MWANAFUNZI FANYA HIVI UPATE KUFAULU MITIHANI YAKO YA
TAIFA
Awali
ya yote niwasalimu na kama ilivyo ada kwa tamaduni zetu za kiafrika baada ya
salamu kifuatacho ni kujualiana hali ya familia na utokako. Vivyo hivyo na mimi
niwe na tumaini moyoni kwamba wewe msomaji wa makala hii u mzima na bukheri wa
afya pamoja na familia yako.
Leo
nimelenga kutoa darasa kwa wanafunzi wa shule za sekondari juu ya nini cha
kufanya ili aweze kuhesabiwa kwenye lile kundi la wanafunzi wenye daraja la
kwanza ama la pili na/ama kuondoka kwenye lile ombwe la wanafunzi wenye daraja
la nne na daraja sifuri.
Mada
hii inalenga kumtanabaisha mwanafunzi wa sekondari kuanzia ngazi za awali
kabisa juu ya namna gani ajiweke ama afanye nini ili hatimaye mwishoni apate
matokeo mazuri. Pia kama wale walio na mitihani ya taifa hasa kidato cha nne na
sita wanaweza kutumia kanuni hizi wakati wakijiandaa na mitihani yao ya taifa.
Nisipoteze
kurasa nyingi katika kujadili utangulizi wa mada, sasa nilenge moja kwa moja
kwenye kiini cha mada. Kama mada inavyojitutumua kwa kichwa cha somo
kilichonakishiwa kwa maneno “Mwanafunzi fanya hivi upate kufaulu
mitihani yako ya taifa” nami nitoe ulumbi wangu kwamba nalikua
namaanisha nini kwa somo hili.
Somo
hili linalenga kutoa njia ama kanuni anuai zitakazomsaidia mwanafunzi kufanya
vizuri katika mitihani yake kama atazifuata na kusizingatia. Kanuni hizi
nimezitengeneza mwenyewe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo
wanafunzi, walimu, wazazi, viongozi na makundi mengine mbalimbali kwenye jamii
ambayo yana mapenzi ya dhati kwenye sekta hii ya elimu.
Kanuni (principles) za kufaulu
1.
Fahamu sababu yako ya kusoma (Tambua ni kwanini
unasoma) (Reasons for being at school)
Wanafunzi walio wengi hata baadhi ya wazazi (hasa wa
jamii ya wafugaji, wakulima, wavuvi na warinaji) hawatambui ni kwanini
wanasoma/wanawaelimisha watoto wao.
Mtoto anapozaliwa jamii inashangilia na kupiga
vigelegele kwa kumpata mtoto ila ni wachache sana kwenye jamii wanaokuwa tayari
wamekwisha kuandaa mazingira endelevu kwa mtoto wao. Mazingira endelevu ni
pamoja na kumwandalia mototo mpango mkakati wa muda mfupi na muda mrefu yaani
wa kuanzia miaka 0-5, 5-10, 10-15, 15-25. Ili kumwezesha mtoto kuweza kukabiliana
na hali halisi ya mazingira ya dunia ya sasa na kutomtengezea maisha magumu,
wazazi hawana budi kuwatengenezea malengo watoto wao kuanzia ngazi ya awali
kabisa, yaani pale wanapokuwa ujawazito. Hii itawasaidia kuwa na familia bora
ambayo wanaweza kuimudu na kuihudumia kuanzia soksi hadi kofia.
Kwa upande wa mtoto ni lazima atambua ni kwanini
wazazi wake wakampeleka shule, ni kwanini wazazi wake wanatumia gharama nyingi
kumsomesha, ni kwanini wazazi wake wanatumia muda mwingi kuhangaika na elimu yake.
Tathimini hii yapaswa kufanywa na mwanafunzi kwa kutambua umuhimu wa elimu
kwake.
a) Elimu ni silaha itakayomsaidia mwanadamu kukabiliana
na mazingira na changamoto za kila siku za maisha.
b) Elimu ni jamvi litakalomsaidia kijana kupokea na
kurithi mila, tamaduni na desturi za taifa lake. Kwa kusema mila, desturi na
tamaduni za taifa namaanisha tunu na rasilimali za taifa.
c) Elimu ni maji yatumikayo kunyeshea mipango na miradi
mbalimbali ya mwanadamu na taifa lake kwa ujumla.
d) Elimu ni chombo kitakachomsaidia mwanadamu kutumia
rasilimali na tunu zilizopo kwa manufaa chanya kwa jamaa na jamii yake
Hizi ni baadhi tu ya umuhimu wa elimu kwa jamii. Hivyo
kama mwanafunzi anapaswa atambua anasoma ili apate elimu itakayomsaidia
kukabiliana na yaliyotanjwa hapo juu.
2.
Fahamu/Tambua thamani yako kama mwanafunzi (Your value
as a student)
Katika jamii yetu ya kitanzania na hata dunia nzima,
mwanafunzi ni cheo ambacho kinaheshimiwa sana na makundi mbalimbali ya watu
katika jamii. Heshima hii inatolewa na jamii kwasababu wanatambua kwamba
“mwanafunzi” ni mtu anayeandalia kupokea na kurithi tunu na rasilimali za taifa
kwa maendeleo ya taifa husika. Kwa kupitia wanafunzi ndipo tutakapo wapata
viongozi, madakitari, walimu, wanasheria, wahasibu, wahandisi, wakufunzi na
wataalamu mbalimbali. Vivyo basi ni lazima mtu huyu apewe dhamani ili baadaye
tumpate mtu sahihi tunayemtaka kumkabithi tunu na rasilimali za taifa letu.
Kwa mfano tu mrahisi, leo hii wanafunzi (wakiwa
wamevalia sare za shule) wakivuka barabara katika miji yetu magari husimama ili
kuwapisha wanafunzi hao wavuke. Vile vile siku hizi tunaona pia jamii imekuwa
ikichukua jukumu la kuwavusha wanafunzi barabara pale panapo onekana kuna magari
yanayoenda kwa kasi. Si hilo tu, jamii imekuwa ikichukua hatua mathubuti kwa
yeyote atakayeonekana akifanya jambo ambalo linahatarisha maendeleo ya
mwanafunzi shuleni. Mfano ukionekana unaingia gest na mwanafunzi jamii
itakuchukulia hatua haraka, vile vile ukionekana unawauzia wanafunzi madawa ya
kulevya pia jamii haitosita kukuchukulia hatua. Hata serikali inalitambua hili
na kuwadhamini wanafunzi ndio maana wanafunzi wana gharama zao za usafiri
tofauti na watu wengine.
Vivyo hivyo kwa mwanafunzi ni lazima atambue heshima
hii anayopewa na jamii na ajaribu nayeye kuheshimu cheo hiki kwani kwa kufanya
hivyo atakuwa amewaheshimu jamaa wa jamii ile na vile vile ameheshimu dhamana
ile aliyopewa. Mwanafunzi ni lazima afananie na cheo chake na heshima ile anayopewa.
Mwanafunzi avae mavazi yanayoendana na cheo na thamani yake. Mwanafunzi awe ni
mfano wa kuigwa kwenye familia na jamii yake kwa kufanya vile ambavyo vitalinda
na kutunza cheo na heshima yake.
3.
Kuwa na malengo (Your targeted objectives)
Mwanadamu yeyote anapoanza kufanya jambo lolote, huwa
na malengo si ya kumaliza jambo husika bali ni kufanikisha lengo la kufanya
jambo hilo. Kwa yeyote anayefanya hivi mara nyingi huwa na mipango mikakati na
sera (strategies and policies) za kumwezesha kufikia malengo tajwa (Targeted
objectives) kwenye jambo hilo.
Kwa upande wa wazazi, hapana budi kuwa na malengo na
kupanga njia na mipango mikakati za kumwezesha mtoto wao kufikia malengo hayo.
Kwa mfano waweza kuwa na lengo la kuhakikisha mwisho wa siku mtoto anapata
alama daraja la kwanza katika mitihani yake ya mwisho ya kidato cha nne na vile
vile kupata daraja la kwanza katika mitihani ya mwisho ya kuhitimu kidato cha
sita. Kwa kuwa na lengo hili itakulazimu wewe kama mzazi kumtafutia kijana wako
huyo vitabu vya kutosha, kumlipia masomo ya ziada, kuwa karibu na walimu na
kufuatilia maendeleo yake kwa ukaribu mkubwa na kila wakati. Vile vile mzazi
muekee kijana huyo malengo ya muda mfupi ambayo yatamsaidia kufikia lengo
husika katika mitihani ya mwisho kwani kama wasemavyo wahenga, mafanikio ya kesho yanahitaji maandalizi ya
leo.
Kwa upande wa mwanafunzi, pale anapopevuka kiakili ama
pale anapofanikiwa kujiunga na masomo ya sekondari ni lazima awe na malengo
kama nilivyoainisha hapo juu. Vivyo hivyo kwa mwanafunzi huyo pia, aweke
mipango mikakati ya muda mfupi yatakayo mwezesha kufikia malengo yake.
Division one na two vyote vinawezekana kama pande zote
zitaweka malengo ya kupata madaraja hayo kuanzia ngazi ya awali mtoto anapoanza
shule ama hata anapojiunga na masomo ya sekondari
4.
Kuwa na imani (Be faithful)
Labda hili nianze kulizungumzia kwa kutoa mfano, “……..siku zote mtu unapoelekea nyumbani
kwako/kwenu, unakuwa na tumaini kubwa zaidi hata ya 100% kwamba utafika
nyumbani. Hapana hata siku moja ambayo umewahi kuwa na wasiwasi kuwa yawezekana
pale unapoenda patasogea mbele kidogo ama karibu kidogo kukufuata. Wala
hutawaza kwamba yawezekana mahala pale pakawa angani ama kujichimbia
ardhini……..” Sasa kama wote tuanakua na imani hiyo basi hata kwenye masomo
yetu tukiweka imani hiyo hakika tutafanikisha lengo husika. Niwakumbushe pia
kwamba hapana hata siku moja unaweza kufikia lengo ukiwa umakaa ama kwa lugha
nyingine umebweteka yaani pasipo kujishughulisha, hata huyo anayesafiri kwenda
nyumbani kwake anakuwa na malengo kuwa atafika nyumbani kwake/kwao pale tu
atakapochukua hatua kadhaa kuelekea kule, lakini akiwa na malengo hayo ilihali
amekaa tutafananisha imani hiyo na ndoto za Abunuazi.
Kwa wale wanaoamini katika dini ya kikristo, kitabu
takatifu cha Bibilia katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waebrania sura ya kumi na
moja mlango ule wa kwanza hadi ule wa mwisho wa thelathini na mbili
(Ebr.11:1-32) sura yote hiyo inazungumzia imani na baadhi ya shuhudu zenye
kujenga imani (faithfulness) ya mtu. Sasa kwa kutumia maandiko hayo, nasi
tunaweza kuwa na imani kwamba division
one and two are within our scope and we can achieve, but don’t forget to
struggle for it.
5.
Kuwa mshindani (Be competent)
Katika mashindano yoyote hata ya kufukuza kuku au ya
kula andazi, kila mshiriki huwa anaingia pale akiwa na lengo la kwamba
atashinda. “……….Before trial, all
probabilities are equals to one……..” Hii inamaanisha kwamba kabla ya
michuano yoyote kuanza kila mtu uwezekano wake wa kuibuka mshindi ni moja.
Tuje kwa upande wa elimu na masomo, ila nianzie kwa
mzazi. Mzazi yeyote anayependa maendeleo ya mwanae hana budi kumtengenezea
mtoto wake mazingira ya kuwa mshindani. Kwa mfano, unaweza ukampa mtoto ahadi
ya kwamba kama atapata wastani wa alama kuanzia 61 na kuendelea utampeleka
mbuga za wanyama. Mtoto huyo akifanikiwa kupata mtimizie ahadi hiyo. Na kama
atashindwa kufikisha, usimkatishe tama, mpongeze kwa alama zile alizopata na
mpe ahadi nyingine bora zaidi ambayo itamfanya aongeze bidii zaidi.
Kwa upande wa wanafunzi, unapokuwa darasani huna budi
kujitengenezea alama ambazo unataka kuzipata kwa kila somo. Usiwe mzembe
ukijiwekea alama za chini kwani utakua ni sawa na yule mwizi anayeiba mfuko wa
kulia na kuweka mfuko wa kushoto. Panapotokea hujaweza kufikia malengo hayo,
jiulize kwanini mwenzako mnayesoma naye amefikisha alama hizo. Ikiwezekana
tengeneza urafiki naye ili akupe mbinu anazotumia kupata alama za juu.
6.
Fanya kusoma ni sehemu ya maisha (Make reading a part
and parcel of your daily life and routine)
Wanafunzi hujisifu kwa kufanikiwa kukesha wakiwa na
vitabu ama hujinasibu kwa kufanikiwa kusoma twisheni ya masomo yote. Jambo la
msingi la kufanya si kusoma kwa kukesha, ama kusoma twisheni ya masomo yote,
kwa maana njaa haimalizwi kwa kula sana bali pale utakapohisi. Mwanafunzi
anatakiwa atambua kwamba cheo na hadhi yake ni “uanafunzi” hivyo popote pale
atakapojisikia kufanya shughuli yake iliyokuu ya kusoma na asome. Pamoja na
hayo kila mwanafunzi na awe na ratiba yake ambayo itamfanya angalau kwa siku
nzima ya masaa 24 atumie masaa 8 kila siku kusoma. Masaa haya ni tofauti na
muda ambao mwalimu anakuwa darasani. Kwa kutumia ratiba hiyo mwanafunzi
atalazima kufuata na ikitokea ameikosea ratiba itabidi atafute muda wa ziada ya
kutilimiliza ratiba hiyo (find the alternative ways to supplement the lost
time). Vile vile pamoja na kuwa na ratiba hiyo, mwanafunzi hana budi kufanya
kazi yake kuu yaani kusoma pale anapojisikia kufanya hivyo hata kama ni nje ya
muda husika. Mfano, unapoweka ratiba kwamba kula ni saa nane mchana, ikitokea
ukasikia njaa saa sita mchana hutaacha kula. Vivyo hivyo na kusoma pia.
Nihitimishe
kwa kuwaasa pande zote na wadau wote wa elimu kwamba mustakabali na maendeleo
ya elimu yetu ipo mikononi mwetu na si mikononi mwa mwalimu na mwanafunzi
pekee. Tukumbuke ya kwamba hata mashine ili iweze kufanya kazi vizuri na kutoa
output nzuri lazima kuwe na ukaribu na resources zote zinazohitajika, ikiwa ni
pamoja na input sahihi, mwanadamu mwenye uzoefu, machine bora na nzima, umeme
na vingine vinavyotakiwa kuendesha mashine.
Pia
kwa upande wa wazazi tukumbuke kwamba mafanikio ya mtoto wako ni mafanikio
yako. Kwa walimu msisahau kwamba mafanikio ya mwanafunzi ni tuzo na inaongeza
credit kwenye taaluma yako. Na kwa mwanafunzi usisahau kwamba mafanikio yako ni
heshima kwa wazazi, jamaa, jamii na taifa lako kwa ujumla.
Imeandaliwa
na kuandikwa na,
Jina:
Ismail Mesaya
Simu:
+255 756 688 090
+255 712 814 285
0 comments:
Post a Comment