Music

Monday, March 24, 2014

Muhimu sana kwa wanafunzi......

MBINU ZA KUSOMA KWA MAFANIKIO
Asallam Allaeikum wenzangu waislamu na tumsifu Yesu kristo kwa wenzangu wenye imani ya kikristo. Vile vile msidhani nimewatenga wale msioamini upande wowote kati ya hizo mbili nilizotaja, la hasha, ila kwa kuwa hakuna salamu moja inayowaunganisha wote basi kila mmoja achukue nafasi yake ajisikie ndani ya moyo wake kwamba nimemsalimu kwa aina ya salamu wanayoitumia kwa imani yao.
Naam! Baada ya salamu hizo nikiwa na imani kwamba kila mmoja amefarijika kwa kutaja imani yake na ameitikia kutoka ndani ya nafsi na moyo wake, nami ni mzima bukheri wa afya tele. Nisileta hoja nyingi sana kwenye utangulizi wa mada ili nisichoshe medulla yako msomaji kabla ya kupata kupakua kile nilichokiandaa.

Katika mada yangu iliyopita, nilijaribu kutoa ulumbi wangu juu ya nini cha kufanya ili mwanafunzi apate matokeo yatakayopendeza machoni kwa yeyeto atakayepata muda wa kukodolea. Katika mada ile ambayo ililenga kumpa ushauri kuntu mwanafunzi na mzazi wake juu ya kanuni muhimu za kufuata ili hatimaye awe na matokeo mazuri mwishoni, nililenga wanafunzi wote hasa kuanzia ngazi ya awali kabisa ya elimu ya sekondari. Mada ya leo nalenga hasa wale wanaojiandaa na mitihani ya taifa juu ya mbinu madhubuti za kutumia kwa muda mdogo waliobaki nao katika kujiandaa kukabiliana na mitihani yao.
Kama ni jambo linapaswa lizungumzwe na lipewe kipaumbele ni mbinu zipi mwanafunzi hasa yule anayejiandaa na mitihani ya taifa azitumie ili afanikishe safari yake kwa mafanikio. Hili linapaswa hasa lizingatiwe na mwanafunzi kwani yeye ndiye mhusika mkuu katika tukio hilo. Sasa ungana nami katika kujadili baadhi ya mbinu ambazo mwanafunzi akizifuata na kuzingatia atapata mafanikio katika mitihani yake. Mbinu hizi za kusoma kwa mafanikio zitafanya kazi tu pale na kwa yule mwanafunzi ambaye anazifuata kanuni zile nilizozitaja katika mada iliyopita kwa kuziita principles of a good and successful student.
Mbinu za kusoma kwa mafanikio
i.                    Tanguliza nidhamu katika kusoma
Kama nitaambiwa nitaje mbinu moja iliyo kuu katika mafanikio ya mwanafunzi basi sitochelea kutaja NIDHAMU. Mwanafunzi mwenye nidhamu ni yule anayeheshimu sheria za shule pamoja na kanuni na taratibu zilizowekwa. Sizungumzii nidhamu kama kuwaogopa waalimu, la hasha, bali nalitaja neno nidhamu katika tasnia ya elimu kama, kufuata na kuheshimu ratiba zilizowekwa, kuhudhuria kwenye vipindi vyote kadiri ratiba inavyosema, kufuata kanuni, taratibu na sheria za shule, kujidhamini na kudhamini mali ya shule na kuwa mkweli na muwazi kwa wanaumajimui wote.


ii.                  Fanya kusoma ni sehemu ya shughuli zako za kila siku
Kama utaambiwa utengeneza ratiba yako ya siku, basi kusoma uwe umeipa kipaumbele. Kwa kuwa hiyo ndiyo shughuli yao kuu, hapana budi kuhakikisha kwamba unatumia muda mwingi katika kufanikisha. Kusoma kwako kuwe ni muda wowote ujisikiapo kufanya vile na hata ule muda ambao mwalimu hayupo hakikisha unautumia vizuri katika kufanya maswali yanayohusiana na soma husika.
iii.                Tambua fani yako na elekeza nguvu ya ziada huko
Natumaini kila mwanafunzi amalizapo kidato cha pili hutakiwa kuchagua fani atakayoendelea nayo. Aitha ni sayansi au biashara au sanaa. Kabla ya kufanya machaguo hayo huna budi kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu wanaokuzunguza wakiwepo walimu wako, wazazi, ndugu, jamaa na rafiki zako. Usifanye machaguo kwa kufuata mkumbo, ama kwasababu wataka kuonekana kwamba upo juu…. Fanya seleksheni kwa kuangalia pale unapomudu zaidi pia kwa kufuata ushauri kutoka kwa walimu na wazazi wako na pia kwa kulinganisha na matokeo yako toka ulipojiunga na elimu ya sekondari.
iv.                Tengeneza ratiba yako ya kujisomea
Mbali na kwamba shule inakuwa na ratiba yake ambayo hutumika katika kufundishia, kila mwanafunzi mwenye kutaka kufanikiwa hana budi kujitengenezea ratiba yake binafsi. Hii ni kwasababu muda ambao mwanafunzi anakuwa darasani akifundishwa ni mchache ukilinganisha na muda anaokuwa peke yake akijishughulisha na shughuli zingine.
Masaa ambayo mwanafunzi anakuepo darasani kwa siku ni masaa 6 tu. Hivyo kwa mwezi anakaa darasani kwa jumla ya masaa 132  sawa na siku 5.5. Kwa mwaka mwanafunzi hukaa darasani kwa muda wa miezi isiyozidi 9. Kama kila mwezi anasoma siku 5.5 basi kwa mwaka ataingia darasani kwa siku zisizozidi 50 kati ya siku 365. Kwa maana hiyo kwa jumla ya miaka minne atakaa darasani kwa siku si zaidi ya 200 kati ya siku 1460 ambayo ni sawa na asilimia 13.7 ya muda wake wote wa kusoma ordinary level. Hivyo asilimia 86.3 zilizobaki mwanafunzi anakuwa free kufanya shughuli zake. Hivyo kuna haja ya kujitengenezea ratiba yako ya kujisomea ili kufanya “effective utilization of that ample time”
v.                  Soma kwa kushirikiana (Group discussion)
Kusoma kwa kutumia Group discussion, kutamsaidia mwanafunzi kuelewa zaidi pale ambapo yawezekana hakuelewa vizuri mwalimu alipokuwa anafundisha. Natambua kasi na uwezo wa uelewa ni tofauti kwa kila mtu, hivyo kama wanafunzi watasoma kwa group watasawazisha yale ambayo hayakueleweka ipasavyo kwa upande wao. Vile vile kusoma kwa makundi kunamfanya mwanafunzi atambue uwezo wake akilinganisha na wengine, na vile vile kuongeza ushindani miongoni mwao.

vi.                Kuwa karibu na walimu
Mwalimu ana mchango wa 25% katika mafanikio ya mwanafunzi. Kwa maana hiyo mwanafunzi anayehudhuria darasani na kuwa karibu na mwalimu wa somo, hata pasipo kusoma ana 25% za kufaulu kwa somo hilo. Hivyo kama mwanafunzi atakuwa karibu na mwalimu wa somo, kutamsaidia kulipenda somo husika na vile vile kulazimika kuongeza jitihada zaidi ili kufaulu somo hilo. Kama atafanya hivyo atakuwa amepata zile 25% za mwalimu na sehemu ya 75% za yeye mwenyewe kujitafutia.
Idadi ya mbinu hizi nilizozitoa haimaanishi kwamba ndizo mbinu pekee zilizopo, hasha, kuna zingine zaidi ambazo msomaji anaweza akazipata kutokana na kusoma makala hii. Hivyo si vibaya ukaongezea kwani wote tuna lengo la kuboresha elimu yetu.
Nihitimishe kwa kuwataka wanafunzi wote, walimu na wazazi wajaribu kuzitumia ili tupunguze ombwe na kadhia hii ya wanafunzi wengi kufeli kwani kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaofeli kunasababisha kuongezeka kwa idadi ya vijana wasio na ajira na wasio na utaalamu wowote. Hili linapelekea kuongezeka kwa vitendo viovu katika jamii na uvunjifu wa amani.
Imeandaliwa na kuandikwa na:
Jina: Ismail Mesaya
Mob: +255 756 688 090
Vile vile utapata kwenye: http:/fukununu.blogspot.com


1 comments: