An impressive
speech
Asalam aleykum/Bwana yesu asifiwe wanazuoni wenzangu
na wanaumajimui wote?
Awali ya yote nimshukuru mwenyezi Mungu kwa
kuniwezesha kujumuika nanyi kwa mara nyingine tena japo ni watu tofauti ili
dhima kuu bado ni ile ile.
Pili nimwage shukrani za dhati kwa wana-UDBS wa
2009-2012 kwa kutuunga mkono na kutusaidia kwa namna moja au nyingine.
Tatu nitoe shukrani zangu kwa wazazi wangu, ndugu,
jamaa na rafiki zangu ambao hawakuishiwa neno na wala hawakuchoka kunipa
mwongozo na shauri mbalimbali ili niweze kufanikisha malengo yangu.
Nne niwashukuru pia uongozi wa Chuo kikuu cha Dar es
Salaam kwa kukubali kukaa chini na kulijadili suala hili kwa mara nyingine na
kwa kina na hatimaye manufaa haya yakafikiwa ijapokuwa “the decision was final
and conclusive”
Na mwisho nitoe shukrani zangu za dhati kutoka moyoni
kwenu wote kwani najua wote mliguswa na hili jambo kwa namna tofauti. Wapo
ambao walitambua dhamani yetu na hawakusita kumwomba Mungu wao kwa namna
mbalimbali wajuavyo wao kwa lengo moja tu la sisi kuweza kujumuika nao kwa mara
nyingine kwenye tasnia hii ya elimu. “Mbarikiwe sana”
Wapo pia ambao walishusha pumzi zao na kumshukuru
maulana kwa namna tofauti wajuavyo wao baada ya kupata taarifa kwamba hatukuwa
tena sehemu ya umma wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Hawa walitoa dinari za
shukrani zao kwa Mwenyezi Mungu kwani watu ambao wamekuwa vizuizi na kukosoa
yale maovu wanayoyafanya, walikuwa wamechinjiwa baharini tayari. Nao pia
wabarikiwe sana
Baada ya salamu hizi nichukue nafasi hii kuwasihi
vijana wenzangu jambo moja muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Kuna usemi ambao umezoeleka sana masikioni kwa kila
mmoja wetu unaosema “KIJANA NI TAIFA LA KESHO”. Usemi huu
tumeuzoea na hata tunauunga mkono kwani hata wenye nyadhifa na nafasi
mbalimbali nao pia wameuridhia na kila kukicha na kuchwea wanatushawishi kuhusu
hili. Si kwamba nawalaumu kwa hili bali naamini tunautumia kwa kuwa tumeukuta
na vile vile hatukuwahi kuruhusu akili zetu kutafakari na kuchambua maana
halisi ya usemi huu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu na jamii zetu
kwa ujumla.
Kwa kifupi tunapozungumzia taifa la kesho
tunawazungumzia wataalamu, viongozi, wafanyakazi, wazazi, walezi, washikadau
mbalimbali na wajasiriamali wa baadae. Mkumbuke ya kuwa vitu vyote hivi
vinahitaji maandalizi ya leo ili kesho yaweze kufanikiwa. Kama mtakubaliana na
mimi katika hilo, basi hatuna budi kukataa kwa akili na nguvu zetu zote usemi
huu ambao kama vile una lengo la kubana uwezo wetu wa kufikiri.
Kwa ukweli na msimamo huo naweza kusema kuanzia sasa
usikubali kuitwa taifa la kesho ukiwa kama kijana bali tuwe na usemi mbadala
unaosema “KIJANA NI MAANDALIZI YA TAIFA LA KESHO”
Chukulia mfano leo hii tunalalamika maadui wakubwa wa
taifa letu, badala ya kupungua wanazidi kuongezeka. Nadhibitsha hilo kwa hali
halisi iliyopo sasa kwani awali tulikuwa na maadui watatu, yaani UMASIKINI,
UJINGA na MARADHI lakini kwasasa maadui hao wameota mizizi na kutoa mazao
mengine ya RUSHWA na UFISADI. Hii imefanya maadui hawa kuongezeka na kufikia
watano kwa idadi kwasasa. Sasa kwa nafasi uliyonayo sasa kama utasema wewe ni
taifa la kesho basi umeruhusu mind yako ku-relax kwenye hili. Lakini
tukijikubali kuwa sisi ni maandalizi ya taifa la kesho basi hatutakuwa na budi
kupambana na hili kuanzia sasa ili tutengeneze aina ya taifa tunalotaka kuishi.
Mwalimu J.K. Nyerere aliwahi kutanabaisha hili kwa
wasomi wa Afrika kwenye hotuba yake aliyoitoa kwenye Chuo cha Monrovia- Liberia
mwaka 1968, feb 29. Alisema, “……..Sisi
vijana bado katika Afrika tunaweza kwa kutumia ujuzi wetu, kuwasaidia wananchi
kuleta mapinduzi katika masiha yao yaliyo ya kimasikini sana. Lakini kama
tunataka kufikia sifa hiyo ya kufanya kazi nzuri na kuridhika, basi kuna kipimo
kimoja tu lazima tufikie. Sisi wenyewe ni lazima tuwe sehemu ya taifa hilo
tunalotaka kulibadili…..” Mwisho wa kumnukuu.
Vile vile dhana hii ya kusema kijana ni taifa la kesho
imeendelea kuwaathiri vijana wengi hadi leo kwani wengi wa vijana wenzangu
wanaona hawana la kufanya kwa ajili ya taifa lao kwa sasa kwani wao ni taifa la
kesho. Kwa hili hata waasisi wa taifa hili walilikemea tena kwa nguvu mno
wakijua ya kwamba vijana hawataweza kurithi tunu, mila na tamaduni za taifa lao
kama hawatafanya maandalizi ya kutosha pindi wawapo vijana. Niwakumbushe tena
nukuu ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa 3/07/1964 Ikulu kwenye maazimisho ya miaka
10 tangu kuanzishwa kwa TANU alipokuwa akizungumza na watoto na vijana.
Alisema, “…….Wajibu wenu ni kujifunza. Si
kwa kusoma vitabu tu maana yawezekana kujua mambo mengi lakini pia ukawa huna
manufaa kwa nchi yako na kwa wananchi wenzako. Kazi ya kujifunza, kujua mambo
na kutumia ujuzi huo ni lazima kutumiwa kwa ajili ya kazi za maendeleo ya nchi
na watu wake. Ni lazima kila mara ujiulize swali hili “Nifanye nini kumsaidia
mwananchi mwenzangu au nifanye nini kuisaidia nchi yangu? ……Tukumbuke mambo
haya yote hayangoji mpaka ati hapo mtakapofikia umri wa mtu mzima. Mnaweza sasa
kuanza kujifunza, na mnaweza sasa kuanza kuanza kusaidia kazi ya kujenga
nchi……” Mwisho wa nukuu.
Kwa hilo nami nawaasa sana vijana wenzangu tuachane na
dhana ya kwamba kijana ni taifa la kesho na kuanzia sasa tuanze kuandaa taifa
letu la kesho kwa kukemea na kunyooshea vidole yale yote ambayo yanakwamisha
ama yana lengo la kukwamisha maendeleo ya taifa letu na Afrika kwa ujumla.
Mwisho kabisa niwaage kwa kuwakumbusha maneno haya, “……..We now have no alternative but to
apply ourselves scientifically and objectively to the problem of our country.
We have to think, and then act on our thinking. We have to recognize the
poverty, the ignorance, the diseases, the corruption, the embezzlement of
public fund, the social attitudes and the political atmosphere which exist, and
in that context think about what we want to do and how can we move from the
existing situation towards one which we like better”.
Asanteni sana
Mungu ibariki UDSM, Mungu ibariki Tanzania, Mungu
ibariki Afrika
Imeandaliwa na kuandikiwa na
Mesaya Ismail
Mob: +255 756 688 090
well spoken suma
ReplyDeleteAsante kaka
Delete