Ndugu mfuatiliaji wa kisa hiki, karibu ungana
nami kwenye sehemu ya pili ya “unaifahamu
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam?” Kabla sijakudokeza wapi tuliishia wiki
iliyopita, nisiwe mchoyo wa fadhila kukupeperushia zangu salamu zikukumbe
popote ulipo. Bila hiyana nikupongeze pia kwa kunipa muda wako tena bure kabisa
kwa kusoma mtiririko wa makala zangu kupitia kitovu cha fikra endelevu cha “Fukununu.blogspot.com”. Hii inanipa
moyo wa kuzidi kuandika, kuanika na kuchimbua na kuibua mengi ambayo yapo nyuma
ya pazia ama yanasikika kwa nadra sana kutokana na mfumo beberu na kandamizi
ulioota mzizi ndani ya jamii yetu hii ya “adabu
na utii kwa bwana mkuu” (Amani)
Najua wale wenzangu na mimi mtahoji sana
kwanini amani iliyopo hapa nchini nimeifungia mabano na kuita ni adabu na utii
kwa bwana mkuu. Mnaweza kufika mbali zaidi na kujiridhisha nafsini na mioyoni
mwenu kwamba Ole anayafanya haya kutokana na mrengo na msimamo wake kisiasa.
Sitowashangaa kwa hilo kwani imekuwa ada na jambo la kawaida kwenu kwa yeyote
atakayewananga kwa lahaja za kweli bila kupepesa macho na kumung’unya maneno
kuitwa “mpinzani”. Hivi kweli
tunaweza kusema kuna amani ilihali kina “We-Lema,
Tiba-Ibuka, Man-Swi, Chen-Ge, Kik-Ikweta, Pin-Ndao” na wale wengine
wamechota bilioni 321 za Escrow huku walalahoi wakishinda kwa “suti” kuanzia asubuhi hadi asubuhi????
Kuna amani gani wakati bwana mkuu anatibiwa busha kwa Obama huku Matonya
akijificha ndani kwa kudhuriwa na honi ya magari??? Kuna amani gani wakati
mawazo yangu na wakulima wa Nadosoito yametupiliwa mbali kwenye mapendekezo ya
katiba na kuchukua mawazo ya kikundi Fulani cha watu kilichojitengezea kanuni
na sheria za kuwadanganya wananchi ili wapewe ridhaa ya kuongoza taifa???? Kuna
amani gani kama watu wote wenye mawazo tofauti na wizi na ufisadi huchomolewa
kucha na meno Mwabepande tena bila ya ganzi??? Kuna amani gani wakati kila
mwaka bei ya bidhaa za chakula na gharama za maisha zinaongezeka kwa mwananchi
wa kawaida huku tabaka la juu likizidi kujiimarisha kwa unyonyaji???? Kuna
amani gani kama mtoto wa Ole Lengai kutoka En’donyo Kumur aliyefaulu kujiunga
na masomo ya elimu ya juu anashindwa kusoma kwa kukosa mkopo huku mtoto wa “Afisa” aliyesoma ughaibuni akipata
asilimia mia????? Kuna amani gani kama mke wangu anajifungulia chini na kitovu
cha mtoto kukatwa kwa kipande cha jiwe kwa kukosekana kwa huduma za afya bora
vijijini na miundombinu ya barabara???? Damn it!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!! Huu
udanganyifu sasa uwe bayana kwa watu wa tabaka na rika zote wa jinsia
mbalimbali pasipo kujali itikadi zetu za dini, kabila wala siasa. Narudia tena
HATUNA AMANI BALI TUNA ADABU NA UTII KWA BWANA MKUU.
Baada ya kukuamsha hisia zako juu ya udokozi
unaofanywa na hawa manyang’au wanaojificha kwenye mwamvuli wa chama Fulani cha
siasa, sasa nikupeleke kwenye mada yetu kuntu ya wiki iliyopita hasa pale
tulipoishia. Nilikuacha na ulumbi juu ya kufinywa kwa fikra na uhuru wa kutoa
mawazo kwa vijana wasomi wa kitalu hiki. Sasa ungana nami kuendelea kurutubisha
mawazo yako juu ya “the un-revealed story about UDSM”
Baada ya kufanikiwa kuzima malumbano ya
mawazo miongoni mwa vijana wenye fikra sanifu na sadifu juu ya mhimili wa taifa
letu, watu hawa ambao kwa majina hujulikana kama “maprofesa” wamezima pia uhuru
wa kutoa mawazo kwa kutumia makala, vipeperushi na mabango. Awali chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kiliweza kuzalisha waandishi mahiri wa makala na wachambuzi
wazuri wa mada mbalimbali kutokana na vijana wasomi wenye ukombozi wa fikra
kujihusisha na uandishi wa makala na nakala mbalimbali na kubandika kwenye mbao
za matangazo za UDSM. Tulikuwa na majarida kama Mlimani Leo, Mlimani Kesho,
Fukununu na Wazo Pevu ambayo yalijikita kuchambua masuala mbalimbali ya
kiuchumi, kielimu, kisiasa, kiutamaduni na kijamii yanayotokea ndani na nje ya
nchi yetu ya Tanzania. Vijana waliokuwa wanajitutumua katika uandishi huu
walipata moyo wa kuziendeleza karia hizi kutokana na kuwapata hadhira wengi
ambao walitumia muda wao kusoma na kutoa mawazo yao juu ya mada zilizokuwa
zikijadiliwa.
Baada ya kupitishwa kwa waraka wenye jina
maarufu kama waraka wa Kawambwa ambao uliandaliwa mahususi kuzima mawazo pevu
na hojaji zenye mrengo wa kutia mchanga kitumbua cha mabeberu wa nchi hii ambao
ndio walioshikilia nafasi mbalimbali za kiutawala. Madubwana haya yaliona namna
pekee ya kuzima mawazo kuntu kutoka kwa umajumui wa wasomi na wanazuoni wa
elimu ya juu ni kuwadumaza kimawazo na kutowaruhusu kutawanya mawazo yao juu ya
changamoto zinawakabili wananchi wa Tanzania.
Hali ya kutokea kwa dumuzi huyu ilianza
kuonekana pale mkuu wa nchi Ndugu Kikwete alipozuru Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kampas ya Mlimani na kujikuta akipata tumbo joto baada ya kukutana na
mabango yaliyoandikwa kisomi na yaliyobeba mada kuntu zenye kuelezea hali
halisi ya maisha ya watanzania. Vilevile kila alipojitahidi kubwabwaja kama
kawaida yake kuwadanganya watanzania, mkuu wa nchi alijikuta pia akikumbwa na
zomea zomea kutoka kwa fikra zilizokamaa na zilizochoka na unyonyaji uliopo
ndani ya nchi hii.
Kutokea kwa hali hii kuliamsha hisia za
mabwanyenye wa nchi hii na kumshawishi kada mkuu na mshauri wa Baba Riz kwenye
masuala ya kisiasa, Prof Mkandala kuwachukulia haraka sana ikiwa ni kuwafukuza
masomo wanafunzi wote watakaohoji jambo lolote ndani ya chuo na vilevile
“kifaranga” huyu akapewa rungu lenye mamlaka ya kuwanyima udahili kwenye vyuo
vyote vya umma wanafunzi watakaokutwa na kadhia hii lakini zaidi pia ni
kutopewa mikopo ya serikali tena hata kama watapata vyuo vya binafsi.
Hali ilivyo sasa ndani ya UDSM ni “mind your
own business” kama ilivyo kwa shule za sekondari hasa zinazoongozwa na taasisi
za dini. Jamii ile ya chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo ilijulikana kama
Think tank, kwa sasa tunaweza kuita ni Thin tank kwani kinachofanywa na
wanaoitwa wasomi wa jamii hii ya mlimani ni “kupiga desa tu”…. Hata kuhoji kama
chakula hakina chumvi vijana hawa wamebanwa na hawaruhusiwi kujielekeza kwenye
hili kwani kwa tafasiri yao wanasema hali jiyo itaharibu amani ya chuo. Sasa
swali, Je, kumfungia nyoka kwenye shimo na kuwasha moto juu yake, utakuwa
umemaliza ukali wa huyo joka na utaweza kulala kwa amani? Tusije tuakawa
tumezificha shida na kero za vijana wa elimu ya juu kwenye majani yenye urefu
wa ndengu, huku karaha hizi zikiendelea kuota na kumea kila kuitwapo leo.
Ndugu msomaji, hali ilivyo sasa ndani ya UDSM
ni hatari katika sekta mbalimbali za kiafya na kimawazo na kwa wale ambao mna
mawazo kama yangu awali za kujiunga na UDSM kama kitovu cha mawazo na fikra
endelevu, hicho kitu hakipo tena. Ni bora ukajiunga na vyuo vingine ambavyo
unaweza kuendeleza karia yako nyingine mbali na masomo kwani ndani ya mlimani
wanaoweza kufanya hivyo ni wale ngedere wa Hall 2 na 5.
@Comrade Ole
0 comments:
Post a Comment