
Salamu zangu zikufikia popote ulipo mwana wa nchi ya Tanzania. Nisitaje sentensi nyingi kwenye utangulizi huu ili nisikuchoshe kwa lahaja tamu zilizojawa na pijini za kiharakati na ukombozi.
Jana nilienda kwenye kata yangu mpya ya Muriet kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili nipate fursa ya kushiriki Octoba mwaka huu kwenye harakati za kumpata kiongozi bora atakayelinda na kutetea rasilimali za nchi yangu na kutumika kwa maslahi na manufaa ya wananchi wote.
Baada ya kumaliza zoezi hilo nilirejea kwenye maskani yangu mkoa wa Kilimanjaro na kujipumzisha kwa uchovu wa siku nzima. Baada ya kuvuta blanketi na kufumba macho nilipitiwa na usingizi mnono ambao ulinisukuma kwenye ndoto sadifu na tukio nililoshughulika nalo siku nzima ya jana.
Ndoto hii ilianza kwa kunivuta kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 na ushiriki wangu. Hii ndoto ilikuwa murua kwani ilifanya kama kila mtu anavyotaka iwe. Nasema imenitendea haki kwasababu, baada ya kupiga kura nilikaa hatua mia kusubiri matokeo yatangazwe na Mungu sio ajizi mgombea niliyemchagua ndiye aliyeshinda.
Ilikuwa siku ya tarehe 25/10/2015, niliposhuka na Ndugu zangu Musa Kumondawa na familiya yake, Meleji Kitumi, Happy, Thomas Siodi, Lemburis Njivainey na wadau wengine. Baada ya kufika kwenye vituo vyetu tulipiga kura na wote tulibaki hatua mia kulinda kura zetu isipokuwa Bwana Musa Kumondawa ambaye tulimpakiza kwenye Rav 4 yeye pamoja na familiya yake wakapumzike wasubiri matokeo.
Ilipohitimu saa saba usiku matokeo yakatangazwa rasmi na msimamizi mkuu wa uchaguzi wa kata ya Muriet kwamba Mshindi wetu alikuwa ni MUSA K MOLLEL. Nilibubujikwa na machozi ya furaha na kujikuta naimba wimbo wote wa “Tuwamwage mafisadi”
Baada ya matokeo kutangazwa tulizunguka kata yote ya Muriet kuanzia kwa Morombo hadi Nadosoito kusini tukiimba “Karibu Yoshua utufikishe Kaanani”. Tulipata mapokezi ya kutosha kila mtaa tuliofika na kilichonishangaaza ni pale nilipowaona kina mama wakitandaza khanga na mitandio chini ili “Yoshua” apate kupita. Nilizidi kushangazwa na malaigwanani wa rika zote kuanzia nyangulo hadi nyagusi, kwa kumkabithi “Yoshua” Olenywa, Oikuma na Oiburangeti. Hiyo ni ishara ya kukabithiwa uongozi wa jamii na familia zote bila kujali dini, rangi, kabila nk. Viongozi wa Imuran (Ngopir) nao walimpa embere sirwa wakiashiria kumpa jukumu la kuwa mlinzi kiongozi wa jamii yote. Haikuishia hapo tu, wakinamama nao walimpa engiliko, engoti pamoja na emoti. Hii iliashiria kwamba anakabithiwa jukumu la kuhakikisha jamii yote inapata lishe bora pamoja na shibe kwa kila kaya.
Wakati nikiendelea kushangaa hayo nilisikia wimbo wa wazee ukiimba “eewo emunyani enyoito endang’amu”. Kina mama nao wakaanza kuiba “Inyo yeyo taramatisho nasirie etii engijape engai”.... Kwa kweli nilishuhudi usiku ambao niliadithiwa na Babu yangu Mzee Simanga jinsi ilivyokuwa tarehe 9/12/1961 siku ya uhuru.
Baada ya shamrashamra hizo za usiku kucha, Diwani wetu mpya aliapishwa na akaanza majukumu yake mapya kwa kufanya yafuatayo:
- Alianza kwa kuwaita na kufanya mazungumzo na wale wote waliokuwa wapinzani wake katika uchaguzi mkuu kutoka vyama vyote na kufanya nao mazungumzo juu ya kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kufikia maisha bora kwa kila mwana-Muriet na maendeleo ya kata kwa ujumla.
- Baada ya zoezi hilo kufana na kufurahiwa na wote, Diwani huyu kijana alikutana na viongozi wote wa mitaa ya kata ya Muriet kila mmoja kwa muda wake ili kujua changamoto kubwa na malengo yake kama kiongozi wa mtaa husika. Baada ya kuwasikiliza wote alifanya nao kikao cha ndani kwa kuchambua changamoto za kila mtaa na kuweka bayana vipaumbele anuwai kwa kila mtaa.
- Aliwaita viongozi wastaafuna waliomaliza muda yao ya kiuongozi wa kata ya Muriet na kuzungumza nao juu ya maendeleo ya jamii za watu wa Muriet na nafasi zao katika kulifanikisha hilo.
- Aliwaita wazee wa mila (Laigwana) wote wa rika zote katika kata ya muriet na kufanya nao mazaungumzo juu ya namna ya kuimarisha uchumi na pato la kaya. Vile vile kurejesha heshima, nidhamu na utii kwa rika zote ili kujenga jamii imara na chapakazi na yenye upendo usio wa kinafiki.
- Alikutana na wazee wa kila mtaa na kufanya nao mazungumzo juu ya changamoto sugu zilizopo kwenye mitaa hiyo na hatua anuwai zilizokwisha kuchukuliwa na zilipoishia. Vile vile ili kuimarisha ushirikiano na upendo kwenye jamii aliona kuna haja ya kuashirikisha wazee hawa.
- Baada ya wazee, alitoa muda wake kukutana na kina mama wa kila mtaa akiamini kwamba watu hawa ndio wanaobeba familia. Alipata kuzungumza nao namna ya kuanzisha uchumi mbadala kwa kila mtaa ili kuimarisha na kupandisha uchumi na pato la kaya.
- Alizungumza na vijana ambao ndio nguvu kazi ya kila mtaa kwa kufahamu ni namna gani wanaweza kujiajiri na kuacha kukimbia nje ya kata yao na familia zao wakati kuna rasilimali nyingi.
- Alipata muda wa kuzungumza na wafanyabiashara wakubwa na matajiri wanaoishi ama kuendesha shughuli zao ama ni wazaliwa wa kata ya muriet juu ya namna ya kuongeza uwekezaji katika kata hii na kuangalia fursa zilizopo ili kuinua wigo wa ajira na pato la kata kwa ujumla.
- Alimalizia kwa kufanya kikao na wasomi wote wazaliwa na wanaoishi kata ya muriet ili kujua mbinu na mikakati ya kuimarisha uchumi na pato la kaya na maendeleo ya kata kwa ujumla. Pia hakusita kuwajuza nafasi zao katika kurejesha matunda ya elimu yao nyumbani ili kupanua wigo wa ajira na uwekezaji kwa wakazi wa kata yao.
Baada ya kuzungumza na makundi haya yote kwenye jamii, alipita kila mtaa na kufanya mkutano wa hadhara kuwashukuru wananchi kwa kumpa ridhaa na kuweka bayana vipaumbele vyake kwa kila mtaa na kata kwa ujumla kulingana na mawazo aliyoyapata kutoka kwenye mazungumzo aliyoyafanya na makundi yote. Vile vile alisisitiza juu ya umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na nafasi ya kila mmoja katika kuchangia maendeleo ya kaya na kata kwa ujumla.
Baada ya siku mia, nilianza kuona mabadiliko makubwa sana kwenye kata ya Muriet na viunga vyake. Niliona ufunguzi wa Soko kubwa la En’donyo kumur. Soko hili liliwangunganisha wafanyabiashara wa Mirongoinne, Olokii, Kwa morombo, Mbauda na kisongo-duka bovu. Soko hili liliwapa furasa za kujiajiri vijana zaidi ya 500 wa kata ya Muriet na vile vile kina mama wa kimasai ambao walikuwa wakisafiri na mkaa kutoka Endepesi hadi Sanawari, walijiajiri kwenye biashara ndogo ndodo za mboga mboga, mitumba, mama ntilie na hata kufungua vijiwe vya kudumu vya kuuzia mkaa kwa jumla na rejareja.
Ufunguzi wa soko hilo, ulisukuma ukuaji wa shughuli zingine za kiuchumi kama vile uwekezaji, ujenzi, useremala na biashara ndogo ndogo kwa makundi yote ya kijamii. Huduma za kijamii nazo zilianza kuvutwa na uwepo wa soko hili, ambapo nilishuhudiwa kufunguliwa kwa kituo cha afya cha Mlimani, Kisima kikubwa cha kuvuna maji ya mvua cha Mlimani na pia Bomba kubwa la maji kutoka mto Themi kupitia kwa Ole Njoolay hadi en’donyo kumur. Barabara kutoka Mirongoine hadi en’donyo kumur kupitia kwa Megilienanga nayo ilijengwa kwa kiwango cha moram. Barabara ya kutoka Olokii kupitia Sindila, Kwa Mzee Mesaya hadi en’donyokumur nayo ilijengwa kwa kiwango cha moram. Nilishuhudia pia kufunguliwa kwa barabara ya magari makubwa inayotoka Kwa morombo kupitia Nadosoito Pr hadi En’donyokumur ikifunguliwa na kuanza kutumika rasmi.
Dah!!! Kwa kweli ilikuwa ni ndoto ambayo sikutaka kuikatiza. Nilishuhudia pia kufunguliwa kwa kituo kidogo cha machinjio eneo la En’donyo Kumur. Kituo hiki kilitoa fursa ya upatikanaji wa nyama kwa kaya zilizopo mitaa yote ya kata ya Muriet na vilevile kutoa soko la uhakika kwa jamii za watu wa Muriet na maeneo jirani ambao wengi wao ni wafugaji.
Eneo la Mlimani (En’donyo KUmur) liligeuka Muriet business center. Kutokana na kukuwa kwa eneo hili, mapato ya ndani ya kata hii yaliongezaka zaidi ya 500%. Ukuwaji wa pato hili la kata, lilisababisha kuongezeka kwa huduma za kijamii kama shule na hosipitali. Vile vile huduma inayotolewa kwenye vituo hivyo iliboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Lilifunguliwa geti maeneo ya shule ya msingi nadosoito ambalo lilitumiwa na watalii kufika eneo linalosadikiwa kwamba liliangukiwa na Kimondo, almaarufu kwa jina la “Shimo la Kikofu”. Hii ilifanya kuongezeka kwa fedha za kigeni na kupaa kwa pato la kata hii na vijana wengi kupata ajira.
Nilishuhudia kampuni za simu zikikimbizana kuweka minara yao katika eneo la Mlimani na wawekezaji wengi kujenga hoteli za kitalii karibu na eneo la kikofu ili kukithi haja na mahitaji ya watalii wa nje na ndani.
Nilishuhudia wasomi wengi wa kata ya Muriet wakirudi na kuungana na vijana wazawa wa kule kuanzisha vikundi vidogo vidogo vya SACCOS na VICOBA. Vikundi hivi vikakuwa na kuwawezesha vijana wengi wakiweza kukopa na kujiendeleza kwenye shughuli zao za kimaendeleo.
Kutokana na jitahada binafsi za kiongozi huyu, serikali ikampa ekari 2500 za eneo la THG ambapo alifanya shamba la kijiji na kuhakikisha maji ya mto Themi yanatumika kunyeshea shamba hilo na vile vile kuotesha mazao yanayostahili ukame kwa upande ambao haukufikiwa na maji. Alihimiza kuoteshwa kwa mazao ya Karanga, Viazi, Mihogo, Mtama, Uwele na maharage. Shamba hili lilikuwa linaendeshwa na serikali ya kata kwa kushirikiana serikali ya wilaya Arusha. Lilikuwa ni jukumu la vikao vya mtaa kutoa watu wa kushiriki kwenye shughuli za shamba hilo. Pato lililokuwa linapatikana asilimia 50% baada ya makato ilitumika kuendeleza shamba hilo ikiwa ni pamoja na kuwapa ujira wale wote ambao walitolewa na mtaa kushiriki kwenye shughuli za shamba hilo kwa kila siku. Asilimia 10 ilienda moja kwa moja kwenye pato la kata. Asilimia 30 iligawanywa kwa sawa kwa serikali ya mtaa ili kukamilisha vipaumbele vyao vya kimaendeleo na asilimia 10 iliyobaki ilitumika kuwatunza wazee wasiojiweza na kina mama wajane wasiojiweza wa kata ya Muriet.
Kwa kweli niliona kata mpya ya Muriet ambayo ilikuwa inawanufaisha wakazi wote wa Muriet na kutengeneza nguzo dhabiti za maendeleo kwa vizazi vijavyo.
OOOh!!!! Nilishtushwa na sauti ya Azana ikiashiria kwamba saa 11 alfajiri ilishafika. Hapo ndipo ndoto yangu ilipokata na kujikuta nikishangilia na kuburudika moyoni kwa kuota ndoto ambayo inanusuru hali duni ya maisha ya watu wa kata yangu na kutengeza misingi mizuri ya maendeleo yenye tija kwa watu na makundi yote.
Sasa kazi ni kwetu kuhakikisha tunajiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katka uchaguzi mkuu ujayo ili kumpata kiongozi bora wa ndoto yangu amabaye ataweza kufikisha kata ya Muriet sehemu ndoto yangu ilipoishia.
Imeandaliwa na kuandikwa na
Mesaya Ismail
Cont: +255 (0) 756 688 090
+255 (0) 712 814 285
Email: ismail.mesaya@gmail.com
June 2015
0 comments:
Post a Comment