Lengo la Uongozi lisiwe Madaraka bali Mabadiliko yaliyojaa Utu – LEMA
Nimekuwa nikifuatilia mijadala mbali mbali inayohusu CDM katika vyombo vya habari na hususani mitandao ya jamii , nimeona fikra nyingi halali na haramu na nikajiridhisha kwa uhalisia kabisa kuwa Taifa linahitaji ukombozi mkubwa wa fikra . Watu wengi wanaopita katika mitandao ya jamii na kutoa maoni juu ya hali ya Nchi na Vyama vya siasa na matukio mengine mbali mbali unaweza kabisa kusema ni kundi kubwa ambalo lina mwanga kiasi katika matumizi ya vifaa vya electroniki au komputya na kundi hili linaweza kutajwa kama kundi lenye uelewa wa mambo japo kidogo .
Hata hivyo kuna tofauti kubwa sana kama utajaribu kufanya utafiti kupitia maandiko yao mbali mbali na michango yao katika kuelimisha Jamii , pengine tofauti hii kubwa inatokana na hisia za kishabiki ambazo zinapewa kipaumbele kuliko mambo ya msingi yanayoweza kuleta fikra chanya katika Jamii . Nimeona maandiko mbali mbali kuhusu Chama changu ninachokitumikia na Nchi yangu , nimekuwa nikishangazwa na ushauri wa maadui zetu kuhusu mustakabali wa Chama Chetu , Maadui zetu ambao wanatupiga kila siku , kutubambikia kesi , kuuwa watu katika mikutano yetu na mateso mbali mbali mabaya kuna saa unawaona wakijaribu kuhimiza umoja wetu kama nguzo muhimu ya kuwatoa madarakani wao . Hili ni fumbo kubwa kwetu ?
CHADEMA itachukua Dola 2015 . Changamoto na matatizo yeyote yatakayoonekana sasa na hapo baadae hayatakuwa kikwazo katika ndoto hii muhimu bali ni ufunguo katika kufikia haya mafanikio kwa ufasaha zaidi . Natambua kuwa Viongozi tunawajibu muhimu katika kujenga Demokrasia isiyo na chembe ya hofu wala uoga kwani katika ujenzi wa demokrasia ya ukweli ni vyema tukaendelea kufundisha watu namna muhimu ya kushinda hofu na uoga kama nguzo kuu ya ulinzi wa rasilimali na Nchi yao , Chama hiki kitakuwepo na kitaendela kuwepo na hakuna Mtu wala kelele za kuangusha Chama hiki natambua juhudi kubwa zinafanyika ndani yetu na nje yetu kuangusha Chama hiki na faraja ya maadui imekosa hekima kwani kuua chama Kikuu cha upinzani Nchini ni kuua demokrasia na kuua demokrasia sio faida kwa watawala kwani wananchi wanapotaka mabadiliko kama wakiyakosa kwa haki na njia sahii watayatafuta kwa silaha , kwa hiyo ukuaji wa demokrasia ni muhimu katika ulinzi wa Amani ya Nchi , ingekuwa kuuwa Upinzani na Chadema ni kumzorotesha Mtu binafsi na sio maono muhimu katika utawala wa Nchi yetu basi Chama hiki kingeweza kufa , lakini kwa sababu sio hivyo basi ni vyema maadui wakajua wanafanya kazi ambayo hawatafaulu kwani Demokrasi , Haki , Ukweli , Usawa na Utu ni tabia ya Mungu na hivyo Chadema ni mpango wa Mungu kelele za shetani na Watu wake haziwezi kuangusha Mbingu .
Wanachama wetu ni muhimu wakajua CCM ni adui wetu si kwa sababu ya rangi ya bendera yao ila ni kwa sababu ya matendo yao , hatuwachukii CCM kwa sababu rangi yao ni kijani isipokuwa tunachukia matendo yao na tabia zao ambazo zimezorotesha Taifa katika kila Nyanja mbali mbali na huu ndio ugomvi wetu mkubwa na Chama hiki katili .
Tulipowafukuza Madiwani Arusha nilisema hivi “ Kama Madiwani wanaweza kukaidi agizo la Kamati kuu juu ya mahusiano yenye usaliti katika baraza la Halmashauri ya Jiji la Arusha na sisi tukaona ni vyema wao kuendelea kwa sababu ya kuhofia uchaguzi , Je tutawezaje kama Chama cha Upinzani kikubwa kuwanyooshea Chama tawala vidole kwa kushindwa kuwawajibisha viongozi wake wenye tuhuma mbali mbali tena waliokuwa na nyadhifa kubwa Serikalini ? . Kuliko tuchukue Dola 2015 na Watu wasio na rangi inayojulikana ni bora tuendelee kuwa Chama cha Upinzani , kwani lengo la msingi la Chadema lisiwe kutafuta heshima na utukufu katika uongozi bali mabadiliko na utu wa kweli katika Taifa letu .
Huu ni wakati muhimu kuelekea uchaguzi mkuu 2015 ambao ni lazima tutafakari sana , je tunataka kura kwa ajili ya utawala au kura kwa ajili ya mabadiliko ? Maadui zetu wa nje ni wepesi sana wamekwishalegea kinachosubiriwa ni juhudi zetu ili kufika kileleni , hatuwezi kufika kileleni huku wasaliti wakiwa ndani yetu ni lazima kama Chama sasa tuchukue hatua . Hatua hizi ngumu haziwezi kuwa na test ya raha bali uchungu ambao ni lazima uvumiliwe ili kufikia malengo muhimu , Mwanamke mjamzito ana njia mbili ya kujifungua Mtoto , moja ni kwa njia ya kawaida na pili ni njia ya upasuaji na zote zina maumivu na mateso lakini baada ya hapo Mtoto huwa anakuja na furaha na faraja na zawadi mbali mbali na Mama kusahau changamoto zote alizopitia . CHADEMA ni tumaini kubwa Tanzania ni muhimu sasa kuchagua njia muhimu ya kusafisha Chama kabla mambo hayajifika mbali na kama tukikosa madaraka na sababu ikawa ilikuwa kujisafisha wenyewe basi sababu hii itakuwa ina maana kubwa kwa sisi kutokuchukua madaraka na utawala wa Nchi hii , kwani lengo lisiwe madaraka bila mabadiliko bali Mabadiliko na mamlaka ili kuweza kurudisha utawala unaojali haki , utu na heshima katika Taifa hili .
Katika msingi wowote wa maamuzi magumu lazima tutambue kwamba , kelele , dhihaka , matusi , kashfa vitainuka kwa kiwango cha juu na kwa msaada mkubwa wa maadui zetu lakini ni vyema tukatambua kuwa Uongozi ni kukumbana na Changamoto mbali mbali kama vile hofu , mashaka na vishawishi na kuamua kuzishinda kama ambavyo Wright Brothers walifanya katika ugunduzi na utafiti wa kurusha ndege Duniani hata hivyo faida kubwa tuliyo nayo ni kuwa Wanachama wetu wamekuwa wengi sana kwa hiyo hatuna Mtu maarufu tena ila tuna CHAMA maarufu na mashuhuri , tulipofukuza Madiwani Arusha kuna Watu walisema Chadema imekwisha Arusha na wengine walijitapa kuwa wao walikuwa wanakubalika kuliko Chama lakini uchaguzi wa hivi karibuni wa Madiwani unaonyesha kuwa CDM Arusha imeshinda kwa aslimia kubwa kuliko ilivyokuwa mwaka 2015 tena kwa Watu wapya na wenye sura ngeni katika Siasa , pamoja na kuwa maamuzi ya kufukuza madiwani yalipigiwa kelele sana lakini msingi wa kufukuza madiwani ulikuwa muhimu kwa afya ya Chama na Nchi kwani utawala usiokuwa na nidhamu ni sawa na kupanda mahindi katika tiles , japo kuwa tiles ni nzuri kuliko udongo lakini mahindi hayawezi kuota na kwa hiyo kwa kadri utovu wa nidhamu unavyokuwa sugu ndivyo ambavyo roho ya usaliti inakuwa muhimu kwani “ you can not feel bad to discourage the move that you do not respect “ Ukitafakari kwa makini sana utagundua kuwa historia haijawi kuwapa kipaumbele wasaliti hata siku moja, kwa hiyo ni muhimu wanaosaliti hii kazi muhimu wakajua hivyo kwamba heshima yetu ni Chama Chetu na sio Majina yetu kwani tukijenga Chama imara hata kama hatutakuwepo Chama kitaendelea kuwepo na hapa kanuni ni moja tu “ Nguvu kubwa ya mshikamano na Upendo wetu itakapokuwa muhimu kwetu kuliko Ubinafsi wetu na Sifa binafsi basi safari itakuwa imefika mwisho “ Sio tu kwa kushinda dola bali kwa kubadilisha mitazamo ya fikra katika Siasa jambo ambalo ni muhimu sana kwa wakati huu kuliko hata kushika madaraka .
Kuna uoga mkubwa sana katika Taifa hili ni vyema tukajenga kizazi kinachoweza kushinda hofu na kusimamia Nchi yao katika haki na kweli kwani ni hatari sana kwamba leo ndani ya Bunge hata kutaja majina ya wezi wa mali ya Umma eti inahitaji ITIFAKI , lakini katika hatua hii muhimu ya kuondoa hofu na kufundisha ujasiri Jamii lazima Viongozi wakubali kuwa wataitwa majina yote mabaya kama ambavyo Mandela aliitwa wakati alipokuwa anataka utu wa Watu wake .
" Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni uoga "
Godbless J Lema
0 comments:
Post a Comment