
“PANYA ROAD” MSAMIATI MPYA JIJI LA DAR ES SALAAM
Ulikuwa mwanzoni kabisa mwa mwaka 2015, viunga kadhaa vya jiji la Dar es Saalam vilipokumbwa na kimbia kimbia na kupotea kwa amani ya raia wake kwa muda. Hali hii ilishtua na kutikisa sio tu jiji la Dar es Salaam bali nchi nzima. Taifa lilibaki masikio na vinywa wazi kutokana na kuibuka kwa kikundi hiki ambacho hakina tofauti na Boko Haram, Mungiki, Tamil Tigers, M23 n.k. Labda utofauti uliopo kati ya kikundi hiki chenye jina “Panya road” ni utofauti wa madhumuni, malengo na makusudi ya kuanzishwa.
Kimfumo na kwa namna kundi hili lilivyoibuka hapa Tanzania, hauna tofauti kabisa na namna makundi ya Tamil Tigers na SIS yalivyoanza ila tu ni maudhui anuwai ya makundi haya.
Tamil Tigers lilikuwa kundi la waasi huko Sri Lanka ambalo lilipigana kupinga serikali ilyokuwa madarakani na kusababisha kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe zilizodumu kwa zaidi ya miaka 30 kabla ya serikali kukubaliana nao na kumaliza mvutano wao mwaka 2010.
SIS lenye kirefu cha Syria Islamic State, nalo ni kundi la waasi lililoibuka huko Syria mwaka 2010/2011 kwa kupinga serikali ya Rais Al Hasad.
Kwa ujumla makusudi ya makundi haya kama nilivyoainisha, ni kuleta mapinduzi kutokana na kuchoshwa kwa utawala na serikali iliyopo madarakani.
Tunaweza kusema kwamba makundi yote haya yameanza kutokana na wananchi kuchoshwa na jambo fulani hivyo kutafuta njia mbadala za kukabiliana na hali hiyo.
Ripoti ya jeshi la Polisi baada ya kuchukua hatua kukabiliana na kundi hili lililoibuka jijini, linaonyesha kwamba idadi ya wanaounda kundi hili wamefikia zaidi 625. Ripoti iliendelea kutanabaisha kwamba wanaounda kundi hili wana umri usiozidi miaka 24.
Kuwepo kwa kundi hili si jambo ngeni kwani matukio ya uvamizi na unyang’anyi yameanza kutekelezwa na kundi hili kwenye miezi ya March mwaka jana. Kikundi hiki kinatumia silaha za kawaida, yaani nyembe, visu, panga na fimbo kutekeleza shughuli zao.
Swali ambalo kila mmoja wetu amebaki bila majibu ni, Je, Nani aliasisi kikundi hiki? Nani alipendekeza jina hili? Nini maana ya hili jina? Nini sifa za kujiunga na kundi hili? Je, kundi hili lipo mikoani ama ni jijini Dar es Salaam tu? Nani kiongozi wa kikundi hiki? Kama hawana viongozi, ni vipi wanatekeleza shughuli zao? Nini chanzo cha kuanzishwa kundi hili?
Nadhani msomaji wa makala hii utanisaidia kutoa majibu ya maswali haya kama litakuwepo mojawapo ambalo utakuwa na majibu sahihi ya kutusaidia.
Msingi wa makala yangu hii ya leo nimelenga kujenga kwenye chanzo cha kuibuka kwa kikundi cha “Panya Road”. Kimtazamo kikundi hiki kinaundwa na vijana ambao wamekosa fursa za ajira hapa nchini. Kiumri vijana hawa tunaweza kusema ndio wameihitimu masomo yao katika ngazi mbalimbali kulingana na umri wao.
Nasema watakuwa wamehitimu masomo, kwani kulingana na mfumo wetu wa elimu, mtoto anaanza elimu ya msingi akiwa na umri wa kati ya miaka 6 au 7. Ukiongeza miaka 7 ya elimu ya msingi, utapata miaka 12 au 13. Kama mtoto huyu atafanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari, basi atahitimu kidato cha nne akiwa na umri wa miaka 16 au 17. Zaidi kama ataendelea na kidato cha tano na sita, huku atahitimu akiwa na umri wa miaka 19 au 20. Kwa wale ambao watafanikiwa na kujiunga na elimu ya juu, muda wa kuhitimu shahada zao watakuwa na umri wa miaka 22 hadi 24.
Kulingana na ripoti ya jeshila polisi, umri wa vijana wanaounda kundi hili wana umri kati ya miaka 12 hadi 24. Kama nilivyoonyesha kwenye aya iliyopita, umri wa kuhitimu darasa la saba kwa watoto wa kitanzania ni miaka 12/13 na umri wa kuhitimu elimu ya juu ni miaka 24.
Ni nini basi namaanisha katika hili? Ni vyema watanzania wakafahamu kwamba, kundi hili ni matokeo ya mfumo mbovu wa elimu uliozaa vijana wengi wasio na ajira na ambao hawana mbinu zozote mbadala za kukabiliana na maisha nje ya ajira.
Kwa takwimu zilizopo, vyuo vikuu vyetu vinazalisha zaidi ya vijana 43,000 kila mwaka. Uwezo wa serikali na mashirika binafsi kuajiri ni vijana wasiozidi 7,000 kwa mwaka. Kwa hesabu ya haraka haraka tu ni kwamba vijana zaidi ya 35,000 wanaongezeka mtaani kwenye genge la vijana wasio na ajira. Hapa nimezungumzia tu wale wanaohitimu vyuo vikuu.
Kulingana na matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne, zaidi ya 90% wahitimu wanashindwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita kwa kukosa sifa (kufeli). Asilimia zaidi ya 30 ya wanaohitimu kidato cha sita nao wanaangukia kwenye kundi la kushindwa kujiunga na vyuo vikuu kwa sababu hiyo hiyo ya kukosa sifa. Hii inafanya idadi ya vijana wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu, ijapokuwa wana elimu ya kidato cha nne na/au sita kuwa ni zaidi ya 93%.
Pamoja na hao 7% wanaofanikiwa kuendelea na masomo ya vyuo vikuu, inasadikika kwamba 10% yao wanashindwa kufanikisha ndoto zao hizo kutokana na mfumo wetu wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Hivyo kufanya vijana wanaoendelea na elimu ya juu kuwa chini ya asilimia 7 ya vijana wenye elimu ya kidato cha nne na/au sita kila mwaka.
Kama tulivyoona uwezo wa serikali na makampuni na mashirika binafsi kuajiri, ni vijana 7,000 tu kati ya vijana 43,000 kila mwaka. Hii inamaanisha kwamba 16% ya vijana wanaohitimu elimu ya juu ndio wanapata fursa ya ajira. Kwa maana nyingine asilimia 84 wanarudi mtaani kuungana na wale 93% ambao hawakufanikiwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Hii ni sawa na kusema 95% ya vijana ama nguvu kazi ya taifa ambao wana elimu kuanzia kidato cha nne na kuendelea, kila mwaka wanaongezeka mtaani kwenye genge la vijana wasiokuwa na ajira.
Ni ukweli usiofichika kwamba, mfumo wetu wa elimu na uchumi na mfumo wetu wa utawala uliojawa na rushwa na ufisadi, ndio chachu hasa ya kuibuka kwa “Panya road”.
Tumekuwa na mfumo wa elimu ambao unazalisha vijana wasioendana na matakwa ya mfumo wa uchumi tulionao. Mfumo wetu wa elimu umekosa shabaha ya elimu kwa umma. Ni lazima shabaha ya elimu yetu itambue aina ya rasilimali tulizonazo na jamii tuliyonayo. Elimu ni lazima iwe ni ile inayowandaa vijana wetu kwa kazi watakayotakiwa kufanya katika jamii ya kitanzania huko vijijini ambako maendeleo yatategemea sana kazi na juhudi za wakulima. Kusema hivi sina maana ya kwamba elimu ya Tanzania ipangwe katika namna ya kufunza wakulima wa aina mbalimbali wasiojua kufikiri, wanaofuata tu kama kondoo mipango na amri zote za wakubwa. Lazima elimu izae wakulima bora, na vile vile iwaandae watu kushika madaraka wanayostahili wakiwa wakulima.elimu yetu haina budi iwaandae vijana wetu kutimiza wajibu wao katika kuendeleza vijiji vyao kuliko kulindikana mijini kutafuta kazi za kuajiriwa “White colours jobs”. Mipango ya elimu katika nchi yetu ya Tanzania haina budi kutilia mkazo juhudi ya pamoja siyo maendeleo ya mtu mmoja binafsi.
Nimejaribu kupitia katiba za baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini hasa zile zenye nguvu ili kuona ni kwa namna gani kila mmoja amejipanga kukabiliana na mfumo wetu wa elimu ambao unawaandaa vijana tegemezi wa ajira, lakini sijaona chama ambacho kimeonyesha nia ya kubadili mfumo huu.
Katiba ya chama tawala (CCM) ambayo inaenda kinyume kabisa na matendo ya uongozi wake, kwani inaamini kwamba ujamaa na kujitegemea ndio njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru. Pamoja na imani hiyo, viongozi waandamizi wa chama hiki mwaka 1985 walizika rasmi imani hii kwa Rais Mwinyi (Mwenyekiti wa CCM) kutamka bayana katika kilichoitwa Azimio la Zanzibar, (lililokuwa na lengo la kuzika Azimio la Arusha) kwamba”Likul ajalin kitaabun”, akiwa na maana kwamba kila zama na kitabu chake. Hivyo kupinga kabisa sera za ujamaa na kujitegemea. Kwenye elimu, Ibara ya 15(6) ya katiba ya CCM inatamka wazi kwamba kila mwanachama ana wajibu wa kujielimisha kwa kadiri ya uwezo wake, na kutumia elimu hiyo kwa faida ya wote. Nadhani kila mmoja ataona kwamba hakuna kipengele chochote kwenye katiba ya CCM yenye lengo la kutafuta mfumo sahihi wa elimu na wenye tija kwa nchi yetu.
Vivyo hivyo kwa katiba ya CHADEMA Ibara ya 4.3(2) inasema; Kuboresha na kutunza na kutoa huduma za jamii, kwa mfano, Afya, Elimu, Maji, Makazi na usalama wa raia, kwa ajili ya kukuza hali ya maisha ya watu. Nayo haijaweka bayana kama ina nia ya dhati ya kubadili mfumo wa elimu hii inayozalisha Panya road.
Nilitangulia kusema mfumo wetu bado haujawa na jibu la NINI DHIMA YA ELIMU. Hii namaanisha elimu ni lazima ilandane na aina ya rasilimali tulizonazo ili iwe kichocheo katika kukuza uchumi usio tegemezi. Namaanisha elimu ni lazima iwaandae vijana kupenda na kujua namna ya kutumia na kutunza rasilimali zao. Vile vile ni lazima iwatengeneze vijana kuwa mstari wa mbele kupingana na aina yoyote ya ubadhirifu na ufisadi wa rasilimali za umma.
Rasilimali zetu zipo kwenye kilimo, sanaa na ufundi, uvuvi, urinaji, ufugaji na utalii. Kwa mantiki hiyo, ni lazima tuwe na mfumo wa elimu wenye kujibu maswali ya namna gani tutakuza na kuendeleza uchumi wa nchi yetu kwa kutumia rasilimali hizi na vile vile namna ya kuhifadhi sekta zetu hizi kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.
Hivyo kutokana na rasilimali zetu hizi tulizonazo, mfumo wetu ungekuwa unawaandaa vijana kuzitumia rasilimali hizi kujikwamua kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mfumo wa elimu ambao naupendekeza ni ule ambao elimu ya msingi itakuwa ni darasa la kwanza hadi la nane. Elimu hii ya msingi iendeshwe kikanda chini ya mwongozo wa wizara ya elimu ili kuruhusu mtoto kujifunza kulingana na rasilimali zilizopo kwenye ukanda aliopo. Kwa mfano, mbali na masomo ya Maarifa ya jamii, Hisabati na Lugha, mwanafunzi apate masomo yanayoeleza namna ya kutumia, kuvuna na kutunza rasilimali zilizopo katika ukanda aliopo.
Kanda ya kusini watakuwa na masomo ya uvunaji wa makaa ya mawe, uvunaji wa gesi, kilimo cha korosho, mahindi na mpunga. Kanda za Pwani zitakuwa na masomo ya Uvuvi, sanaa na kilimo cha Nazi. Kanda ya Ziwa na Kaskazini vivyo hivyo watakuwa na masomo ya ya ufugaji, kilimo, uvunaji wa madini, utalii n.k. Utaratibu utakuwa hivyo pia kwa kanda zingine.
Baada ya kuhitimu darasa la nane, wale watakaofaulu kwa alama za juu zaidi, watajiunga na elimu ya sekondari. Huko watajifunza njia madhubuti za kusimamia rasilimali tulizonazo. Kwa wale watakaobaki, wataendelea na vyuo vya ufundi. Hapa watajifunza zaidi namna ya kuvuna na kutumia rasilimali zilizopo kwenye ukanda wao.
Kwa watakaopata alama za juu zaidi kwenye mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari, watajiunga na masomo ya vyuo vikuu. Huko watapata utaalamu wa nmna ya kuwekeza, kuendeleza rasilimali tulizonazo na kugundua rasilimali zingine zaidi. Hawa pia watajifunza zaidi masomo yanayohusu uhusiano wa kimataifa ili tupate wataalamu wa kutafuta masoko ya bidhaa zetu katika mataifa ya nje.
Wale watakaoshindwa kuendelea na elimu ya vyuo vikuu, wataandaliwa kuwa wakufunzi na waalimu kwa vijana wetu katika ngazi za chini za elimu. Hii itatusaidia kuwaandaa watu anuwai wa kuwaridhisha vizazi vijavyo dhima mahususi ya elimu yetu.
Ni imani yangu kuwa kwa kufanya hivi, tutajenga mfumo wa elimu ambao sio tegemezi na kujenga uchumi usio tegemezi na unaotokana na rasilimali tulizonazo kuliko kutegemea misaada na hisani.
Mwalimu Nyerere mwaka 1977 aliwahi kusema “Education is incomplete if it only enable man to work out eleborated scheme for universal peace but does not teach him how to provide good food for himself and his famility. It is equally incomplete and counter productive if it merely teaches man how to be an efficient tool user and tool maker, but neglet his personality and his relationship with his fellow human being”
Nimalizie kwa kusema, “Panya road” ni miongoni mwa mabomu ambayo Bwana Lowasa aliwahi kusema linakaribia kulipuka kutokana na udhaifu uliopo kwenye mfumo wetu wa elimu ambao unazalisha vijana na kuwaacha mtaani bila ajira. Nasema ni mfumo kwa kuwa, mfumo tulionao umeshindwa kutambua matakwa ya taifa na kutoa elimu inayoendana na aina ya rasilimali tulizonazo.
Imeandaliwa na kuandikwa na,
Jina: Mesaya Ismail
Phone : 0756 688 090/0712 814 285
Email: ismail.mesaya@gmail.com
Blog: fukununu.blogspot.com
Date: 16th January 2015
0 comments:
Post a Comment