JE,
NI HALALI KUTANGAZA NA KUSHEREKEA TAREHE 9/12 KAMA SIKU YA UHURU WA TANZANIA???
Ilikuwa mwaka 1954,
Julius K. Nyerere mwalimu wa shule ya sekondari na mmojawapo kati ya
watanganyika wawili waliokuwa na elimu ya chuo kikuu walipounda chama cha TANU,
ambacho kilichochea na kusukuma harakati za kudai uhuru na hatimaye tarehe
9/12/1961 nchi ya Tanganyika ilipata uhuru na Mwl. J.K.Nyerere akawa waziri
mkuu chini ya katiba mpya.
Mwaka mmoja baadaye
yaani 9/12/1962, Tanganyika ilikuwa Jamhuri na Mwl. J.K Nyerere akawa rais wa
kwanza.
Mwaka 1964 April 26,
Mwl. J.K.Nyerere (Rais wa Jamhuri ya Tanganyika) na Sheikh Abeid Aman Karume
(Rais wa serikali ya watu wa Zanzibar) waliridhia na kuazimia kuunganisha nchi
zao yaani Tanganyika na Zanzibar, na kuunda NCHI MPYA ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Muungano huu wa nchi
hizi mbili ulififisha na kudhoofisha uwepo wa nchi washirika yaani Tanganyika
na Zanzibar ili kuipa nafasi nchi mpya ya Tanzania kujitengenezea mipaka na
historia yake. Kwa tafasiri nyepesi tunaweza kusema historia ya Tanganyika
ilibaki kama historia ya nchi mshirika yaani Tanganyika na haikurithiwa ama
kukasimiwa kuwa historia ya TANZANIA. Vivyo hivyo kwa upande wa Zanzibar. Hii
ina maana kwamba historia ya nchi hii mpya ya Tanzania ilipaswa kuanza
kutengenezwa siku na tarehe ilipozaliwa yaani 26/04/1964. Kutengenezwa kwa
historia hii ya Tanzania haina maana ya kufuta historia za nchi washirika, kama
vile ujio wa wakoloni, harakati za mapambano ya uhuru na historia yote kabla ya
muungano kama utamaduni, utawala, mila na desturi.
Hoja yangu hiyo
inatokana na ukweli kwamba muungano wetu haukuasisiwa ili kufuta historia za
nchi washirika. Ili kutoa nguvu kwa nchi mpya ya Tanzania kujitengenezea
historia yake yapaswa shughuli zote za kihistoria za nchi washirika kusimamiwa
na kuasisiwa na nchi husika yaani nchi mshirika. Kwa lugha nyepesi tunaweza
kusema masuala kama vile maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika, yapaswa
kufanywa na kusimamiwa na nchi mshirika yaani Tanganyika na sio Tanzania. Vivyo
hivyo kwa masuala ya mapinduzi ya Zanzibar yanapaswa kufanywa na kusimamiwa na
serikali ya Zanzibar (kama ilivyo sasa). Suala pekee ambalo linapaswa kufanywa
chini ya mwamvuli wa Tanzania (yaani muungano) ni maadhimisho ya siku ya
muungano tu. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumetoa nafasi kwa nchi washirika
kuendelea kuenzi na kukumbuka historia yao, na vile vile tutakuwa tumetoa wigo
mpana kwa nchi mpya ya Tanzania kujitengenezea historia yake.
Hali ilivyo kwasasa
Kwasasa tunaona kwamba
masuala yote yanayohusu historia ya Tanganyika yamekasimishwa kwa nchi mpya ya
Tanzania na yale yanayohusu Zanzibar yamebaki kwa wazanzibar. Hii inadhihirishwa pale siku ya tarehe
9/12/1961 siku ambayo nchi ya Tanganyika ilipata uhuru, inapogeuzwa na kufanywa
ni siku ya uhuru wa Tanzania. Maswali ya msingi ya kujiuliza ni:
i)
Je, Nchi ya Tanzania iliwahi kutawaliwa?
Je ilitawaliwa na koloni gani?
ii)
Je, Nchi ya Tanzania iliyozaliwa 1964
kwa muungano wa nchi mbili huru yaani Tanganyika na Zanzibar, ilipata uhuru
lini? Chini ya chama gani? Kutoka kwa ukoloni wa nchi gani? Muasisi wa harakati
hizo alikuwa nani?
iii)
Je, Ni halali kufuta historia ya
Tanganyika na kuikasimisha kwa nchi mpya ya Tanzania?
iv)
Je, Hatutakuwa tunadanganya na kupotosha
vizazi vijavyo kwa kuwarizisha kwamba Tanzania ilipata uhuru desemba 9 1961?
v)
Je, Ni kwanini linashindikana kwa hili
la historia ya Tanzania kuandikwa kama ilivyo pasipo kuchanganya na historia ya
Tanganyika, lakini limewezekana kwa historia ya TANU kutenganishwa na kuandikwa
tofauti na historia ya CCM ambayo nayo imetokana na muungano wa vyama vya ASP
na TANU? Yaani leo hii hatuwezi kujinasibu kwamba CCM ilizaliwa rasmi tarehe
7/7/1954 siku ambayo TANU ilizaliwa, kama tunavyofanya kwa kusema Tanzania
ilipata uhuru 1961 siku ambayo Tanganyika ndiyo ilipata uhuru.
vi)
Je, Ni nani wa kutunusuru kutoka kwenye
upotoshaji huu kama wasomi, wanasiasa na makundi mbalimbali ya kijamii
yamejikita kuhalalisha uongo huu bila kukosoa?
Hatuwezi kukwepa
kukabiliana na masawali haya kama kweli tuna nia ya dhati ya kulinda na kuenzi
historia za nchi washirika wa Muungano, na vile vile kukuza na kuendeleza nchi
hii mpya ya Tanzania ambayo ina miaka 50 kamili kwenye uso wa dunia toka
ilipozaliwa.
Kwa kuendelea kutenda
kama tunavyofanya kwa sasa kwa kuruhusu kwa makusudi kufutika kwa historia ya
nchi ya Tanganyika, mambo kadhaa nayaona:
a)
Kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar
haukuwa na lengo la kuunganisha nchi mbili huru na zenye historia kamili, bali
ulikuwa ni ujanja wa nchi moja kubadili jina na kuitawala nchi nyingine. Yaani
nchi ya Tanganyika ilibadili jina na kuitwa Jamhuri ya Tanzania na kutawala
nchi ya Zanzibar. Hii inadhihirishwa pale tunapoona masuala yote ya kihistoria,
kiutawala, kikatiba, kisiasa, mila na tamaduni za Tanganyika zikikasimiwa na
kurithiwa na nchi mpya TANZANIA
b)
Kuwa kitendo cha nchi ya Tanzania
kutumia rasilimali fedha ambazo zimekusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato
ambazo ni za pande zote za muungano, vyombo vya usalama, utawala wa nchi ya
Tanzania (rais) kuandaa na kutekeleza shughuli zihusuyo historia ya nchi ya Tanganyika, ni unyonyaji na ufisadi wa
rasilimali za Zanzibar kwani siku ya maadhimisho ya mapinduzi ya Zanzibar
hufanywa na serikali ya watu wa Zanzibar na sio serikali ya muungano.
c)
Kuwa muungano umelenga kwa makusudi
kufuta nchi ya Tanganyika na historia yake katika uso wa dunia. Hii
inadhibitishwa pale tunapoona masuala yote ya kihistoria yanayohusu Tanganyika
yakirizishwa kwa nchi ya Tanzania. Vile vile kitendo cha kuondoa uhalali wa nchi
ya Tanganyika kikatiba na kufanya katiba ya Tanzania kuwa ndio katiba ya
Tanganyika ni kuhalalisha kile nilichokiita Tanganyika kubadili jina kwa lengo
la kutawala Zanzibar.
Hitimisho
Ili tusihukumiwe na
historia na tuwatendee haki vizazi vijavyo hatuna budi kutenganisha masuala ya
Tanganyika na yale yanayohusu Tanzania. Kwa mfano masuala ya maadhimisho ya
siku ya uhuru wa Tanganyika, yaani tarehe 9/12 yanapaswa kusimamiwa na utawala
wa nchi ya Tanganyika ambapo kwa katiba ya sasa yanapaswa kusimamiwa na Waziri
mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ndiye msimamizi wa shughuli za
kiutawala zihusuyo Tanganyika.
Vile vile hatuna budi
kubadili katiba yetu ili kutoa mwanya kwa nchi washirika wa muungano kuenzi
historia zao na nchi mpya ya Tanzania kujitengenezea historia yake.
Pia tubadili maandiko
yetu yanayotumiwa kama zana za kufundishia mashuleni na tuweke wazi ukweli kuwa
Tanzania haijawahi kutawaliwa bali imezaliwa rasmi 26/04/1964 kwa muungano wa nchi
mbili huru zenye historia zao. Hii itasaidia kuondoa fikara kwamba tarehe
9/12/1961 ni siku ya uhuru wa Tanzania. Vile vile hii itasaidia kuenziwa kwa
historia ya nchi hizi washirika na historia ya Tanzania (nchi mpya) kujengwa
kwenye fikra za vijana na vizazi vijavyo.
Hongera Tanganyika kwa
kufikisha miaka 53 ya uhuru. Utulivu wako uendelee kudumu daima kwa vizazi na
vizazi.
@Ole Mesaya
Cont: +255 756 688 090
0 comments:
Post a Comment