Asalaam Aleikumu watanzania wote wenye imani ya Kiislamu. Tumsifu
Yesu Kristo kwa wale wenye imani ya Kikristo. Fuatana name kwenye makala yangu
hii kwa Mama Joyce Ndalichako (Waziri wa Elimu)
Mama Ndalichako Shikamoo. Natumaini wewe ni mzima bukheri wa afya
tele. Sisi huku Nadosoito hatujambo tuko na afya njema kimwili ila akili zetu
ziko nzito kutokana na wale watoto wetu Naropil, Namelok na wale wa mzee
Leshabar kushindwa kupata alama nzuri kwenye matokeo yao ya mitihani ya kidato
cha nne.
Mama Ndalichako, hali hii imenifanya nami nichukue kalamu na
karatasi niunde silabi kutoa maoni yangu juu ya suala hili kwani kadiri siku
zinavyozidi kwenda mbele hali inazidi kuwa mbaya.
Mama Ndalichako, nitachanganua baadhi ya mambo yanayochangia
mdororo huu wa elimu kwa kutumia kijiji changu cha Nadosoito kama eneo la
tafiti.
Mama Ndalichako, jambo kuu lililochangia mdororo huu huku kwetu ni kubadilika kwa muundo na mfumo wa elimu.
Mabadiliko haya hasa kwa upande wa shule ya msingi ndio umeleta matokeo haya
kwa elimu ya sekondari.
Mama Ndalichako, awali wakati mimi na kaka yangu tunasoma, tulianza
darasa la kwanza na la pili, Mwalimu Chacha
alikuwa anatufundisha 3K (Kusoma,
Kuandika na Kuhesabu). Si unamkumbuka yule mtoto wa Mzee Menyengera ambaye
alikuwa hajui kusoma na kuandika alirudia darasa la kwanza mara mbili hadi
alipojua kusoma na kuandika ndipo aliendelea na madarasa mengine??? Sasa hali
hii ilikuwa inafanya watoto wanaochaguliwa kuendelea na kila darasa awe ana
uwezo wa kukabili masomo ya darasa husika.
Mama Ndalichako, unakumbuka ule mtihani wa taifa wa darasa la nne
1999, lile darasa letu walifeli wanafunzi wangapi?? Unamkumbuka yule binti wa
Mzee Leng’ojine ambaye alianza darasa la kwanza mwaka 1992 lakini alihitimu
darasa la saba mwaka 2002? Nimekukumbusha scenario hizi mbili ukumbuke jinsi
ule mtihani wa darasa la nne ulivyokuwa unatumika kuwachuja watoto na kuruhusa
tu wale wenye uwezo kuendelea na darasa la tano.
Mama Ndalichako, sina shaka unakumbuka kipindi kile ukiwa Necta,
wastani wa alama za ufaulu kwa mtihani wa darasa la saba. Nakumbuka Mwalimu
Mondare alikuwa anatuasa na kutusisitiza sana kusoma ili tufanikiwe kupata
alama zile ambazo kwa wavulana ilikuwa alama 93/150 na wasichana ilikuwa ni
alama 90/150. Kipindi kile mtihani wa darasa la saba ulikuwa ni masomo matatu
(Maarifa, Lugha na Hisabati). Kila somo lilikuwa na alama 50 hivyo kufanya
masomo matatu kuwa na jumla ya alama 150.
Mama Ndalichako, unakumbuka kipindi hiko wale wanapata alama za juu
zaidi walikuwa wanachaguliwa kujiunga na shule za sekondari za vipaji kama
Ilboru, Mzumbe, Tabora boys, Msalato, Kibaha, Kilakala. Halaf wale ambao
wamekosa nafasi kujiunga na shule za serikali (ambao wengi wao walikuwa ni wale
wenye alama chini ya wastani wa kufaulu) ndio waliokuwa wanajiunga shule za
binafsi. Hii ndio ilikuwa sababu kwa shule za serikali kufanya vizuri zaidi
kuliko shule za binafsi hali ambayo iliwafanya wazazi wawe na imani sana kwenye
shule za serikali kuliko za binafsi hivyo kuwahasisha watoto wao kusoma kwa
bidii ili wachaguliwe kujiunga na shule za serikali.
Mama Ndalichako, nikurudishe tena kwenye kumbukumbuku zako za enzi
zile, pamoja na alama za ufaulu kuwa juu zaidi kwa darasa la saba, bado
kulikuwa na mtihani wa kidato cha pili ambao ulikuwa unawachuja wale wote wenye
wastani wa alama chini ya 36 (D). Hii imenikumbusha wale vijana 24 wa darasa
letu waliorudia kidato cha pili akiwepo yule kijana wa Mzee Lemutan.
Mama Ndalichako, mchujo huu wa kipindi kile ulikuwa na faida
zifuatazo:
1} Ulikuwa unawahamasisha sana wanafunzi kusoma kwa bidii kuepuka
aibu ya kurudia darasa
2} Ulikuwa unawaandaa wanafunzi kuwa watafutaji na wapambanaji
katika masomo yao ili kukwepa aibu ya kurudia darasa
3} Ulikuwa unaongeza chachu ya ushindani kati ya mwanafunzi na
mwanafunzi na kati ya shule na shule. Hii ilichangia sana kuongeza ufaulu na
vipaji kwa watoto
4} Ulikuwa umejenga imani kubwa sana kwa wazazi na jamii kwa ujumla
juu ya shule za serikali wakiamini kwamba wale wanaofaulu pekee ndio walipata
nafasi ya kujiunga na shule za serikali
Mama Ndalichako, hatua ulizochukua hizi karibuni, kwa mtizamo wangu
naona unaenda kujenga taifa lenye vijana wengi waliofika kidato cha nne wasio
na elimu wala taaluma ya kidato cha nne. Hatua hizi utadidimiza zaidi imani ya
jamii kwa shule za serikali lakini pia utafanya ufaulu uwe chini zaidi ya
ulivyo sasa. Mama natumai unaelewa kwamba, ili kujenga taifa imara ni lazima
tuwe na mfumo wa elimu ambao unawandaa vyema vijana kurithi tamaduni na desturi
za taifa kutoka kizazi kimoja na kurithisha kizazi kingine. Hiyo ndio dhima kuu
ya elimu ambayo ina lengo la kujenga na kuimarisha taifa kwa mustakabali wa
vizazi vijavyo.
Mama Ndalichako, nashauri yafuatayo yafanyike kama kweli tuna nia
ya kuboresha elimu yetu na kurudisha imani ya shule za serikali katika jamii. Pia
utakuwa ni mfumo ambao unawandaa vijana wabunifu na watafiti ili waweze kuwa
machampioni wa kulinda na kutumia rasilimali tulizonazo kwa maslahi ya jamii
yetu na taifa kwa ujumla.
11) Turejeshe mchujo kama
ulivyokuwa awali. Yaani mwanafunzi pekee atakayeruhusiwa kuendelea na darasa la
tatu ni yule tu anayejua 3K. Vivyo hivyo kwa darasa la nne na kidato cha pili
kuwe na mitihani ya mchujo.
22) Turejeshe alama zile za
ufaulu wa mwanafunzi wa darasa la saba kwenda kidato cha kwanza kuwa ni wastani
wa alama 31/50 kwa kila somo. Hapa nitatoa mchanganuo ninaopendekeza na faida
zake:
a)
Shule za secondary zigawanywe
katika makundi mawili. Moja, Shule za Sekondari zinazotoa elimu kama ilivyo
sasa. Pili shule za elimu ya ufundi.
b)
Alama za ufaulu ziwe: 31/50-50/50
wananfunzi hawa watajiunga na elimu ya secondary. Elimu hii inawajenga sana
wanafunzi katika usimamizi, uongozi wa rasilimali zetu. Alama zote chini ya
30/50 wanafunzi hao wagawanywe katika makundi kuendelea na elimu ya ufundi
kutegemea ufanisi wa kila mmoja. Elimu ya ufundi ni kama Kilimo, Ufugaji,
Uchimbaji madini, Uchongaji, Uselemala, Uwashi, Urinaji, Uvuvi nk.
c)
Wanafunzi wote watakaofaulu
kwenye mifumo yote miwili yaani wa technical na nontechnical watakutana Chuo
Kikuu kuchukua elimu ya juu zaidi kwenye taaluma yake. Utakuja kuona kwamba
wale watakaofeli elimu ya sekondari watarudi kuendelea na elimu ya ufundi na
wanaweza kurejea tena kusoma elimu ya Chuo Kikuu kwa mfumo huo wa elimu ya
ufundi.
d)
Taifa litakuwa na vijana
wengi wenye utaalamu wa fani mbalimbali, hivyo kuongezaka kwa ajira za
kujiajiri kwa vijana hawa kwani wana elimu ya ufundi.
e)
Wimbi la ukosefu wa ajira pia
utapungua kwa kiasi kikubwa kwani vijana wengi watakuwa wamejiajiri katika
sekta mbalimbali
f)
Itakuwa ni rahisi sana kwa
taasisi na wizara inayohusika na vijana kuwekeza kuboresha mitaji na shughuli
za vijana kwani wengi watakuwa na utaalamu Fulani
g)
Itarahisisha kufika Tanzania
ya Viwanda kwani tutakuwa na tabaka kubwa la vijana ambao wana utaalamu wa
vitendo na ujuzi wa rasimali zote tulizonazo.
13) Tuboreshe sana miundombinu ya
elimu kama kuwa na waalimu wenye uwezo na wito, kuwa naa mazingira sanifu kwa
walimu wetu, kumfanya mzazi awe mwalimu wa nidhamu ya mtoto pindi anaporejea
nyumbani.
44) Kila mmoja serikalini kuanzia
Rais hadi Balozi wa nyumba kumi, amheshimu Mwalimu na aheshimu utaratibu
uliowekwa na shule ilimradi tu hauvunji sheria za nchi. Nimeliongelea hili
kutokana na hali niliyoona juzi na imekuwa ikiendelea kila siku kwa watumishi
wa serikali. Hivi majuzi alitokea mkurugenzi wa halmashauri fulani,
alimsimamisha kazi Mwalimu mkuu na Mwalimu wa taaluma kutokana na kosa la
kuchangisha Sh.500 kwa kila mwanafunzi kwa ajili ya kuweka nembo ya shule
kwenye sare zao. Mbaya zaidi lililoniumiza ni Mkurugenzi huyo kugonga kengele
na kuwaita wanafunzi wote mstarini na kuwasisitiza kwamba hapana kuchangia chochote
na kuwatajia kwamba wale walimu ameshawafukuza kazi. Hali hii inatengeza dhana
ya watoto kuwadharau wanaowalea (Waalimu) na pia inawavunja moyo sana walimu
wetu. Nakumbuka hata mama na baba wakigombana ndani ya nyumba watoto tukiingia
wanatusalimia vyema na kuelekea chumbani kumaliza tofati zao ili watoto tusiige
hiyo tabia lakini pia heshima iendelee kudumu.
Mama
Ndalichako, nisikuchoshe kwa kuandika mengi ijapokuwa bado niko na mengi sana
ya kunena. Naamini ipo siku tutakutana, nitakuelezea zaidi na kwa kina juu ya
haya kwani naelewa toka enzi zile ukiwa Necta ulikuwa na nia ya dhati ya
kufanya elimu yetu iwe na tija na iheshimiwe na kila mmoja ndani na nje ya
nchi.
Mama
Ndalichako, nikutakiwe maisha mema na yenye fanaka. Nikutakie utendaji kazi
bora na Mungu aendelee kukupa hekima na busara ili uboreshe elimu yetu kwa
maslahi ya watoto wetu na vizazi vijavyo.
Ni mimi,
Mkulima
na mfugaji wa Kijiji cha Nadosoito
+255 756
688 090/+255 712 814 285
0 comments:
Post a Comment