na ufundi
Waasisi wa Afrika walitambua rasilimali tulizonazo kuwa ni ARDHI na WATU wenye nia ya kufanya kazi kwa bidii. Hili ni jambo la kweli kwani nyingi ya rasilimali tulizonazo zinatoka ardhini, mfano kilimo, ufugaji, sanaa, uvuvi, uchimbaji wa madini, utalii n.k. Nyanja hizi ndizo zinazoongoza katika kuchangia pato la nchi za Afrika kwa kiasi kikubwa lakini cha Yule mwananchi wa kawaida hanufaiki wala kufaidika nayo kutokana na mfumo na sera zilizopo kwasasa.
Kwa hili ni lazima tuwe na mfumo ambao utawabana wawekezaji watakaojitokeza na kuwa na nia za kuwekeza kwenye nchi zetu za bara la Afrika, wawekeze kwenye nyanja hizi na matokeo ya uwekezaji huu uende kwa wananchi wa kawaida. Kwa mfano kama ni uchimbaji wa madini, wawekezaji wabanwe na walazimishwe kwenye mikataba yao, wasitoe madini ghafi nje ya nchi kwa madai ya kusafisha bali wahakikishe kama wanataka kuwekeza kwenye madini, wajenge kwanza viwanda vya kusafishia madini kwanza ndani ya nchi husika ndipo wawekeze kwenye uchimbaji. Kwa maana hiyo basi, vitu vitakavyosafirishwa nje ya nchi vitakuwa ni vito vinavyotokana na madini hayo. Kama wawekezaji hawa wataona sheria ya kujenga viwanda vya kusafishia madini ndani ya nchi husika kwanza kuwa ni ngumu, basi wasipewe fursa hizo bali wapewe wawekezaji wazawa na wawekezaji hao wazawa wapewe punguzo la kodi ili kuuwapa motisha ya kuwekeza ndani ya nchi.
Kwa upande wa chakula, ili tujitosheleze kwa chakula, nchi za Afrika hazina budi kuwa na mashamba ya umma angalau kila mkoa au jimbo. Hii itawezesha kila mkoa au jimbo kujitosheleza kwa chakula.
Vile vile serikali za Afrika hazina budi kufanya sekta ya sanaa na ufundi kutambulika na kuwa sekta rasmi, kwani itawaajiri watu wengi na kupunguza uwiano kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho.
Tatu; Unaoleta mapinduzi kwenye uchumi wetu wa sasa.
Ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya uchumi wetu wa sasa unategemea wawekezaji wan je na misaada kutoka kwa nchi wahisani. Kwa aina hii ya uchumi, kamwe hatutaweza kuendele kitaifa kwani nchi wahisani wanapotoa misaada wanatupa na masharti ambayo ni lazima yaweze kuwanufaisha wao. Na hii ndio dhana ya mabeberu katika dunia hii ya sasa ya utandawazi na ukoloni mamboleo.
Ili kuondokana na dhana hii ni lazima tuwe na mfumo wenye kuleta mabadiliko katika uchumi wetu ili sehemu kubwa ya uchumi wetu uwe unachangiwa na uzalishaji wa ndani. Kama tutaelekeza nguvu zetu nyingi kwenye rasilimali tuizonazo yaani kilimo, ufugaji, uvuvi, madini, utalii, sanaa na ufundi, kwa kiasi kikubwa tutakuwa tumeruhusu uchumi wetu uende na ushikiliwe na wananchi wote na kuwanufaisha wananchi wote kwa ujumla.
MWISHO
Mwisho kabisa nimalizie kwa kuwakumbusha maneno aliyoyatamka Mwalimu Nyerere 1964,
“We now have no alternative but to apply ourselves scientifically and objectively to the problems our our continent. We have to think, and act up on our thinking. We have to recognize the facts and conditions which exist. We have to recognize the poverty, ignorance, diseases, corruption, embelzement of public resources, the social attitudes and the political atmosphere which exist, and in that context think about what we want to do and how we can move from the existing situation towards one which we like better”
Nami Mesaya niwaambie, “It is possible to dodge the responsibilities, but we cant dodge the concequences of being irresponsible”
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Imeandaliwa na kuwasilishwa na,
Mesaya Ismail

25/05/2014

0 comments:

Post a Comment