Music

Saturday, April 11, 2015

Ndugu zangu jamaa zangu na marafiki zangu, tarehe kama ya leo miaka kadhaa iliyopita Mr & Mrs Mesaya walifanikiwa kumpata mtoto wa kwanza ambaye walimpa jina la Ismail Mesaya. Kama ishara ya upendo wangu kwako mama yangu mzazi, nakuandikia shairi hili ulisome popote pale na kwa nyakati zote utakapom-miss mwanao wa uzao wako wa kwanza…..

Mama wewe ni zawadi, ya maisha duniani,
Kwao wowote weledi, wewe unayo thamani,
Kwazo zako juhudi, nikaja ulimwenguni,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Kwa malezi yako bora, daima huna kifani,
Kwa zako tele busara, na mwongozo maishani,
Mama wewe ni kinara, nuru yangu maishani.
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mama faraja yangu, pindi niwapo shidani,
Hunipooza machungu, moyoni iwe amani,
Nakuombea kwa Mungu, heri tupu duniani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Daima hunipa nguvu, ninapodondoka chini,
Nipatapo maumivu, daima huwa pembeni,
Naupata uangavu, uniwekapo salani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mama u rafiki mwema, mwingine hapatikani,
Wajali pasi kupima, wajali bila rehani,
Mama nakupenda mama, kutoka mwangu moyoni,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Hakuna cha kukulipa, wala hakionekani,
Chochote nitachokupa, hakifikii thamani,
Sala naiweka hapa, akubariki Manani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Mola akujaalie, yalo mema duniani,
Baraka akujazie, akujazie pomoni,
Mabaya akwepushie, ukawe mwenye amani,
Mama wewe ni zawadi, kutoka kwake Muumba.

Imeandaliwa na kuandikwa:
Ismail Mesaya
12/04/2015

0 comments:

Post a Comment