UDSM
INAELEKEA WAPI???
Nawasalimu wote kwa
salamu ya kikamaradi ambayo huamkiwa kwa fanani kusema; “Mbiu ya mnyonge” na
hadhira kuitikia: “Ni kalamu”…!!!!!!!!!!!
Natumai wote hamjambo
na mnaendelea vyema na maandalizi ya sikukuu za krisimasi na mwisho wa mwaka.
Kama mada
inavyojitutumua kwa kichwa cha habari hapo juu, leo nimelenga kueleza hisia
zangu kutokana na kile kinachoendelea ndani ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
ambayo naamini kinafanywa na utawala wa taasisi hiyo kubwa ya elimu chini ya “Prof”
Mkandala.
Mwezi wa pili mwaka
huu, niliandika makala ya kurasa nne niliyoipa jina la “Chuo Kikuu kimegeuga Choo Kikuu”.
Makala hii ilijikita kutanabaisha hali ilivyo ndani ya Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaam hasa katika uongozi na uhuru wa kuhoji, kutoa habari na maoni kwa
vijana wasomi wa kitovu hiki cha elimu. Baada ya makala hiyo kutoka, wengi
wanisifia kwa uthubutu wangu wa kuendelea na harakati za “kalamu” pamoja na
maswaiba yaliyonipata. Wengine walinikebehi na kunikejeli kwa kusema nafanya
hayo kisiasa na eneo hili si kwa ajili ya saisa bali ni kuongeza na kukuza
maarifa ya vijana. Nami niliwajibu kwa kuwakumbusha maneno aliyowahi kuyatoa
Mwalimu Nyerere akiwahutubiwa vijana ikulu mwaka 1964. Mwalimu alisema na
namnukuu “…..Wajibu wenu ni kusoma. Lakini si kwa kusoma vitabu tu kwani mwaweza
kusoma vitabu vingi bila kuwa na manufaa kwa jamii yenu. Hivyo msome huku
mkisaidia jamii zenu kwani hapo ndipo tutakapoona manufaa ya elimu kwenu….”
Mwanzoni mwa mwezi huu
niliendelea kutoa elimu kwa umma juu ya kile kilichopo ndani ya ya taasisi
kubwa ya elimu hapa nchini yaani Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Makala hizi
mbili nilizipa majina ya “Usiyoyajua kuhusu Chuo Kikuu Cha Dar es
Salaam part 1 & 2”. Makala hii ilijikita kuweka bayana hali halisi
iliyopo ndani ya taasisi hii katika sekta muhimu za kiafya na malazi. Kama ilivyokuwa
kwa makala ya awali, pia makala hizi mbili zilipokelewa kwa mitazamo tofauti na
wadau mbalimbali kwa wengine kusifia na wengine kukosoa.
Hali imezidi kuwa mbaya
sana kwa taasisi hii ya elimu kwani uhuru wa kutoa mawazo na uhuru wa serikali
ya wanafunzi kujitawala umezidi kubanwa na kuendeshwa kwa maslahi ya watawala.
Hivi majuzi Rais wa
serikali ya wanafunzi DARUSO, Bwana Nickson Filbert alikiuka katiba ya DARUSO
kwa kufanya mambo mengi chini ya utaratibu wa kikatiba. Kwa kuwa wanafunzi wa
kawaida hawaruhusiwi kuhoji masuala kama haya, wawakilishi wao yaani wabunge
waliliona hili na kuishtaki Rais huyo kwenye chombo cha maamuzi ambayo hutumika
kama mahakama hapo chuoni ambayo hujulikana kama DARUSO BOARD. Chombo hiki kipo
kikatiba kwa mujibu wa katiba ya DARUSO na imeundwa na wenyeviti wa Collages,
Schools na Institutes. Chombo hiki kina jukumu la kuhakikisha kwamba serikali
inatawala kwa mujibu wa sheria na kwa kufuata katiba.
Kama ilivyo ada kwa
shitaka lolote likifikishwa mahakamani, mshitakiwa hana budi kutoa utetezi wake
kwa kujibu hoja. Vivyo hivyo kwa serikali ya DARUSO ilimtumia “Attorney General”
wake ambaye anajulika kwa cheo cha Chief Protocal, kuiwakilisha serikali katika
kutoa utetezi wa kesi inayoikabili. Chombo hiki kilisikiliza utetezi wa
serikali na hatimaye kufikia maamuzi kwa kutoa hukumu kwamba serikali imekiuka
katiba. Kosa la ukiukwaji wa katiba unafanya serikali kufika ukomo kwa Rais
kuvuliwa madaraka yake na baraza la mawaziri kuvunjwa. Hii ni kwa mujibu wa
katiba ya DARUSO.
Baada ya DARUSO BOARD
kutoa uamuzi huu, inabidi bunge kukaa na kulipisha hilo ikiwa ni pamoja na
kupata baraka za ofisi ya mshauri wa wanafunzi. Hili ni suala la kiutawala kwa
serikali ya wanafunzi na ambao hauna mahusiano na utawala wa Chuo ikiwa tu
umefanywa kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria.
Pamoja na suala hili
kufuata taratibu zote kisheria, utawala wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam umejiingiza
kwenye sakata hili kwa KUWASIMAMISHA MASOMO kwa muda usiojulikana viongozi sita
wa DARUSO BOARD na wabunge waliopeleka hoja hii kwenye chombo hiki cha uamuzi.
Nimesikitishwa sana na
hali hii inayofanywa na Bwana Mkandala, Luoga na Mfinanga huku wakijua fika
kwamba wanadumaza demokrasia ndani ya taasisi hii na kujenga kizazi cha vijana
wasio na utashi na uwezo wa kujenga hoja na kuhoji hata masuala nyeti nay a msingi
kwa mustakabali ya nchi yetu. Kutokana na hili nadiriki kusema Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaam kimepoteza hadhi yake ya kujikosha kama Chuo Kikuu na ijulikane
tu kama Chuo Cha Dar es Salaam kwani kuendelea kuweka neon “Kikuu” ni
kudhalilisha taaluma zetu na kubariki kile kinachofanywa na wanafiki na
wazandiki waliohodhi madaraka ndani ya taasisi hii.
Pia nitoe rai kwa
wanafunzi wa Chuo hiki kufanya mambo makuu mawili kuonyesha kutokubaliana na
hali hii inayoratibiwa na kufanywa na haya madubwanya na mafisadi wakubwa wa
mawazo ya vijana.
Mosi, kutojihusisha
kabisa na masuala yote yanayohusu upatikanaji wa serikali ya wanafunzi, yaani
kutojitokeza kuchukua form za kugombea nafasi yoyote siku uchaguzi wa serikali
ya wanafunzi utakapotangazwa. Hii ni kuonyesha kwamba hatuwezi kutafuta nafasi
ambazo kiongozi hayupo huru kuwatumikia wanafunzi na kufanya kazi kwa mujibu wa
katiba iliyopo bali kwa matakwa ya walowezi wa utawala.
Pili, Kutochangia kiasi
cha Tsh. 10,000 ambayo inalipwa kila mwaka kama ada ya DARUSO kwani hakuna haja
ya kutoa mchango kwa chombo ambacho hakifanyi kazi kwa uhuru na kwa kuwatumikia
wanafunzi bali kwa kuwaabudu na kufuata taratibu za walowezi watawala hata kama
ni kinyume na taratibu na yanakiuka katiba ya DARUSO. Kwa kufanya hivi tutakuwa
tumezuia matumizi haya mabaya ya rasilimali za umma ambazo zinatumiwa na
taasisi hii isiyokuwa na manufaa yoyote kwa walengwa.
Vijana wenzangu mliopo
ndani ya taasisi hii, niwache na ujumbe huu kwa leo “….We have no alternative than to
apply ourselves scientifically, physically and objectively to the problems
facing our nation. We have to think about poverty, embezzlement of public
resources, disobeys of rules and procedures and misuse of public resource that
is taking place in every sector of our nation. From that context let us think
on what best we can do for our nation to alleviate these….”
Asante sana
By Comrade Ole
0 comments:
Post a Comment