Shairi naliandika, Natumai mko poa
Izraili amefika, Roho yangu kuitoa
Mwito kifo naitika, Meshindwa kujiokoa
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Ni miezi na masiku, Nami nimevumilia
Nakumbuka ile siku, Nilipo waingilia
Tena mida ya usiku, Nyote mkasubiria
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Saa zenu kwa pamoja, Mlifwata akrabu
Kwa sekunde mojamoja, Mkaweza kuhesabu
Nne tatu mbili moja, Mkanambia karibu
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Hoye! mkafurahia, Kwa shangwe mkanilaki
Tena mkashangilia, Mukawasha mafataki
Kwa masoda na mabia, Hakuna kilichobaki
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Awali mlinipenda, Na mkanigombania
Mkatundika kalenda, Kutani kuning’inia
Kuzikumbuka ajenda, Kukicha kutazamia
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Tumekuwa marafiki, Wa kufa na kuzikana
Tulogawana riziki, Wala hatukunyimana
Hasa wakati wa dhiki, Daima tulifaana
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Vipi leo mwachukia, Kunilani kwa matusi
Tangu nilipoingia, Ni mafua na virusi
Mwatamani nifukia, Mpate ondoa nuksi
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Serikali zalalama, Mgeni mie sifai
Uchumi umeshazama, Benki zinawadai
Bidhaa zote gharama, Mpaka mumenikinai
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Kila siku mwanisema, Siwatoki midomoni
Awamu yangu si njema, Mwanisuta vigogoni
Mwatamani kunitema, Nimewafika kooni
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Nimeshazua vituko, Kuharibu usalama
Mvua ya mafuriko, Jijini Dar-es-salama
Ardhi mitikisiko, Nyumba zote zikazama
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Kenya moto ukazuka, Afrika mashariki
Mabomba kuyazunguka, Watu wengi kufariki
Majumba yakaanguka, Kwa wenzetu Uturuki
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Si sahau Zanzibari, Kule pwani kisiwani
Kulotokea hatari, Feri kukosa ramani
Kuzama kwenye bahari, Kwa kweli ni kisirani
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Uchumi meharibika, Kwa siasa ziso safi
Libya imevurugika, Kumpoteza Gadhafi
Ikawa ni patashika, Kwa dhuluma na ulafi
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Na Somalia usiseme, Ilikuwa ni balaa
Kulipigwa na ukame, Watu wakalia njaa
Mnataka mnizime, Kwa kukosa manufaa
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Namaliza msafara, Nilikuwa tu mgeni
Mliopata madhara, Mtapata afueni
Mliokula hasara, Nasema tena poleni
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Nyote mloathiriwa, Mola awape baraka
Ombeni kujaaliwa, kheri nyingi kila mwaka
Muzidi kunyunyiziwa, Neema ziso mipaka
Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
Hivi sasa nawatoka, Bora tu niwaacheni
Kuwa nanyi nimechoka, Kwaheri nawaageni
Sina budi kuchomoka, Yupo mwengine mgeni
Hata hivyo yote tisa, Kumi roho yanitoka
@Comrade Ole Mesaya
0 comments:
Post a Comment