Music

Saturday, July 20, 2013

KAMA LOWASA NI MSAFI, SASA NANI MCHAFU CCM?

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimemaliza vikao vyake mjini Dodoma wiki iliyopita. Kama kawaida yake kwa siku za karibuni, kumalizika kwa vikao vya chama hicho, ni mwanzo wa mnyukano mpya ndani ya chama na maandalizi ya harakati mpya za kumalizana. 
Kama wengi wetu tulivyotabiri tangu Aprili, mwaka huu kuwa dhana ya kujivua gamba ndani ya CCM ilikuwadaganya toto, imetokea kweli na safari hii Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) imegwaya mbele ya ubabe wa mafisadi na kuishia kuagiza eti suala hilo lirudishwe katika vikao vya ngazi za chini.
Pamoja na utitiri na urefu wa vikao vya maandalizi ya NEC, haikuwezekana kutekeleza dhana ya kujivua gamba kama ambavyo ilikuwa ikipigiwa chapuo na watendaji wapya wa sekretariati ya CCM, wakiongozwana Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. 
Alikuwa ni Nape pamoja na wenzake kina John Chiligati, Wilson Mukama na Mzee Pius Msekwa waliorindima baada ya kikao cha NEC ya April 2011, wakidai mafisadi ni ama wajiondoe haraka ndani ya chama au wafukuzwe ndani ya siku 90. 
Walianza kampeni hiyo baada ya kikao hicho wakisafiri kwa barabara na kufanya mikutano katika miji ya Dodoma, Morogoro, Chalinze na kupokelewa jijini Dar es Salaam kwa mbwembwe nyingi. Rais Kikwete alinukuliwa baadaye kidogo akiwa katika uzinduzi wa nyimbo za Injili kuwa aliyokuwa akiyasema Nape Nnauye yalikuwa na baraka za Chama cha Mapinduzi.
Kwa mshangao wa wengi, katika kikao kilichopita, ambacho kilitarajiwa kutekeleza azimio muhimu la NEC ya April, aliibuka Edward Lowassa na kudai bila kigugumizi kuwa alichokifanya akiwa Waziri Mkuu na kutafsiriwa kuwa ni fisadi, kilikuwa na baraka za Rais Kikwete, Baraza la Mawaziri na timu ya makatibu wakuu. Alilalamika wazi kwa jinsi alivyoendelea kudhalilishwa huku uongozi wa serikali na chama ukikaa kimya kana kwamba haujui ukweli wa mambo. 
Kimsingi, Edward Lowassa alimaanisha kuwa yeye ni mtu safi kwa sababu alitekeleza yale aliyoelekezwa kutekeleza na kwa hiyo, kujiuzulu kwake kamwe kusitafsriwe kama alama ya kukubali kuwa fisadi. Alikumbusha na kuonya kuwa ikiwa tuhuma tu zinatosha kumfukuza mtu kutoka kwenye chama, basi hata Rais Kikwete asingeweza kuwa Rais, ila kwa busara na hekima za Mzee Mkapa, Rais Kikwete sasa ni Rais pamoja na tuhuma zote alizorundikiwa wakati ule. Kimahesabu, Lowassa alisema ikiwa yeye ni mchafu, basi wote au wengi sana ndani ya CCM ni wachafu, vinginevyo yeye ni msafi.
Tunaambiwa ilibidi Rais Mkapa aingilie kati ili kuzuia Rais Kikwete asijibu tuhuma alizorushiwa na Lowassa na wala watu wasiruhusiwe kuendelea na mjadala huo ulioelekea kuchafua hali ya hewa ndani ya ukumbi. 
Hii ni kawaida sana katika falsafa ya utawala wa Kiafrika kwani tuhuma mbaya dhidi ya mtawala huwa haziruhusiwi kujibiwa ili kuepusha hatari ya watu wabishi kuja na ushahidi wa kuthibitisha tuhuma zao dhidi ya mtawala.
Swali la msingi tunalohitaji kujiuliza ni ikiwa Edward Lowassa anadai yeye ni msafi, na baadhi ya wajumbe wa NEC wanakubaliana naye, je ni nani ndani ya CCM ya sasa ni mchafu? Sina maana kuwa Edward Lowassa ndiye alikuwa mchafu peke yake na kwa kuwa sasa inadaiwa ni msafi, kwa hiyo wachafu hawapo! La hasha, hii si maana yangu.
Maana yangu haswa ni kuwa, Edward Lowassa tangu enzi ya hayati Baba wa Taifa, hajawahi kuwa na sifa ya usafi au uadilifu. Yeye ana sifa ya uchapakazi, uthubutu na ukarimu. Tangu enzi hizo na hasa baada ya kuzodolewa na Baba wa Taifa juu ya utajiri mkubwa usiokuwa na maelezo, Edward Lowassa aliingia katika mgogoro mwingine na Rais Benjamin Mkapa pale alipohamasisha Umoja wa Vijana (UVCCM) kugoma kumpigia kampeni baada ya kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM, mwaka 1995. 
Rais Mkapa alinyenyekea na kukubali masharti aliyopewa na ndipo vijana wakaingia katika kampeni. Hata hivyo, Mkapa aliamua kumwacha nje Edward Lowassa katika serikali yake ya kwanza hadi alipofuatwa na wazee miaka kadhaa baadaye na kumrejesha tena serikalini. Rais Mkapa alikiri baadaye kuwa alimrejesha serikalini kwa heshima ya wazee wale na wala si kwa uadilifu wake.
Edward Lowassa ana kipaji cha kuhamasisha na kutisha watawala wasiojiamini. Alifanya hivyo mwaka 2005 ili kumwingiza Jakaya Kikwete madarakani. Kama alivyodai mwenyewe wiki iliyopita mbele ya NEC, tuhuma nyingi zilimkabili Jakaya Kikwete na kutishia kuondoa jina lake katika kinyanganyiro cha urais.
Edward Lowassa kwa umahiri mkubwa, alikusanya vijana kutoka nchi nzima na kuwaleta Dodoma ili kuwatisha wazee kuwa Jakaya Kikwete asipoteuliwa, CCM ingesambaratika vibaya sana. Pamoja na jeuri yake na msimamo wake, Rais Mkapa aliogopa sana pale alipoitwa na wazee aliowakuta Dodoma na kuambiwa kuwa “chaguo ni Jakaya” vinginevyo Dodoma hapatatosha. 
Mkapa alinywea na kujikuta anaimba wimbo wa Jakaya huku Lowassa akiwa anachekelea kwa kejeli ya hali ya juu. Akiwa ni kamanda wa mtandao uliomwingiza Kikwete Ikulu, Lowassa kwa wema na ubaya, aliufahamu udhaifu wa Kikwete na kuufanya mtaji wa kumhujumu wakati wowote. Alichokifanya wiki iliyopita ni utangulizi wa makubwa yajayo.
Mbinu aliyoitumia Lowassa mwaka 2005 kumtisha Mkapa ili kumwachia Jakaya aingie bila mikwaruzo, ndiyo hiyo hiyo aliyoitumia ‘kummaliza’ Kikwete wiki iliyopita mjini Dodoma. Alikusanya makundi ya vijana kutoka sehemu mbalimbali na kuwaleta Dodoma huku akiwachochea kuwa umoja wao unafutwa; aliwakamata wazee kadhaa maarufu katika chama na kuwafadhili; akawakamata baadhi ya wenyeviti wa mikoa; akaigawa sekretariati ya CCM na kisha akawapata Wazanzibari wengi upande wake. 
Hii ilitosha kumtisha Kikwete mpaka akawatosa majemedari wake waaminifu akina Nape, Chiligati, Sitta, Membe, Makongoro Nyerere na Kinana. Tishio la kuenguliwa katika nafasi ya uenyekiti wa chama lilimfanya hata amtose katibu wake Mkuu, Wilson Mukama, ambaye ndiye mjenzi wa dhana ya kurejesha hadhi ya chama kwa kuwaondoa wanaokichafua.
Kama ilivyokuwa kwa Mkapa mwaka 2005 kwa watu kudhani amerogwa na nguvu za giza, ndivyo ilivyokuwa kwa Jakaya Kikwete wiki iliyopita ambaye watu wengi wa karibu naye wanaamini amerogwa na nguvu ya “TV Emmanuel” au nguvu ya aina fulani inayomfanya awe na kigugumizi kisicho cha kawaida. 
Waafrika ni wepesi wa kuamini ushirikina lakini kilichofanyika si kigeni katika siasa za makundi. Wanasiasa wajanja hutumia mbinu za kuwafitini wenzao kwa kuwatisha kuwa watatoa hadharani madhambi yao na kuwafanya wafyate mikia yao. Edward Lowassa anajua vema kutumia nafasi hii na anaelekea kufanikiwa. Pigo alilotoa kwa Kikwete wiki iliyopita linatishia kabisa kuua fikra zozote za kuibua tena dhana ya ufisadi katika nafasi na haiba ya Edward Lowassa.
Pigo hilo lilimfanya Kikwete akatae au asahau hata kuwapa nafasi ya kuongea wale aliokuwa amewapanga waongee ili kumtetea yeye binafsi au kummaliza Edward Lowassa. Baadhi ya marafiki zake wanaomboleza kwa kunyimwa nafasi ya kumsaidia baada ya Edward Lowassa kuwa amemrushia makombora mazito sana.
Mpaka hapa, bado swali linabaki, ikiwa Edward Lowassa amefanikiwa kujinasua katika tuhuma za ufisadi na kuwafanya washtaki wake wagwaye, ni nani basi anaweza kumzuia kuwa Rais ajaye kupitia CCM?
Je, wale waliokuwa msitari wa mbele kumtuhumu hadharani watafanya nini watakapotakiwa kupanda jukwaani kumnadi kama “tumaini la pili lililorejea”? Jambo moja ni wazi: Uongozi dhaifu waweza kuwafanya mamluki kuwa mashujaa na wahenga wa kizazi husika;

Source: Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment