KARUDI BABA MMOJA
Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali
Wakataka na kauli iwafe maishani.
Akatamka mgonjwa, ninaumwa kwelikweli
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali
Roho naona yachinwa, kifo kimenikabili
Semeni niseme nini, kiwafae maishani.
Yakawatoka kinywani, maneno yenye akili
Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali
Urithi tunatamani, mali yetu ya halali
Sema iko wapi mali, itufae maishani?
Baba aliye kufani, akajibu lile swali
Ninakufa maskini, baba yenu sina hali
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali
Kama mnataka mali, mtayapata shambani
Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali
baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili
akili zetu nyembamba, hazijajua methali
kama tunataka mali, tutapataje shambani?
Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli
Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali
haya sasa buriani, kifo kimeniwasili
kama mnataka mali mtayapata shambani.
Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili
mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili
na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli
kama mnataka mali, tutayapata shambani.
Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali
Tangu zile za mibuni, hadi zitupazo wali
Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Shamba wakapalilia, bila kupata ajali
Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali
Wote wakashangilia, wakakumbuka kauli
Kama mnataka mali, mtayapata shambani
Wakanunua na ng’ombe, majike kwa mafahali
Wakapata na vikombe, mashine na baiskeli
Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali
Wakakiweka kibao, wakaandika kauli
“KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA SHAMBANI”.
0 comments:
Post a Comment