Nikisema tunaendeleza utamaduni wa chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi watu wengine inawakera na wanaanza kulalamika na kunilalamikia. Lakini sitoacha kusema kwa sababu mimi ni muumini wa falsafa mojawapo ya Steve Biko kwamba “I write what I like’.
Nililisema hili kabla ya Sitta kuchaguliwa na sasa narudia kulisema tena baada ya yeye kuchaguliwa. Chama tawala wamekaa kwenye caucus yao wakamenyana weee hatimaye wakachagua mgombea wao kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na makamu wake. Wakaibuka na Samweli Sitta. Kitendo cha kukaa kwenye caucus ya kichama ni kwamba huyu ni mgombea wa chama. Kazi za caucus za vyama huwa ni kuweka misimamo ya kichama katika mambo ya kisera. Ndio kusema CCM walipompitisha Sitta kugombea wana imani naye katika kusimamia mambo yao kichama katika katiba. Ajabu ni kwamba wapinzani wote walimshangilia Sitta kabla na baada ya kuchaguliwa. Wanamshangilia mgombea aliyewekwa na chama pinzani kwao!! Msingi mkubwa katika mfumo wa vyama vingi ni ushindani wa kisiasa. Tunaporuhusu mgombea wa chama kimoja anapita katika uchaguzi bila upinzani kutoka chama cha upinzani maana yake ni nini? Si ndio hiyo kuendelea na utamaduni wa chama kimoja katika mfumo wa vyama vingi?
Wapinzani walishindwaje kuweka mgombea mmoja kwa upande wao ili ashindane na mgombea wa CCM? Ukijumlisha wabunge wa CHADEMA, CUF, NCCR, TLP na UDP pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CUF wanafika 110. Ndio kusema walikuwa na mtaji wa kuanzia. Kazi kubwa ilikuwa ni kushawishi wajumbe kutoka kwenye kundi la watu 201 ambao naamini wasingekosa nusu ya wajumbe hawa. Kwa hiyo kulikuwa na uwezekano mkubwa sana mgombea wa upinzani kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM Ndungu Sitta. Sasa swali ambalo lazima tujiulize kwa nini wapinzani hawakusimamisha mgombea? Kwamba wanamkubali sana Sitta au walimuogopa? Ikiwa hivi ndivyo, tutarajie kuwa na mgombea wa CCM pekee wa urais kwenye uchaguzi mkuu mwakani kama ikitokea Sitta ndiyo mgombea wa CCM? Hivi ndivi upinzani unavyopaswa kuwa au tunataniana?
Kwa maoni yangu ni kwamba wapinzani walikosea sana kuogopa kuweka mgombea kwa kumuogopa Sitta. Nawashauri wasirudie kosa hili katika uchaguzi wa makamu mwenyekiti. Wamtafute mwanamama mmojawapo kutoka Zanzibar apambane na mgombea wa CCM. Anaweza asishinde kutokana na namba kubwa ya wana CCM ndani ya bunge hili, lakini ni muhimu wakashindana. Kuacha mgombea mmoja kutoka chama tawala anapita bila kupingwa ni taswira mbaya sana kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini. Ningeelewa kama hawa wangekuwa wanagombea kivyao badala ya kusimamishwa na chama chao. Lakini inapotokea chama tawala kinateua mgombea ni muhimu wapinzani pia wawe wanatoa mgombea. Vinginevyo, wataendelea kujenga taswira kwamba wapinzani wawekeze nguvu kwenye nafasi za chini kama ubunge na udiwani lakini waachane na ndoto za urais. Hii ni dhana dhaifu na wapinzani wanapaswa kuikemea na kuikataa kwa nguvu zote tena kwa vitendo.
0 comments:
Post a Comment