Music

Sunday, January 4, 2015

BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA DIWANI KATA YA TERAT



BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA DIWANI KATA YA TERAT
MheshimiwaDiwani, nianze barua yangu hii kwa kukusalimu kama ilivyo ada na desturi yetu watu wa Afrika ambao tumelelewa na kukuzwa kwa maadili na miiko ya jamiii inayotuzunguka. Kwakuwa barua hii inawakilisha makundi mbalimbali ya watu kwenye jamii yetu, name nitoe salamu yangu kwakuzingatia makundi hayo yanayounda jamii yetu. Shikamoo Mheshimiwa Diwani, hii itasimama kuwakilisha makundi yote ya vijana wa kike na wa kiume pasipo kuzingatia mrengo wowote wa dini wala siasa. CCM oyeeee!!! Hapo natumai umenielewa nimewakilisha kundi lipi na mrengo upi. Peoples…..!!!!! Wengine najua watakusihi usiitike salamu hiyo kwasababu ni mrengo tofauti na wewe pasi na kusahau kwamba wewe ndio baba wa watu na vitu vyote vyenye mrengo na itikadi mbalimbali kwa kuzingatia ule msemo wa kibeberu unaosema “Minority rights and majority rule” Vile vile nisisahau wale wenye misimamo ya kiimani kwa kuwajumuisha kwa salamu ya Bwana Yesu asifiwe Mheshimiwa Diwani, na/au Asaalam aleikum warahman tulai Allah Wabarakatu!!!!

Mheshimiwa Diwani, Mimi ni kijana mzaliwa wa mtaa Nadosoito kusini niliyebahatika kupata elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu kwa busara, hekima na malezi mema ya watu wa Nadosoito. Hivyo kwa fadhila zao hizo, sina budi kujitwika mzigo wa kutoa sehemu ya maisha yangu kuwatumikia kwa namna yoyote ile kama njia ya kulipa fadhila zao kwangu.
Mheshimiwa Diwani, baada ya aya mbili za salamu na utambulisho, nikupongeze kwa kujitoa kuwa kiongozi wetu kwa zaidi ya miaka 20. Nakumbuka uliingia madarakani kwa mbwembwe na bashasha nyingi kutoka kwa wakazi wa Terat ukimtoa aliyekuwa Diwani wa wakati ule Mzee Lavuye. Hii inathibisha kwamba watu wa Terat walikupenda sana, na ulikuwa mtu sahihi kwao katika tasnia ya uongozi. Ulichukua kata yaTerat ikiwa na shule 3 za msingi, Zahanati 1, na isiyokuwa na shule hata moja ya sekondari wala barabara na miundombinu ya maji. Ni ukweli usiofichika pia kwamba, suala la elimu, afya, demokrasia, uchumi na maendeleo kwa watu wa Terat kwa wakati ule ulikua chini sana ukilinganisha na hali ya sasa.
Mheshimiwa Diwani, Kwa miaka 20 ya uongozi wako, kata ya Terat kwasasa ina shule 2 za sekondari, shule nne za msingi (za serikali), shule zaidi ya 3 zinazomilikiwa na watu binafsi, miundombinu ya maji, barabara zinazopitika, usafiri wa uhakika na ongezeko kubwa la vijana wasomi. Hii ndio tafasiri ya mafanikio kama alivyo tanabaisha mwanasiasa nguli wa Uingereza katika miaka ya 1990 Bwana John Major kwenye mkutano mkuu wa wafanyabiashara Jijini Leeds 28/1/1994 alipokuwa akihutubu juu ya changamoto zinazoikumbuka nchi ya Uingereza. Alisema “Success means: Investing in our infrastructures, investing in people and skills,……..”
Mheshimiwa Diwani, Barua hii ni mtiririko wa makala ambazo nimekuwa nikiziandika kama njia mojawapo za kufunza umma juu ya mambo fulani. Makala ya kwanza yenye mfumo wa barua niliandika mwezi mei mwaka 2012 kwa waziri mkuu wa nchi yetu nikimjulisha ukweli ulijificha juu ya wanafunzi waliofukuzwa vyuo vikuu. Bwana Pinda alinijibu barua yangu hiyo mwezi machi mwaka 2013 jambo ambalo lilinifanya niamini kwamba jumbe za namna hii huwa zinawafikia walengwa. Barua ya pili niliandika kwa Mheshimiwa Rais wetu mapema mwezi uliopita ni kumjuza juu ya hali ya sasa ya muungano na mustakabali wa baadaye.
Mheshimiwa Diwani, Utamaduni huu wa kufikisha ujumbe kwa namna ya barua haujaanza kwangu, kwani nadhani utakuwa unamkumbuka waziri mkuu wa kwanza wa Indra Bwana Jawaharalal Nehru alipokuwa gerezani kutokana na harakati za kisiasa za kumuunga mkono Bwana Mahatma Gandhi, alikuwa anatumia utaratibu huu kumwandikia mtoto wake Bwana Indra Gandhi juu ya hali halisi ya dunia [Glimpses of World History].
Mheshimiwa Diwani, Sasa nijikite kwenye lengo kuntu la barua hii kwako ambayo nadhani ni ya kwanza kuandikiwa. Sina maana kwamba hujawahi kupata barua zingine za mrengo na mantiki tofauti, hasha. Barua hii imelenga kukujuza baadhi ya mambo na kudai ufafanuzi juu ya mambo baadhi yenye utata.
Mheshimiwa Diwani, Mwaka jana Kata yetu ya Terat ilipokea kiasi cha TSH. 20,000,000/- kama gawiwo la mfuko wa jimbo. Kiasi hicho kililenga kumalizia majengo na miundo mbinu ya Shule ya Sekondari ya Mkonoo. Katika kile ambayo naamini unakijua wewe na kamati ya maendeleo ya kata, kiasi kile hakikutumiwa na kilikaa kwenye akaunti ya kata kwa zaidi ya miezi mitatu. Baadaye kiasi kile kilirudishwa kana kwamba hatukuwa na uhitaji nayo. Mmoja wa wajumbe wako wa kamati ya maendeleo ya kata alinithibitishia kwamba ulilazimisha kiasi kile kirudi kutokana na kutofautiana kisiasa na mbunge wa Arusha mjini. Inamaana Mheshimiwa unafanya kazi kwa maslahi ya chama chako au kwa maslahi ya umma?? Mheshimiwa huo ni kwa kufanya hivyo unanyima kata ya Terat fursa za kimaendeleo kwa kutanguliza misimamo ya kisiasa badala ya uhitaji wa wananchi wako??
Mheshimiwa Diwani, CCM na UKAWA ni watoto wa baba mmoja kama walivyokuwa Isaka na Ishumael. Wote wanajenga nyumba moja, wote wamezaliwa na baba mmoja na wote wana lengo moja tu na kuendeleza uzao wao. Vivyo hivyo kwa vyama hivi vya siasa. Utofauti pekee ninaouona ni namna watu hawa wawili wanavyotaka kutimiza ndoto zao. Kwa mtizamo huo sitaki kuamini kwamba kuna haja ya kukwamisha harakati za maendeleo kwenye “Boma” lako kwasababu tu ya utofauti wa kisiasa.
Mheshimiwa Diwani, Nadhani utakuwa unamkumbuka yule mwanamke waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa India miaka ya 1966-1977, 1980-1984, Mrs. Indira Gandhi, alipoalikwa kutoa muhadhara kwa wanazuoni wa Chuo Kikuu Cha Delhi, April 1, 1980. Alisema “I do not wish to make this a ritual of giving advice to new graduates. Advice is a commodity for which there are more sellers than buyers….” Nami nimuunge mkono kwa kauli hiyo hiyo kwamba sina nia ya kutumia barua hii kutoa ushauri kwako kwasababu zile zile alizotoa mwanamama huyu. Nia thabiti ya kutoa hili ni ile ile ya siku zote ya kutoa elimu kwa umma kuhusu mambo yanayotendeka wasiyoyajua.
Mheshimiwa Diwani, Kwa leo nihitimu hapa nikiwa na uhakika kwamba ujumbe huu utakufikia na vile vile ikikupendeza waweza kunijibu kwa kutumia mawasiliano yangu niliyoyaweka mwishoni mwa makala hii.
Ni wako katika ujenzi wa taifa
Ismail Mesaya
Phone: 0756 688 090/0712 814 285
Blog: fukununu.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment