Music

Monday, November 18, 2013

An impressive speech-Mesaya

An impressive speech
Asalam aleykum/Bwana yesu asifiwe wanazuoni wenzangu na wanaumajimui wote?
Awali ya yote nimshukuru mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kujumuika nanyi kwa mara nyingine tena japo ni watu tofauti ili dhima kuu bado ni ile ile.
Pili nimwage shukrani za dhati kwa wana-UDBS wa 2009-2012 kwa kutuunga mkono na kutusaidia kwa namna moja au nyingine.
Tatu nitoe shukrani zangu kwa wazazi wangu, ndugu, jamaa na rafiki zangu ambao hawakuishiwa neno na wala hawakuchoka kunipa mwongozo na shauri mbalimbali ili niweze kufanikisha malengo yangu.
Nne niwashukuru pia uongozi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa kukubali kukaa chini na kulijadili suala hili kwa mara nyingine na kwa kina na hatimaye manufaa haya yakafikiwa ijapokuwa “the decision was final and conclusive”
Na mwisho nitoe shukrani zangu za dhati kutoka moyoni kwenu wote kwani najua wote mliguswa na hili jambo kwa namna tofauti. Wapo ambao walitambua dhamani yetu na hawakusita kumwomba Mungu wao kwa namna mbalimbali wajuavyo wao kwa lengo moja tu la sisi kuweza kujumuika nao kwa mara nyingine kwenye tasnia hii ya elimu. “Mbarikiwe sana”
Wapo pia ambao walishusha pumzi zao na kumshukuru maulana kwa namna tofauti wajuavyo wao baada ya kupata taarifa kwamba hatukuwa tena sehemu ya umma wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Hawa walitoa dinari za shukrani zao kwa Mwenyezi Mungu kwani watu ambao wamekuwa vizuizi na kukosoa yale maovu wanayoyafanya, walikuwa wamechinjiwa baharini tayari. Nao pia wabarikiwe sana
Baada ya salamu hizi nichukue nafasi hii kuwasihi vijana wenzangu jambo moja muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Kuna usemi ambao umezoeleka sana masikioni kwa kila mmoja wetu unaosema “KIJANA NI TAIFA LA KESHO”. Usemi huu tumeuzoea na hata tunauunga mkono kwani hata wenye nyadhifa na nafasi mbalimbali nao pia wameuridhia na kila kukicha na kuchwea wanatushawishi kuhusu hili. Si kwamba nawalaumu kwa hili bali naamini tunautumia kwa kuwa tumeukuta na vile vile hatukuwahi kuruhusu akili zetu kutafakari na kuchambua maana halisi ya usemi huu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu na jamii zetu kwa ujumla.
Kwa kifupi tunapozungumzia taifa la kesho tunawazungumzia wataalamu, viongozi, wafanyakazi, wazazi, walezi, washikadau mbalimbali na wajasiriamali wa baadae. Mkumbuke ya kuwa vitu vyote hivi vinahitaji maandalizi ya leo ili kesho yaweze kufanikiwa. Kama mtakubaliana na mimi katika hilo, basi hatuna budi kukataa kwa akili na nguvu zetu zote usemi huu ambao kama vile una lengo la kubana uwezo wetu wa kufikiri.
Kwa ukweli na msimamo huo naweza kusema kuanzia sasa usikubali kuitwa taifa la kesho ukiwa kama kijana bali tuwe na usemi mbadala unaosema “KIJANA NI MAANDALIZI YA TAIFA LA KESHO”
Chukulia mfano leo hii tunalalamika maadui wakubwa wa taifa letu, badala ya kupungua wanazidi kuongezeka. Nadhibitsha hilo kwa hali halisi iliyopo sasa kwani awali tulikuwa na maadui watatu, yaani UMASIKINI, UJINGA na MARADHI lakini kwasasa maadui hao wameota mizizi na kutoa mazao mengine ya RUSHWA na UFISADI. Hii imefanya maadui hawa kuongezeka na kufikia watano kwa idadi kwasasa. Sasa kwa nafasi uliyonayo sasa kama utasema wewe ni taifa la kesho basi umeruhusu mind yako ku-relax kwenye hili. Lakini tukijikubali kuwa sisi ni maandalizi ya taifa la kesho basi hatutakuwa na budi kupambana na hili kuanzia sasa ili tutengeneze aina ya taifa tunalotaka kuishi.
Mwalimu J.K. Nyerere aliwahi kutanabaisha hili kwa wasomi wa Afrika kwenye hotuba yake aliyoitoa kwenye Chuo cha Monrovia- Liberia mwaka 1968, feb 29. Alisema, “……..Sisi vijana bado katika Afrika tunaweza kwa kutumia ujuzi wetu, kuwasaidia wananchi kuleta mapinduzi katika masiha yao yaliyo ya kimasikini sana. Lakini kama tunataka kufikia sifa hiyo ya kufanya kazi nzuri na kuridhika, basi kuna kipimo kimoja tu lazima tufikie. Sisi wenyewe ni lazima tuwe sehemu ya taifa hilo tunalotaka kulibadili…..” Mwisho wa kumnukuu.
Vile vile dhana hii ya kusema kijana ni taifa la kesho imeendelea kuwaathiri vijana wengi hadi leo kwani wengi wa vijana wenzangu wanaona hawana la kufanya kwa ajili ya taifa lao kwa sasa kwani wao ni taifa la kesho. Kwa hili hata waasisi wa taifa hili walilikemea tena kwa nguvu mno wakijua ya kwamba vijana hawataweza kurithi tunu, mila na tamaduni za taifa lao kama hawatafanya maandalizi ya kutosha pindi wawapo vijana. Niwakumbushe tena nukuu ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa 3/07/1964 Ikulu kwenye maazimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa TANU alipokuwa akizungumza na watoto na vijana. Alisema, “…….Wajibu wenu ni kujifunza. Si kwa kusoma vitabu tu maana yawezekana kujua mambo mengi lakini pia ukawa huna manufaa kwa nchi yako na kwa wananchi wenzako. Kazi ya kujifunza, kujua mambo na kutumia ujuzi huo ni lazima kutumiwa kwa ajili ya kazi za maendeleo ya nchi na watu wake. Ni lazima kila mara ujiulize swali hili “Nifanye nini kumsaidia mwananchi mwenzangu au nifanye nini kuisaidia nchi yangu? ……Tukumbuke mambo haya yote hayangoji mpaka ati hapo mtakapofikia umri wa mtu mzima. Mnaweza sasa kuanza kujifunza, na mnaweza sasa kuanza kuanza kusaidia kazi ya kujenga nchi……” Mwisho wa nukuu.
Kwa hilo nami nawaasa sana vijana wenzangu tuachane na dhana ya kwamba kijana ni taifa la kesho na kuanzia sasa tuanze kuandaa taifa letu la kesho kwa kukemea na kunyooshea vidole yale yote ambayo yanakwamisha ama yana lengo la kukwamisha maendeleo ya taifa letu na Afrika kwa ujumla.
Mwisho kabisa niwaage kwa kuwakumbusha maneno haya, “……..We now have no alternative but to apply ourselves scientifically and objectively to the problem of our country. We have to think, and then act on our thinking. We have to recognize the poverty, the ignorance, the diseases, the corruption, the embezzlement of public fund, the social attitudes and the political atmosphere which exist, and in that context think about what we want to do and how can we move from the existing situation towards one which we like better”.
Asanteni sana
Mungu ibariki UDSM, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
Imeandaliwa na kuandikiwa na
Mesaya Ismail
Mob: +255 756 688 090


2 comments: