Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Nianze waraka wangu huu kwa kutanguliza salamu
zangu za dhati kwako. Kwa taratibu za mila na desturi za kimasai, napaswa nikusalimie
kama baba yangu kwa kusema “Airoroki papa”. Tukirudi kwa lugha yetu mama ya taifa
napaswa nikusalimu kwa kusema “Shikamoo baba”. Vile vile kwa kuwa una
wawakilisha watanzania wanaoamini kwa Imani za dini mbalimbali, nisiwanyime nao
ladha ya salamu zangu kwako. Nianze kwa salamu za kikristu ambapo napaswa niseme
“Bwana Yesu asifiwe Mheshimiwa Rais”. Nikisema pia “Asalam Aleikum Warahman tulahi
Allah wabarakatu” nafikiri utanielewa nawakilisha kundi lipi.
Mheshimiwa Rais, ama baada
ya aya nzima ya salamu zangu kwako, nikupe pole sana kwa maradhi yaliyokupata hivi
majuzi na kupelekea mwili wako kufanyiwa upasuaji. Pole sana kwa hilo na Mwenyezi
Mungu mwingi warehema muumba wa mbingu na dunia akujalie kheri upone haraka na urudi
katika hali yako ya kawaida kiafya ili uendelee kuwatumikia watanzania.
Mheshimiwa Rais, mimi ni
kijana wa kimasai niliyebahatika kupata elimu hadi ya chuo kikuu kwa kutegemea ufugaji
wetu ule ule wa kuhama hama kutafuta malisho ya mifugo na maji. Aina ya uchumi wetu
huu umetusaidia tulio wengi kupata fursa za kusoma ijapokuwa kwasasa tumedhamiria
kuwarudisha watu wa jamii hii katika lindi la umasikini tororo kwa kuona umuhimu
wa mwekezaji kwenye ardhi yao na kuyapa kisogo matunda wanayoyapata kwa aina hii
ya uchumi wanaoendesha kwenye ardhi yao.
Mheshimiwa Rais,
nadhani umezunguka na kupita kila kona ya nchi hii. Nadiriki kusema kila hatua uliyopiga
ndani ya viunga vya nchi hii, hujawahi kumkuta ama kumwona mtanzania mwenye asili
ya umasai ambaye amekaa barabarani akisubiri wapiti njia wamtupie japo chochote
kitu ili afanikishe kusonga mbele kwa maisha yake. Bali umekutana na wamasai ambao
wamekuwa mstari wa mbele wakichakarika huku na kule ama kwa kuwalinda watanzania
wengine ili apate ndarama za kuendeshea maisha yake, ama kwa kusokota na kusuka
nywele za dada zetu ili tu mdomo uende kinywani, ama wakizunguku kila kona kutoa
huduma za kuponya afya za watanzania kwa kuuza dawa za asili ili mradi tu kuitwe
jioni na hatimaye kesho, ama wakisafiri huku na kule na mikokoteni yenye madumu
ya maji wakihakikisha kwamba watanzania wote wanapata huduma ya maji kwa malipo
yatakayowawezesha kupata mkate wa kila siku. Hiyo ndiyo asili ya mmasai, kamwe haishi
kutafuta ili mkono uende kinywani na kamwe hawezi kuwa ombaomba.
Mheshimiwa Rais, Lengo langu
kubwa leo si kukupa sifa za kabila hili la wa masai bali nimejaribu tu kukuonyesha
ni athari gani tutapata jamii ya wamasai kama sera hii ya taifa itaendelea ya kutunyang’anya
ardhi yetu tuliyopewa na Maulana na kumpa mwarabu ama mzungu kwa kisingizio cha
uwekezaji.
Mheshimiwa Rais,
Nisikuchoshe sana kwa utangulizi mrefu ambao sio lengo kuntu la barua yangu hii
kwako. Lengo hasa la Makala hii kwako, ni kufikisha mawazo yangu kama mtanzania
wa daraja la mwisho kabisa kwako ambaye sidhani kama ipo hata siku moja nikapata
nafasi japo hata ya kukusalimu shikamoo na ukaitikia marahaba.
Mheshimiwa Rais, Mawazo
yangu haya ya leo yanaweza yakawa yamezungumzwa na watanzania walio wengi wenye
nafasi mbalimbali ndani ya nchi hii ila sidhani kama walizungumza kwa namna hii
ambayo mimi leo nimeamua kuwasilisha kwako. Nimekuwa na desturi ya kuandika
Makala za kila namna kwa umma kama njia niliyojiwekea kuwalipa fadhila watanzania
wenzangu wa Vijiji vya Nadosoito na Mkonoo ambao naamini nimepata elimu na makuzi
yaliyo bora kwa busara, hekima na malezi yao.
Mheshimiwa Rais, Kama
mtiririko na muendelezo wa karia yangu ya uandishi wa Makala, leo nimeona niwasilishe
Makala yangu kwako kwa namna ya barua kama alivyokuwa anafanya mwanamapinduzi wa
India Nerhu kwa kijana wake Indra Ghandhi (Glimpses of the World history)
Mheshimiwa Rais, Makala
yangu hii ya leo inahusu mustakabali wa muungano wetu kwa vizazi vijavyo.
Naamini utavutiwa sana kuona uwepo wa vijana wachache ndani ya taifa hili ambao
wanawaza juu ya mustakabali wa nchi hii na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Rais, Nianze
kwa kukumbusha japo kidogo juu ya sababu za Tume ya Jaji Nyalali kupendekeza uwepo
wa serikali ya Tanganyika. Sina maana kwamba hujui, wala sina maana kwamba umesahau,
bali nataka nitengeneze msingi wa hoja yangu ya mustakabali ya muungano wetu kwa
vizazi vijavyo.
i.
Kutambua usawa wa nchi mbili ambazo zimejiunga
katika Muungano uliozaa Tanzania. Tume ilizingatia hali ya sasa ambapo nchi moja
kati ya zile zilizoungana, inatambuliwa wakati nchi nyingine imefutika katika utambulisho
wa serikali ya Muungano.
ii.
Kwa kuipa Tanganyika serikali yake,
unaondoa ile hofu ambayo imeelezwa mara kwa mara kwamba Zanzibar itamezwa na
Tanganyika, hasa kwa kutambua ukweli kwamba masuala ya Tanganyika na yale ya Muungano
yanashughulikiwa pamoja, jambo ambalo linawapa watendaji wa serikali ya muungano
fursa ya kuingilia mambo ya Zanzibar bila sababu.
iii.
Kuondoa hisia za watu wa Tanganyika
kwamba wananyonywa na wazanzibari katika kuchangia gharama za uendeshaji na katika
kugawana madaraka, hasa kwa kuzingatia hali ya sasa ambapo nafasi za Tanganyika
ziko wazi kwa Wazanzibari wakati za Wazanzibari haziguswi na Mtanganyika.
iv.
Kuondoa hali isiyoeleweka na isiyoingia akilini,
ya kuwa na Muungano ambao unabaki ni kitendawili daima. Nchi mbili zinajiunga halafu
moja inakuwa na serikali yake lakini ya pili serikali yake inaipata mumo humo ndani
ya Muungano
Mheshimiwa Rais, Kung’ang’ania
kusema kwamba Tanzania lazima itakufa kama serikali ya
Tanganyika ikundwa ni jambo ambalo haliishi kushangaza walio wengi. Kwanza
tunasahau kwamba ili kuunda Tanzania ilibidi kwanza iwepo Tanganyika. Kama
kuwepo kwa Tanganyika 1964 hakukuzuia Tanzania kuzaliwa, kwanini leo kuwapo kwa
Tanganyika LAZIMA kupelekea kufa kwa Tanzania? Hii ni mantiki ya wapi?
Mheshimiwa Rais, Kwa
kuwa hoja ya msingi inayosimamiwa na wabunge wa CCM katika kupinga serikali
tatu ni idadi ya watu ya watu waliotoa mapendekezo hayo kuwa walikuwa wachache,
kwanini usifunguliwe mjadala utakaoongozwa na hasasi mbalimbali za kiraia juu
ya hili ili ukweli upatikane?
Mheshimiwa Rais, Kama
tunavyosema mwamba ngozi haishi kuvutia upande wake, chukulia mfano kukatokea
ubishi kati ya serikali ya Zanzibar na ile ya Tanzania na ikabidi timu mbili
zikutane kupata suluhisho, na upande mmoja ukiwakilishwa na wazanzibari watupu
na upande mwingine ukawakilishwa na nusu wazanzibari na nusu watanganyika, huo
utakuwa mjadala wa aina gani?
Mheshimiwa Rais, Kwa
hakika, huu ni muundo ambao kudumu kwake kunategemea kutokuwepo na migongano
ambayo inahitaji mjadala wa pande mbili, kila upande ukisisitize maslahi yake,
jambo ambalo ni upuuzi kuliamini katika dunia hii ya nipe nikupe.
Mheshimiwa Rais, Aina
hii ya Muungano wa serikali mbili uliyopendekezwa na “Bunge maalumu la Katiba
la CCM” kwenye katiba pendekezwa ni bomu na manowari za kuuwa Muungano huku
tukiimba wimbo wa “Tudumishe Muungano”
Mheshimiwa Rais, Rai
yangu katika hili ni kwamba iwapo tunataka kudumisha Muungano, hatuna budi
tuchague moja, ama tunaunda Muungano wa serikali moja ama tunaunda Muungano wa
serikali tatu.
Mheshimiwa Rais, Ili
kuendelea kuwa na Muungano ulio imara na unaokubalika na wananchi wa pande
zote:
a)
Hatuna budi kutambua kwamba wananchi
hawawezi wakaupenda Muungano kwasababu tu viongozi wa pande mbili wanaalikana,
hawa kwenda kule na wale kuja huku, wakastarehe na kufurahi basi. Ni lazima
kuhakikisha kwamba wananchi wa kawaida wananufaika kutokana na manufaa
yanayotokana na Muungano.
b)
Hatuna budi kuachana na dhana potofu za
kudhani kwamba Muungano uliopo ndio huo huo na wala hauruhusiwi kufanyiwa
marekebisho
c)
Viongozi na wananchi wanaowaongoza
hawana budi kujenga utamaduni wa kujadili waziwazi matatizo yao badala ya
kujiingiza katika manung’uniko ya chini chini, ambayo ni dalili ya unafiki na
chanzo cha vurugu katika nchi. Kama uwazi na ukweli havitathaminiwa, kuvumiliwa
na kuheshimiwa, matokeo yake yatakuwa ni chuki dhidi ya Muungano na dhidi ya
viongozi na pia Tanganyika dhidi ya Zanzibar na Zanzibar dhidi ya Tanganyika.
d)
Hatuna budi kuamini pia kwamba, jambo
lingine linaloweza kuamsha hisia za chuki lile la upande mmoja kuona kwamba
upande mwingine unaingilia mambo yake ya ndani huku hauna uwezo wala haki ya
kuingilia mambo ya ndani ya upande ule mwingine.
e)
Hatuna budi kuelewa kwamba hali ilivyo
sasa wabunge wa Zanzibar wa kuchaguliwa wapo watano (5) Kwenye bunge la Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania. Maana yake kila mbunge anawakilisha wananchi wapatao
laki mbili na sitini (260,000) wakati baadhi ya wabunge wa bara wanawakilisha
wananchi zaidi ya laki tatu na thelathini (330,000). Pamoja na kuwepo kwa idadi
hii ya wabunge watano kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, bado Zanzibar ina Baraza la wawakilishi ambalo lipo kwa ajili ya
kutunga sheria zinazohusu Zanzibar pekee. Ilihali hawa wa Tanganyika wapo
kutunga sheria za Tanganyika na Zanzibar kwa wakati mmoja kwani Bunge la
Tanzania ndio hili hilo Bunge la Jamhuri. Ili kulinda muungano hatuna budi
kutafuta na kuweka utaratibu ili wabunge wa Zanzibar wawe na idadi inayowiana
na wingi wa wananchi wanaowawakilisha.
f)
Ni lazima tutambue kwamba kuendelea na
mtindo uliopo sasa, ni kuwanyima baadhi ya wananchi haki ya kuwa na uwakilishi
unaofanana na mazingira yao. Kama haifai kuwa na serikali ya Tanganyika ambayo
maana yake inakuwa na Bunge au Baraza la Tanganyika, itabidi tutafute njia
nyingine ya kuhakikisha kwamba uwakilishi wa walio wengi haufutwi kwa nguvu ya
wachache. Ninachosema ni kwamba, kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania mabadiliko ya kikatiba hayawezi kupitishwa bungeni ila tu kwa kupata
theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar. Hii ina maana iwapo wabunge wa Zanzibar
hawataki jambo lipite, wanaweza kuliua kwa kukubaliana miongoni mwao, hata kama
jambo lenyewe ni kipengele kinachohusu bara katika katiba.
g)
Ni lazima yawepo mabaraza matatu, moja
la Zanzibar, moja la Tanganyika na moja la Muungano. Katika Baraza la Muungano
ambalo litakuwa kama Seneti, uwakilishi uwe sawa sawa kwa bara na visiwani, kwa
kutambua usawa wa dola mbili zilizoungana. Yale mabaraza mengine mawili yafanye
kazi kwa uhuru unaotambuliwa na katiba na yakubali kuelekezwa na Baraza la
Muungano. La sivyo, kama serikali ya Tanganyika ni haramu kwa hiyo baraza lake
pia ni haramu, tukubali kutekeleza mantiki ya uwiano wa wingi wa watu.
Tanganyika ambayo ina watu wapatao milioni 43 iwe na wabunge 300 na Zanzibar
yenye watu milioni 1.3 iwe na wabunge 5
Mheshimiwa Rais,
nisikuchoshe sana kwa siku ya leo ila uapatapo barua yangu hii aitha moja kwa
moja ama kupitia kwa vyombo vyako vya usalama, tafadhali legeza moyo wako na
tafakari juu ya mustakabali wa Muungano wetu kwa vizazi vijavyo ili lisijebaki
kama historia kama ilivyokuwa kwa Muungano wa Nchi za Kisoviet.
Mheshimiwa Rais,
Nashukuru sana kwa kunipa muda wako kwa kupitia maandiko haya ya kijana wa
kitanzania mwenye ndoto za kuvunjika kwa Muungano kama tutaendelea na mfumo huu
wa serikali mbili. Mwisho kabisa nimalizie na usemi wetu wa Kimasai unaosema “Tanzania
tamelono nimunyanu kanaa naishi oo kule”
Asante
Ni mimi wako katika
harakati za ukombozi wa fikra,
Ole Mesaya
0 comments:
Post a Comment