UNAIFAHAMU
CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM?
Uuuuuwiiiiiiii!!!!!!!!!!!! Yarabiiiiii!!!!
Mwaka 2009 nilipatwa na furaha isiyokuwa na kifani baada ya kuchaguliwa
kujiunga na masomo ya juu katika ngazi ya uhasibu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nilimshukuru maulana kwani ndoto yangu imetimia kwani sio tu kwamba
nimefanikiwa kujiunga na masomo ya juu bali ni kwa kufanikisha ndoto zangu za
kusoma Chuo Kikuu barani Afrika na duniani kwa ujumla. Toka utotoni nalikua na
fikara za kuitwa mwanazuoni wa “Mlimani”…..
Taswira niliyokuwa nayo awali juu ya kisima
hiki cha fikra na kituo kikuu kilichozalisha nguli wa kila aina barani Afrika
na ulimwenguni ni tofauti kabisa na hali halisi niliyoikuta ndani ya mdumange
wa Mlimani. Ama kweli wahenga wanasema urembo wa mwanamke si muonekano wa sura
bali kilichopo ndani ya kijuba cha moyo wake.
Chuo kikuu cha Dar es Salaam, ndicho
kilichokuwa kitovu cha harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Kina Robert
Mugabe, Samora Machela, Senghor, Madiba, Kenyata na wengine lukuki wakiongozwa
na Mwalimu J.K. Nyerere waliendesha harakati za ukombozi na kudai uhuru wa nchi
zao na bara la Afrika kwa ujumla chini ya “Rev Square” ya chuo cha Mlimani.
Maraisi kama kina Salvar kiir, Yoweri
Museveni, mwanaharakati Garang’ wote ni mazao ya chuo kikuu cha mlimani. Usisahau
kina Walter Rodney (how Europe underdeveloped Africa) naye ni mjeshi wa kitalu
hiki cha Mlimani.
Hapa Tanzania viongozi wa sekta mbalimbali na
hasasi tofauti tofauti ni mazao ya UDSM. “Prof” Kikwete, PROF. Lipumba, Zito
Kabwe, Mbatia, Mnyika, Shivji, Kabudi, Bana na wengine kedekede ni tanzu za
kitalu cha Mlimani.
Daaah!!!! Ama kweli kwa UDSM kuwa chuo bora
Afrika ya mashariki na kati inastahili kutokana na mazao yake kuonekana kote
duniani na mbegu zake kuota na kutoa vivuli kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Nikiendelea
kulumbana juu ya umahiri na umaarufu wa kijiwe hiki cha wasomi nitamaliza
kurasa nyingi bila kufika tamati.
Pamoja na mbwembwe na sifa lukuki za mrembo
huyu “Mlimani”, kuna baadhi ya mambo nikiyaanika hadharani hutaniamini ama
utaniona nina kinyongo na mzee wa posta, Prof Mkandala. Wengine watasema ni
msukumo wa msimamo na mrengo wangu kisiasa na wengine watadiriki hata kusema
natukana wakunga baada ya kumwona mwana. Lakini ukweli niwahubirie hadhira
yangu, sina hila yoyote na kitalu hiki na mtizamo wangu huu utasaidia wadau
mbalimbali warejee nyuma na kusaidia kukabiliana na changamoto hizi ambazo
zinaelekea kuzaa hadi vilembwekeza.
MAZINGIRA YA
KULALA
Kwa mtu asiyejua unaweza kupiga picha na
kudhani mazingira ya kuishi kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Afika yanalandana na
hadhi ya chuo chenyewe. Mazingira ya hostel za Mwalimu Nyerere Campus ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, hayafanani hata na mazingira ya Shule ya Sekondari
Arusha (Sekii).
Nianze na majengo. Kila mwaka ripoti
mbalimbali za wataalamu wa majengo, zinaonyesha kuwa jengo la Hall V na Hall II
of resident ya Mlimani Campus hayafai tena kuishi binadamu. Wataalamu hawa
ambao nao pia ni sehemu ya waadhiri ya UDSM wamekua wakitoa tahadhari hizo kwa
utawala wa Chuo na serikali kwa ujumla lakini wote hawa wameonekana kukalia
masikio na kutosikia lolote linalonenwa na wasomi hao. Kwasasa imekuwa ni
desturi ya kila mwaka kubomoka kwa sehemu ya ukuta wa maghorofa haya
yanayotumiwa kwa malazi tena wanafunzi wakiwa wamejipumzisha na hakuna hatua
zozote zinazochukuliwa na wahusika. Lakini labda wanasubiri siku moja watu wafe
halafu baadaye iundwe tume ya kuchunguza na kikundi Fulani kujitengenezea fedha
kupitia dili hilo.
Vuta picha majengo ya ghorofa kumi na moja
kila moja (11 Floors) yaliyojengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na hadi sasa
yanatumiwa na watu na mbaya zaidi idadi ya wananchi wanaoishi humo wameongeza
ijapokuwa hakuna urekebishwa wala uboreshwaji wa miundombinu zilizopo. Vyoo
vinavyotumika kwa kila floor ni kama matundu 3 na mbaya zaidi ni ya kukalia. Idadi
ya watu wanaokaa kwa kila floor ni zaidi ya 35 na wote wanapata huduma kwenye
matundu haya matatu tu ya kukalia. Je, Hapa kupata maradhi ya fangasi sehemu za
siri kutakwepeka kweli?? Je, Serikali na wadau mbalimbali hawalioni hili??
Mbali na miundombinu ya kupatia huduma
binafsi kuwa hafifu, vitanda vilivyopo kwenye kila chumba ni viwili vya double
deka. Vitanda hivi ni size ya mita 2 kwa sita (2x6) lakini hulaliwa na watu
wawili kwa kulala mzungu wanne. Nikisema mzungu wanne namaanisha kunyonyana
vidole kwa mmoja kuelekeza kichwa mashariki na mwingine magharibi. Hali ya
malazi haijaisha hapo, bado kuna vigodoro vinavyojulikana kwa jina maarufu kama
“ulimi”. Vigodoro hivi hutumiwa na wanafunzi ambao wamekosa malazi kama sehemu
ya kuweka mbavu zao unapoingia usiku. Ifikapo kipindi cha mitihani wengine
hulala kwa kupokezana na wengine hufikia hatua ya kulala juu ya meza za kusomea
kama sabufa na hata wengine kulala uvunguni kama mende. Dah!!! Ebwana hiyo
ndiyo Mlimani ambayo wengi walio nje ya karandinga hili hawajui yaliyomo ndani
yake.
MIUNDOMBINU
YA MAJI MACHAFU
Chuo Kikuu na cha kuheshimika barani Afrika
na chenye wanataaluma na wataalamu nguli Afrika, kila kona kuna mifereji
yaliyojitengeza ya vinyesi na mikojo. Ukiwa eneo la Academic bridge kwa wale
waliopata bahati ya kufika eneo hili, kuna matiririko ya mchanganyiko wa mavi
na mkojo ambao hutirirka ovyo tena imekua jambo la kawaida sana na
lililozoeleka kwa wanazuoni wa jamvi hili kwani wanafunzi na waalimu wanaotoka
Economics department kuhudhuria lecture za Theater one na two wamekuwa
wakisaidia kuchanganya mchanganyiko huu wa vinyesi kwa kutumia miguu yao bila
kupenda.
Miundombinu hii ya maji machafu kila kona ya
kitalu hiki cha fikra hayaridhishi kwani kila kona ukipita utakutana na
mtirirko wa mavi na mikojo kitu ambacho kinaharbu na kushusha hadhi ya kiota hiki
cha enzi cha kitaaluma.
MIJADALA,
KONGAMANO NA MIDAHALO YA KITAIFA/NA KIMATAIFA KWA WANAFUNZI
Ili kukuza uwezo wa vijana wetu kuhoji na
kuyafahamu mambo mbalimbali yanayotokea duniani na yanayoikumba nchi, wazee wa
zamani waliweka eneo maarufu kwa jina la Revolution Square kama sehemu ambayo
vijana wasomi wa kiota hiki cha fikra wataweza kukutana na kujadili masuala
mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa manufaa ya nchi yetu na bara letu kwa
ujumla. Hali ilivyosasa, lile eneo limegeuzwa ni haramu na mtu yeyote
atakayesimama pale mara moja hufukuzwa chuo na kufungiwa udahili katika vyuo
vyote vya umma na kupata mikopo ndani na nje ya nchi. Shughuli mbadala
inayoendeshwa ndani ya eneo hili ni ukataji wa majani ya kulishia ng’ombe. Kama
Mwalimu Nyerere angekua mbinafsi na kuzuia vijana kujitengenezea uwezo wa
kuhoji na kujenga hoja, leo tungekua na kina Kikwete tungewapata? Kwanini mnakuwa
waoga kwa kuwafunga vijana midomo ili wasikemee uozo na utumbo mnaoufanya? Eti kisa
cha kufunga eneo hili ni kwasababu Ndugu Mkandala amepewa onyo na Ndugu mmoja
wa Posta kuwa eneo hilo linazalisha vijana wenye uwezo kwa vyama vya upinzani.
Shame up on you!!!!!!!!! Yaani unatanguliza mrengo wako na msimamo wako kisiasa
kuliko maslahi ya nchi na vizazi vijavyo? Kweli akili ndogo siku hizi imetawala
akili kubwa na akili hiyo kubwa imekubali kufyata na kuuza dhamani ya maarifa
na ujuzi wake kwa digrii za kichina…….
Itaendelea
next week…..
Imeandaliwa
na Comrade Ole.
0 comments:
Post a Comment