Music

Friday, December 5, 2014

KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA


Enyi ndugu wazalendo, Nahubiria hadhara
Tuzidi kukaza mwendo, Kuongoza msafara
Uongozi ni vitendo, Si fujo wala papara
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali

Napuliza vuvuzela, Kusema kwa ukaidi
Msinizuge kwa hela, Kura yangu siinadi
Viongozi mna hila, Ondoeni itikadi
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali
Mashavu yamewavimba, Viti mwaviona tamu
Matumbo sawa na mimba, Kazi kula vya haramu
Najitosa kwenye dimba, Nieleze mufahamu
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali
Mmezoea kusema, Maneno yaso busara
Hamna utu na wema, Raia twagaragara
Nia zenu sio njema, Bungeni ni mishahara
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali
Uongozi wa tamaa, Ulobeba ubinafsi
Mkatuwacha na njaa, Kutudhulumu nafusi
Kata kata nakataa, Nyoyo zenu ni nyeusi
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali
Msidhani tuna chongo, Twaona mnayofanya
Tumefunguka mabongo, Acheni kutudanganya
Kura sipigi kwa hongo, Komeni ninawakanya
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali
Sitaki kusema sana, Nikapigwa marufuku
Nakutumiwa vijana, Kunijaza dukuduku
Kura yangu naibana, Mpaka siku ya sanduku
Uchaguzi wanukia, Nampa anotujali

0 comments:

Post a Comment